Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Friday, August 16, 2013

Dk. Shein azindua sherehe za miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar
Na Rajab Mkasaba, Ikulu
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewataka wananchi kushiriki kikamilifu na kuonesha umoja na mshikamano walionao katika sherehe za miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar ambazo kilele chake kitafanyika tarehe 12 Januari 2014.
Dk. Shein aliyasema hayo leo katika risala maalum aliyoitoa kwa wananchi kupitia vyombo vya habari ikiwa ni kwa ajili ya uzinduzi wa sherehe za miaka 50 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Katika risala hiyo ya uzinduzi, Dk. Shein alisema kuwa sherehe hizo ni za kila mmoja na si za Serikali pekee yake wala chama fulani, bali ni za kila mwananchi awe mmoja mmoja au kwa makundi huku kusisitiza kuwa kila mtu ana wajibu na haki ya kushiriki katika sherehe hizo kwa namna utaratibu utakavyoelekeza.
“Hizi ni sherehe zetu, kwa hivyo huu ni wakati mzuri wa kuonesha umoja na mshikamano wetu nchini tuzingatie usemi usemao ‘Mtu lake, hawezi kumwachia mwenzake kwa hivyo na sisi shughuli hii yetu inahitaji kila mmoja wetu ashiriki’,alisema Dk. Shein.
“Miezi mitano ijayo, yaani ifikapo tarehe 12 Januari, 2014 Mapinduzi yetu yatakuwa yamefikia miaka 50 sawa na nusu karne, bila shaka nusu karne hii ya Mapinduzi inatufikia wakati nchi yetu ikiwa imepiga hatua kubwa za kimaendeleo na kuimarika kwa amani, utulivu, umoja na mshikamano.”alieleza.
Aidha, Dk. Shein alieleza kuwa ni dhahiri kuwa matunda ya Mapinduzi ya Zanzibar ndani ya kipindi cha miaka 50 yanabainika wazi wazi katika kila sekta na nyanja za maisha iwe ni serikalini au ndani ya jamii.
Aliendelea kueleza kuwa wananchi wanapaswa kujivunia na kuyathamini mafanikio hayo ya Mapinduzi nchini kwa vitendo.
Pia, alieleza kuwa hatua kubwa ya maendeleo iliyofikiwa ni ithibati na kielelezo muhimu cha ufanisi kwa wale wote wanaoikumbuka Zanzibar ilivyokuwa kabla ya Mapinduzi Matukufu ya mwaka 1964 na kuwataka wananchi kuyaimarisha maendeleo hayo na kudumisha hali ya amani na umoja wetu
Dk. Shein alitoa wito kwa wananchi wote, taasisi za Serikali ambazo tayari zimeshaelekezwa, taasisi zisizo za kiserikali pamoja na mashirika na kampuni binafsi kushiriki kikamilifu kwa hali na mali katika kufanikisha sherehe hizo.
Dk. Shein alisisitiza kuwa katika sherehe za miaka 50 ya Mapinduzi Matukufu, Serikali imejipanga kufanya mambo mbali mbali katika kipindi hichi cha miezi mitano kabla ya kufika kilele hapo Januari 12, 2014, huko katika Uwanja wa Amaan mjini Zanzibar.
Alisema kuwa Serikali imetoa muongozo wa namna sherehe hizo zitakavyofanyika katika maeneo mbali mbali ya visiwa vya Unguja na Pemba kwa shamra shamra na mvuto wa kipekee.
“Leo tarehe 15. 8.2013 nachukua fursa hii kutamka kwamba Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 50 ya Zanzibar yamezinduliwa rasmi. Nakutakieni nyote ushiriki na maandalizi mema”,alieleza Dk. Shein.
Pamoja na hayo, Dk. Shein alisema kuwa sherehe hizo zinakwenda na kauli mbiu isemayo “Tuimarishe Amani, Umoja na Maendeleo-Mapinduzi Daima” na kusisitiza kuwa kauli mbiu hiyo itawashajiisha wananchi wote kujivunia amani na umoja uliopo sambamba na hatua kubwa ya maendeleo iliyofikiwa.
Alieleza kuwa jambo la msingi ni kulinda amani, kudumisha umoja na kuthamini, kuyaenzi na kuyaimarisha maendeleo yaliopatikana huku akiwataka wananchi kutambua kuwa mambo hayo ni hazina muhimu kwa mustakbali mwema wa Wazanzibari na Watanzania wote waliopo na watakaokuja baadae.
Zanzinews

No comments :

Post a Comment