dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Thursday, October 8, 2015

Mchungaji Mtikila aagwa na Bendera ya Tanganyika.

Waombolezaji wakiuaga mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Democratic Party (DP), marehemu Mchungaji Christopher Mtikila, katika Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam jana. Picha: John Badi
Rais Jakaya Kikwete, jana aliongoza mamia ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kuuaga mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, ambaye jeneza lake lilipambwa kwa Bendera ya Tanganyika kwenye viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam, jana.
 
Mbali na Rais Kikwete, viongozi wengine waliohudhuria tukio hilo kabla mwili wa marehemu haujasafirishwa kwenda kwao mkoani Njombe ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mohamed Ghalib Bilal na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Maalim Self Shariff Hamad na viongozi wa vyama vya siasa na dini.

Akizungumza kabla ya kuagwa kwa marehemu, Dk. Bilal alisema Mtikila atakumbukwa kwa ujasiri wake wa kusimamia kile alichokuwa akikiamini na pia mchango wake katika siasa nchini.
 
Kadhalika, Dk. Bilal alisema kupitia harakati zake mbalimbali, Mtikila amesaidia kuudhihirishia ulimwengu ni kwa namna gani Tanzania inatoa uhuru wa kujieleza kwa wananchi wake.“Hata mimi nilikuwa napata wakati mzuri wa kuzungumza na marehemu Mtikila. Na wakati ule alikuwa akitoa mchango mkubwa sana kwa vyuo vikuu, hata pale tulipokuwa tukikwazana katika harakati zake hizo, bado tulikuwa tunapata muda wa kuzungumza na kumaliza tofauti zetu. Hivyo tunataka Tanzania inayoruhusu mawazo tofauti,” alisema Dk. Bilal.
 
Maalim Self alisema Mtikila alikuwa muwazi na ambaye hakuwahi kumuogopa mtu, na mara zote alipenda kusimamia kile alichokiamini.
 
Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, alisema Mtikila atakumbukwa kwa mchango wake katika masuala ya sheria kwa vyama hivyo, akiongeza kuwa ataenziwa kwa utii wa sheria pale alipopigania kile alichokiamini, hasa kwa kutumia vyombo vya sheria kudai haki pasipo kufanya maandamano.
 
Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Peter Kuga Mziray, alisema bado mchango wa Mtikilia ulikuwa unahitajika, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.
 
Makamu Mwenyekiti wa DP Zanzibar, Peter Mapwila, alisema wamepata pigo kubwa kumpoteza kiongozi wao na kwamba katika kumuenzi, wamepanga kuendeleza mambo ya msingi aliyokuwa akisimamia hasa uwapo wa Tanganyika.
 
Dada wa Marehemu, Maria Mtikila, pamoja na kushukuru kwa faraja ambayo wamepata kutoka kwa watu mbalimbali tangu kuondokewa na mpendwa wao, pia alisema Mtikila kwao alikuwa chachu ya familia, aliyetegemewa kwa mambo mbalimbali na kwamba wanamfananisha na nuru ambayo sasa imezimika.
 
Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufunuo Tanzania, Paul Bendera, alisema ni vema Watanzania wakajitambua na kuwa makini katika kuheshimu maisha ya mtu, kudumisha upendo, amani na uhuru wa maisha ya kila mtu.
 
Mchungaji Mtikila, pamoja na kujishughulisha na mambo mbalimbali, pia alianza kujikita katika masuala ya siasa miaka ya 1990 ikiwamo kuanzisha chama chake cha DP.
 
Akisoma wasifu wa marehemu, Victor Manyai, alisema Mtikila alizaliwa Juni 7 mwaka 1950 katika Kijiji cha Milo, wilayani Ludewa, mkoani Njombe.
 
Alifariki kwa ajali ya gari Oktoba 4, mwaka huu katika Kijiji cha Msolwa, mkoani Pwani wakati akitokea mkoani Njombe kwenye kampeni za uchaguzi za wagombea udiwani na ubunge wa chama chake katika Jimbo la Njombe Kusini. 
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment