dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Tuesday, April 28, 2015

TANZANIA: Urais wauzwa kwa bilioni 20

• Masikini sasa shauri yao
• Mgombea adai hali inatisha
• Wenye fedha hiyo wako CCM

MMOJA wa wanasiasa wanaotajwa kutaka kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu amedai kwamba mshindi atakayepatikana atakuwa ametumia walau shilingi bilioni 20.
Fedha hizo zinajumuisha malipo ya hongo kwa wajumbe wa Halmashauri Kuu na Mkutano Mkuu wa chama chake, malipo kwa wapambe mbalimbali, malipo kwa ajili ya vifaa na zana za kampeni, malipo kwa ajili ya matangazo kwenye vyombo vya habari na malipo mengine yaliyopewa jina la “ matumizi maalumu”.
Raia Mwema limeambiwa kwamba mojawapo ya kazi maalumu ambazo zinafanyika mwaka huu ni zile za kuchafua wagombea pinzani kwa kutumia vyombo vya habari na njia nyingine; huku watakaotumika wakiwa wanalipwa kwa kazi hiyo.
Akizungumza katika mahojiano na gazeti hili, Mbunge wa Wawi (CUF), Hamad Rashid Mohamed, alisema Watanzania wanapaswa wajiangalie vizuri kwa sababu sasa siasa zimevamiwa na watu wenye maslahi tofauti na yale ya Taifa na wako tayari kutumia gharama yoyote kupata wanachotaka.
Hamad ambaye aliwahi kuwa waziri katika Serikali ya Awamu ya Kwanza na ya Pili, na baadaye Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni katika Bunge la Tisa, anasema wagombea ambao wana uwezo huo wa kifedha kwa sasa ni wanaotoka Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Ngoja nikupe mfano mdogo tu. Kuna mmoja wa wanaotajwa kuwania urais kupitia CCM alidaiwa kugawa kiasi cha shilingi bilioni 1.5 wakati wa mojawapo ya sherehe za mwishoni mwa mwaka hapa nchini. Kama mtu anatumia bilioni 1.5 kwa sikukuu moja tu, hebu chukulia kwamba anafanya hivyo mara nne kwa mwaka kwa maana ya sikukuu mbili za Wakristo na mbili za Waislamu. Jumlisha na mwaka mpya.
“Jumla hapo unapata shilingi bilioni 7.5 kwa mwaka mmoja. Sasa hapo jumlisha malipo anayolipa kwa watu wake mbalimbali wanaomfanyia kazi katika mitandao ya kijamii na magazeti ambayo hakuna anayejua ingawa ni kiwango kikubwa pia.
“CCM ikiruhusu waanze kujitangaza rasmi, itabidi waanze kulipia matangazo makubwa katika vyombo vyote vya habari vya ndani na nje ya nchi. Na hapo ndipo waziwazi wataanza kuwahonga wajumbe zaidi ya 1,000 wa Mkutano Mkuu ambao watakuwa tayari kupiga kura. Hapo atakayeshinda ni yule atakayehonga zaidi kuliko wengine. Usisahau kwamba wapo ambao itabidi watumie helikopta wakati wa kutafuta saini za wanachama wanaohitaji,” alisema.
Hamad ambaye sasa anahusishwa na chama cha Alliance for Democratic Change (ADC) kutokana na mgogoro alionao ndani ya CUF, alisema kwa vyovyote vile, uchaguzi wa mwaka huu utakuwa wa gharama kubwa kuliko mwingine wowote uliopata kufanyika katika historia ya Tanzania.
Kwenye mahojiano hayo, Hamad alisema kwamba huu ni mwaka ambao Watanzania wanatakiwa kutoa ujumbe mzito kwa watu wanaotumia fedha au kufanya fedha kama msingi wa uongozi bora kwa kuwakataa kwenye uchaguzi.
Hamad alisema anaweza kuamua kuwania urais wa Zanzibar badala ya ule wa Muungano kwa sababu anaamini anakubalika zaidi; ingawa amekadiria kwamba mgombea atakayeshinda atatakiwa kutumia walau kiasi cha shilingi bilioni mbili katika uchaguzi huu.
“ Mimi nimelelewa ndani ya CCM na kule tulikuwa tukifundishwa kwamba fedha si msingi wa maendeleo, lakini leo hiyo ndiyo inaonekana sifa ya mtu kuwa kiongozi. Watanzania wanatakiwa wawakatae watu wa namna hii mwaka huu. Kama tukiruhusu tu, huo utakuwa mwisho wa mtu masikini kutawala Tanzania hata kama atakuwa ndiye mgombea bora,” alisema.
Akizungumzia maelezo hayo ya Hamad, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Profesa Kitila Mkumbo, alisema ingawa kiasi kilichotajwa ni kikubwa, hawezi kukataa kwamba kuna watu wanaotaka urais walio tayari kutumia hata kiasi hicho kwa ajili ya kushinda.
“Kilichopo hapa ni kwamba hizi fedha zinaweza zisiwe za mgombea peke yake, bali makundi ya nje kama wafanyabiashara na makampuni ya kigeni ya kimataifa ambayo pengine yatataka kumdhibiti rais ajaye na waendeleze uvunaji wao wa rasilimali pasipo matatizo.
“ Kwa uzoefu wangu, wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 chama nilichokuwamo cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kilitumia takribani shilingi milioni 700 hivi kwenye uchaguzi huo. Na hizo ni rasmi, na inawezekana kuna matumizi mengine ambayo yanaweza kuongeza kiasi hicho,” alisema Kitila.
Tanzania ina Sheria ya Gharama za Uchaguzi iliyosainiwa kwa mbwembwe na Rais Jakaya Kikwete mnamo Machi mwaka 2010, kwa lengo la kudhibiti matumizi ya kiasi kikubwa cha fedha wakati wa chaguzi za hapa nchini.
Aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, aliwahi kuonya kwamba sheria hiyo haingekuwa na uzito uliotarajiwa kwa sababu ilitengenezwa katika mazingira yasiyo na uhalisi na hali iliyopo nchini kwa sasa.
Hadi sasa, takribani miaka minne baada ya kufanyika kwa uchaguzi wa mwaka 2010, bado Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kupitia kwa Msajili wake, Jaji Francis Mutungi, imeshindwa kutoa hesabu za gharama zilizotumika katika uchaguzi kwa sababu ambazo hazijawekwa wazi hadi leo.
Ofisi hiyo ndiyo yenye jukumu la kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Vyama vya Siasa namba tano ya mwaka 1992 na Sheria ya Gharama za Uchaguzi namba saba ya mwaka 2010 katika chaguzi zote zinazofanyika nchini.
Gazeti hili lina taarifa kwamba ofisi hiyo imeshindwa kufanya kazi hiyo kutokana na upungufu wa wataalamu wa hesabu ambao wangeweza kufanya vizuri kazi ya kukokotoa gharama hizo kwa mujibu wa sheria iliyopo.

1 comment :

  1. Kama ningelikuwa ninazo bilioni 20 basi nami ningelijitia kwenye kinyang'anyiro cha urais kwa mwaka huu wa 2015 kupitia chama chochote kile.
    Ukijumlisha safari za Kikwete nje peke yake kwa mwaka huu ni zaidi ya bilioni 50, sasa kutoa bilioni 20 ukapata bilioni zaidi ya 50 umekosa nini?
    Pia, usisahau, ikiwa Pinda anapokea 26 milioni kwa mwezi, je, Rais atapokea ngapi, ukiacha marupurupu mengineneyo?

    ReplyDelete