dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Friday, February 27, 2015

Chenge akwaa kisiki Escrow.

Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge.


  Akimbilia Mahakama Kuu.



Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge, jana ‘alikwaa kisiki’ baada ya Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma kutupilia mbali pingamizi lake aliloliwasilisha juzi kuzuia kusikilizwa kwa shauri lake kuhusiana na tuhuma za kukiuka sheria ya maadili ya viongozi wa umma.
Pamoja na mambo mengine, Chenge, ambaye ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali mstaafu, anatuhumiwa kwa kujipatia mgawo wa Sh. bilioni 1.6 kutoka kwenye fedha zilizochotwa kifisadi katika akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kinyume cha maadili ya viongozi.
Katika pingamizi lake, Chenge alidai mbele ya baraza hilo juzi kuwa amri ya Mahakama Kuu inazuia mamlaka zozote kujadili au kulifanyia kazi suala lolote linalohusu kashfa ya akaunti hiyo.
Kutokana na hali hiyo, hakuhojiwa baada ya Baraza kutenga siku moja ya kuipitia amri ya zuio hilo la mahakama kabla ya kutoa uamuzi juu ya pingamizi hilo.
Akitoa uamuzi huo jana, Mwenyekiti wa Baraza hilo, Jaji mstaafu, Hamisi Msumi, alisema zuio hilo la mahakama halilihusu wala kulizuia baraza kufanya kazi yake, isipokuwa Bunge, wasaidizi wa sheria au mawakala wanaofanya kazi za kisheria.
Baada ya Jaji Msumi kutoa uamuzi huo, Chenge hakukubaliana nao na kusema anakata rufaa ya kwenda Mahakama Kuu kuomba mwongozo wa mahakama juu ya kuendelea kujadiliwa suala hilo au la.
“Sitaki kubishana na maamuzi yaliyotolewa na Baraza, lakini nafikiri wanasheria wa baraza hili wangejaribu kwenda masjala kusoma zaidi, naamini wangeelewa hili ninalozungumza. Ninakubaliana na maamuzi, lakini naomba nikate rufaa, niende Mahakama Kuu kwa ajili ya kupata mwongozo zaidi juu ya suala hili,” alisema Chenge.
Waandishi wa habari walipotaka kufahamu sababu za yeye kukata rufaa muda mchache baada ya kutoka katika baraza hilo, Chenge alikataa kuzungumza.
Kufuatia uamuzi huo wa Chenge, Jaji Msumi alisema wanamruhusu kwa hatua yake hiyo aliyoamua kuichukua kwa kuwa ni haki yake kisheria kufanya hivyo.
Alisema hata kama ataenda Mahakama Kuu kuomba rufaa, shauri lake lipo palepale,  baraza litasubiri uamuzi utakaotolewa na mahakama ili kujua nini la kufanya.
“Ameomba kukata rufaa kwenda Mahakama Kuu na sisi tumemruhusu kwa kuwa ni haki yake kisheria, ila shauri lake bado tunalo, tunachosubiri na uamuzi utakaotolewa na mahakama kuendelea na shauri lake au la,” alisema Jaji Msumi.
Wakati Chenge akiwasilisha pingamizi hilo juzi, kulizuka mvutano mkali wa kisheria baina ya wanasheria wa baraza hilo na Chenge, ambaye alilitadharisha kutokubali kuingia kwenye siasa, badala yake waiache majukwaani na washughulikie masuala ya msingi kisheria.
Chenge alidai ana maelezo ya kutosha ya tuhuma zilizoorodheshwa na baraza hilo dhidi yake, lakini kabla ya kuanza kujieleza ni vyema akapata mwongozo.
Mvutano huo ulizuka muda mfupi baada ya Mwanasheria wa Baraza hilo, Hassan Mayunga, kusoma hati yenye malalamiko 10 dhidi ya Chenge, yakiwamo ya ukiukwaji wa Sheria ya Maadili ya Umma tangu akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) mwaka 1995.
Baada ya kusomewa malalamiko hayo, Chenge aliomba mwongozo wa baraza akidai kuna zuio la mahakama kwa mamlaka zozote za serikali kushughulikia suala hilo.
MVUTANO ULIKUWA HIVI
“Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mwongozo. Malalamiko dhidi yangu chimbuko lake ni maamuzi ya Bunge katika mkutano wa 16 na 17. Ninavyofahamu mimi suala hili lipo mbele ya Mahakama Kuu na uamuzi umeshatoka kuwa mamlaka yoyote hairuhusiwi kushughulikiwa kwa namna yoyote ile,” alisema Chenge.
