dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Thursday, May 28, 2015

CCM inavyojikwaa kupata wagombea


  • Mungu ametupa akili, busara na hekima, kisha akatupa ufahamu, fikra na uwezo wa kuunda taasisi ili zitusaidie kuturatibu, kutuwezesha na kutusaidia. 
  • Leo hii nidhamu ya baadhi ya wana CCM na viongozi imeshuka,  hata kuzomeana kumo katika vikao. Kuheshimiana miongoni mwa viongozi ndiyo msingi mkubwa wa kujengeana imani na kuaminiana.
Uongozi ni dhamana, ni jukumu zito, mtu hupewa uongozi na watu. Uongozi hautafutwi kwa udi na uvumba.
Dini zote na jamii za watu katika historia, viongozi walitengenezwa. Hata wale waliozaliwa katika mnyonyororo wa uongozi iliwapasa kulelewa kiuongozi.
Ilimpasa kiongozi kuhakikisha kwamba anawaleta watu wake pamoja, maskini na matajiri, wakulima na wafanyakazi, wafanyabiashara wadogo na wakubwa.
Kiongozi anapaswa kuwa msingi imara wa umoja wa kitaasisi, jamii na taifa kwa jumla. Kiongozi anayeanza na mpasuko badala ya umoja, hana ishara nzuri kwa Taifa.
Kiongozi anayeanza na chuki badala ya  upendo, makundi badala ya  taasisi, tafsiri yake siyo njema kwa Taifa. Huyu hana tija na anaendeleza  nyufa katika taasisi.
CCM na wagombea
Juzi, Chama cha Mapinduzi (CCM) kimetoa utaratibu na mchakato wa kumpata mgombea wake wa urais.
Tukumbuke CCM ndiyo chama kilichopo madarakani sasa, hivyo inapaswa kuonyesha mfano, kinapaswa kuwa kioo.
Najua CCM imejikwaa wakati mwingine kwa makusudi na wakati mwingine kwa bahati mbaya.
Sifa kubwa ya uongozi thabiti ni kuonyesha uongozi pale na watu ndani ya taasisi au kwa ujumla taasisi inapojikwaa.
Kuonyesha uongozi kunaweza kuwa katika namna nyingi, mojawapo ni kwa hali yoyote kuukumbatia ukweli pasina kuathiri menejimenti ya siasa.
Uongozi ni kuonyesha kutovunjika moyo, kutokukata tamaa. Kujikwaa siyo kuanguka na kama CCM imetetereka bado inaweza kuamka tena na kuthibitishia umma wa Watanzania kwamba misingi ya kusimamia maadili na miiko ya viongozi bado, iko imara kama ilivyo misingi iliyokiasisi chama.
Nitoe mfano wa mambo kadhaa ambayo kwa makusudi baadhi ya wana CCM wamesaidia kukiteteresha.
Mosi, chama kinavyoshughulikia masuala ya ubadhirifu wa mali ya umma tangu kuanza kwa tuhuma kadhaa katika miaka 10 iliyopita.
Tumeona uwajibikaji, lakini CCM ingeweza kufanya vizuri zaidi ili kurudisha imani ambayo inaonekana dhahiri kutetereka miongoni mwa wananchi.
Uongozi wa chama hicho tawala, unapaswa kuwa mkali zaidi kwa wale wanaokwenda kinyume na misingi ya kuanzishwa kwake. Urafiki ni jambo jema, lakini misingi yake inapaswa kuwa juu ya urafiki wakati wowote.
Viongozi wa CCM waliokuwapo kipindi cha Mwalimu Julius  Nyerere,  wengi ni mashahidi wa namna alivyotenda kama kiongozi.
Mwalimu alikuwa mkalimu lakini pia alikuwa kama baba; alikuwa msikivu na mpole, kama kiongozi mkuu ndiyo mwenye dira, ndiye anayetupa hamasa kupiga makasia katika bahari iliyochafuka ili tuelekee uelekeo sahihi na salama.
Leo hii nidhamu ya baadhi ya wana CCM na viongozi imeshuka,  hata kuzomeana kumo katika vikao. Kuheshimiana miongoni mwa viongozi ndiyo msingi mkubwa wa kujengeana imani na kuaminiana.
Viongozi wasioaminiana, hawaheshimiani, viongozi wasioheshimiana hawapendani na wasiopendana hawazungumzi kwa uwazi na ukweli.
Zamani ilikuwa tunasema zidumu fikra za mwenyekiti, usemi huu haukuwa wa bahati mbaya, ni kwamba kiongozi alilitizama Taifa na akatuhamasisha kupiga juhudi kuelekea kule wananchi wetu wanapopaswa kuwa yaani kule kwenye nchi ya maziwa na asali.
Leo hii fikra za mwenyekiti siyo jambo tena, inaweza isiwe kama kipindi kile cha zamani, lakini sidhani kama mwenyekiti anapewa heshima yake kama kiongozi.
Dhihaka ya Katiba
Mchakato wa Katiba, umekuwa dhihaka kwa Watanzania. Mwenyekiti wa CCM ambaye ndiye mkuu wa nchi alianzisha mchakato wa kuandikwa Katiba Mpya kwa masilahi ya Taifa.
Nini kilitokea katika kusimamia fikra yake hii adhimu na adimu kwa Taifa letu? Mzaha kabisa. Wako waliohoji, ninaposema kumhoji simaanishi katika namna ya heshima ya kutaka taarifa au maelezo kutoka kwa kiongozi, bali katika namna ya kiburi, dharau na ujuvi usio na tija kwa chama hicho na kwa Taifa.
Mwenyekiti alikosa uungwaji mkono ndani ya chama katika jambo lililokuwa na masilahi kwa Taifa. Naikumbuka dhamira yake, nayakumbuka maono yake, nayasoma maandiko yake, nasikiliza hotuba zake, kwa hakika kilichokuja kuwa Katiba inayopendekezwa hakiakisi dhamira ile ya awali.
 CCM isipochukua uamuzi wa haraka kutoa uongozi katika mchakato wa Katiba na uchaguzi mkuu, hii haitakuwa ishara nzuri ya chama kuimarika na kukua kiuongozi.
Hebu tufuatilie kalenda hii; Tume ya Uchaguzi (NEC) imesema itamaliza kuandikisha wapiga kura julai 16, kisha utafuata uhakiki wa orodha kwa Mkoa wa Dar es Salaam na mikoa mingine itakuwa imemaliza au inamalizia zoezi la uhakiki.
Ikumbukwe pia kwa desturi Bunge huvunjwa mwezi wa Julai, na imekuwa desturi kwamba kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani huanza kwenye tarehe 20 Agosti mpaka siku ya uchaguzi ambayo huwa wiki ya mwisho ya mwezi Oktoba.
Mpaka leo, hakuna muswada wowote wa kurekebisha Katiba ya mwaka 1977 ambao kuna fununu au ambao imejulikana kwamba utapelekwa bungeni ili kutekeleza ‘makubaliano ya Rais na viongozi wa vyama’ kupitia Kituo cha Demokrasia ( TCD).
Sitaki kusema kwamba tunakwenda kwenye Uchaguzi Mkuu bila marekebisho ya Katiba ya mwaka 1977, kwa maana siyo kila yanapotanda mawingu, yaje na mvua.
Katika hili lazima CCM ionyeshe uongozi, mkishindwa katika hili, mimi nitaendelea kupenda misingi ya kuanzishwa chama chenu ila heshima ya viongozi wetu katika chama kama taasisi itakuwa inakaribia ukingoni. Tusifike huko.
Viongozi wetu, wenye dhamana katika CCM nawaombea mkaongozwe na hekima ya Kimungu. Mkawatazame viongozi wenye nia ya kushika hatamu ya taifa letu kwa macho ya Kimungu na siyo vinginevyo.

Mkifanya uamuzi mbaya, mtakivuruga chama chenu, wanachama na Watanzania watahuzunika, mtatuachia matatizo. Leo hii sura ya CCM haijatukuka katika kiwango chake, watu wetu wana maswali zaidi kuliko majibu.

No comments :

Post a Comment