Aliongeza: “Hii ni ‘public document’ (waraka wa umma) bila mwongozo huo, mimi kama mwanasheria inanisumbua sana.”
Baada ya kauli hiyo, Jaji Msumi aliomba kuona zuio hilo.
" Naomba hilo zuio nilione…nimelisoma kwa uchache, je mnalo hili?, Alihoji.
Mwanasheria Mayunga: Nimelisoma na halituzuii kuendelea na malalamiko yetu dhidi ya Chenge. 
Mayunga alipinga mwongozo huo na kudai zuio la mahakama halihusiani kwa namna yoyote na malalamiko yaliyo mbele ya baraza dhidi ya Chenge.
“Tuhuma zilizopo mbele ya baraza ni ukiukwaji wa sheria na kanuni za maadili ya viongozi wa umma na siyo suala la kinachoendelea na kilichoelezwa katika zuio hilo, hivi ni vitu viwili tofauti,” alifafanua.
Mayunga alidai kwa mujibu wa Ibara ya 132 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Sekretarieti ya Maadili ya Watumishi wa Umma inatajwa ikiwa  na mamlaka kamili ya kuhoji na kwa msingi huo iko huru na haipaswi kuingiliwa.
Alifafanua kuwa Sheria ya Maadili kifungu cha 18 (2) (c) inaeleza majukumu ya sekretarieti ambayo ni kuchunguza madai yoyote ya uvunjaji wa sheria ya maadili.
Mayunga alidai kuwa kifungu cha 4 kinatoa mamlaka kwa sekretarieti kuanzisha uchunguzi na ukiukwaji wowote wa maadili kulingana na matakwa ya sheria.
Alisema kifungu namba 29 cha sheria hiyo pia kinaeleza hakuna chombo kinachoweza kupunguza au kuzuia kufanya kazi yake na kwamba kwa vifungu hivyo Baraza hilo liko sahihi kuendelea na shauri hilo. Baada ya ufafanuzi huo, Chenge alisema anachofahamu hoja aliyoiwasilisha mbele ya baraza ni zuio lililopo Mahakama Kuu na kwamba iwapo chombo hicho (Baraza) kipo juu ya Mahakama hilo ni jambo jingine.
Hata hivyo, alitakiwa kusoma kipengele kimojawapo cha zuio hilo na kutafsiri kwa lugha ya Kiswahili na alifanya hivyo huku akisisitiza moja ya kipengele ni kuhusu miamala ya benki iliyofanyika.
“Nionavyo chombo hiki (Baraza) kiheshimu amri halali iliyotolewa na Mahakama…unapokuwa katika hali kama hii Mamlaka ya chombo hiki yasiwe makubwa kushinda Mahakama Kuu…ni ushauri tu unaweza kuendelea kunihoji na maelezo ninayo ya kutosha,” alisema. 
Aliongeza: “Utawala wa sheria uheshimiwe, masuala ya siasa yabakie kwenye majukwaa mengine yasiingizwe kwenye chombo hiki.”
“Kilichotajwa kwenye malalamiko dhidi yangu ni miamala ya benki ambayo imetajwa katika zuio la Mahakama, tusijifiche katika kichaka cha kusema sheria ya maadili inafanya kazi, suala hili lilianzia bungeni,” alisisitiza.
 Mwanasheria wa Baraza, Filoteus Manula, alidai suala la ukiukwaji wa maadili haliendani na mashauri kama ya jinai, madai na rushwa, na kwamba kinachozungumziwa kwenye malalamiko ni ukiukwaji wa maadili aliyoyafanya tangu akiwa na wadhifa wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali. 
Mwanasheria mwingine wa Baraza, Getrude Cyriucus, alidai kuwa sekretarieti hiyo imepewa mamlaka ya kuanzisha uchunguzi bila kusubiri na wapo huru kuanzisha kuchunguza kupitia taarifa mbalimbali ikiwamo vyombo vya habari.
“Tukiacha viongozi wa umma wajichagulie watakavyo, kamwe hatuwezi kufanya kazi yetu inavyotakiwa,” alidai.
Baada ya mvutano huo wa dakika 30, Chenge alisema alichoomba ni mwongozo na kuwasilisha mbele ya baraza zuio la mahakama, hivyo waamue kama wataendelea au la na kwamba ana maelezo ya kutosha dhidi ya tuhuma zilitotolewa dhidi yake.
 MALALAMIKO DHIDI YA CHENGE 
Chenge akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali mwaka 1995, aliishauri serikali kuingia mkataba wa miaka 20 na Kampuni ya Independent Power Solution Limited (IPTL) wa kuongeza uzalishaji wa umeme.
Pili, baada ya kustaafu wadhifa wake huo, Desemba 24, mwaka 2005, mwaka 2006, aliingia mkataba wa kuwa Mshauri Mwelekezi (Consultant) wa Kampuni ya VIP Engineering  and Marketing Limited iliyokuwa na hisa za asilimia 30 kwenye kampuni ya IPTL.
Tatu, kitendo cha mlalamikiwa (Chenge) kuingia mkataba na kampuni hiyo ya VIP iliyokuwa na hisa na kampuni ya IPTL ni ukiukwaji wa sheria ya maadili ya viongozi wa umma, kifungu cha 6 (j) ambacho kinazuia kiongozi wa umma kujinufaisha utumishi wake uliopita kwa kutumia taarifa alizozipata alipokuwa anatekeleza majukumu yake kwa manufaa binafsi.
Nne, kitendo cha mlalamikiwa kuendelea kuwa mshauri mwelekezi wa Kampuni ya VIP akiwa na wadhifa wa ubunge, ni ukiukwaji wa sheria ya maadili ya viongozi wa umma kifungu cha 6 (e) ambacho kinazuia kiongozi wa umma kujiingiza katika mgongano wa kimaslahi.
Tano, mkataba ambao mlalamikiwa aliingia na VIP ulimpatia manufaa ya kifedha ya Sh. bilioni 1.617 kinyume cha sheria ya maadili ya viongozi wa umma kifungu 12 (1) (e).
Sita, Chenge aliingiziwa fedha hizo Februari 5, mwaka 2014 katika akaunti yake 00120102523901 iliyopo kwenye benki ya Mkombozi, tawi la Mtakatifu Joseph, Dar es Salaam.
Saba, kitendo cha mlalamikiwa kuingia mkataba na Kampuni ya VIP ambayo ilikuwa na hisa na IPTL aliisaidia kujipatia manufaa ya kifedha kinyume cha sheria ya maadili ya viongozi wa umma kifungu cha 12(1) (e).
Nane, mlalamikiwa hakutamka maslahi aliyonayo katika mkataba na VIP aliyoingia nayo mkataba mwaka 2006, kwa mujibu wa sheria ya maadili ya viongozi wa umma kifungu cha 15.
Tisa, mlalamikiwa hakutamka maslahi aliyokuwa nayo katika mkataba wa Tanesco na IPTL kupitia VIP kinyume cha fungu la 18 la sheria ya maadili.
Kumi, mlalamikiwa hakutamka madeni yake aliyokuwa inaidai kampuni ya VIP kwa kamishna wa maadili kinyume cha matakwa ya kifungu la 9 (6) ya sheria ya maadili ya viongozi ya umma.
KAULI YA BARAZA
Baada ya baraza kusikiliza mvutano huo, Jaji Msumi alisema watakwenda kusoma zuio hilo kwa kina na kutoa maamuzi leo.
“Najua tuna madaraka, lakini kama kuna zuio la Mahakama Kuu basi baraza haliwezi kuendelea na suala hili kwa kuwa haliko juu ya sheria,” alisema.
MALALAMIKO YA WANASHERIA
Baada ya Mwenyekiti kuahirisha kikao hicho, wanasheria wa baraza hilo walilalamika mbele ya waandishi wa habari kuwa walisoma zuio hilo kabla ya kuandaa malalamiko dhidi ya Chenge na nakala waliyokuwa nayo ina kurasa tatu, lakini iliyowasilishwa na Chenge ina kurasa saba, jambo ambalo halieleweki.
 KWA NINI CHENGE ANAPINGA
Chenge anapambana dhidi ya tuhuma mbele ya baraza kwa kuwa ikithibitika kuwa alikiuka maadili, anaweza kuathirika kisiasa hasa kwenye kinyang’anyiro cha ubunge baadaye mwaka huu.
Hata hivyo, kushindwa mbele ya baraza kunaweza kuibua kesi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwamba alikwepa kodi, hivyo kuingia kwenye mgogoro wa kikatiba. 
Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 ibara ya 67 (c) inataja mambo yanayoweza kumpotezea mtu sifa ya kuwania ubunge kuwa ni kutiwa hatiani kwa kukwepa kodi ya serikali katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Kushindwa mbele ya baraza kunaweza kuwa mwanzo wa kesi hiyo.
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment