Top Leaderboard Advert

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Zanzibar Diaspora

High class shops @ Fuoni

High class shops @ Fuoni

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Adsense Marquee

Thursday, March 31, 2016

Magufuli ajihadhari na “watumbua majipu” wa geresha!

MAKALA yangu ya mwisho ilionya dhidi ya kudhani kwamba matatizo yetu ni sawa na majipu na kuamini kwamba matatizo hayo yanaweza kuondoka kwa kutumbuliwa. Nilieleza kwamba ndwele inayotuumiza ni mithili ya saratani, na saratani haiwezi kuondoshwa kwa kutumbuliwa.

Kwa kutambua kwamba saratani hiyo ilikwisha kuenea katika mishipa yetu ya damu ya kitaifa na kusambaa mwili mzima, nilisema kwamba hatuna budi kutafuta dawa “mujarrabu” ambayo itaikausha na kuiondoa saratani hiyo kwa njia za kisayansi zaidi. Wiki hii ningependa kujieleza zaidi kidogo.

Matatizo tunayoyashuhudia leo katika “utumbuaji wa majipu” hayakuanza leo wala jana. Tumekuwa nayo kwa miaka mingi, na kwa kweli yamekuwapo hata kabla ya ukoloni, kabla Wajerumani wala Waingereza hawajafika hapa kuja kututawala.

Jamii zetu za jadi zilikuwa na matatizo kama tunayoyaona leo, na wala hakujatokea jamii ikawa haina watu waliojulikana kama wezi, walaghai, wanafiki, waongo, vizabizabina, ndumilakuwili, na kadhalika. Ukiambiwa kwamba kuna jamii kama hiyo, ujue unaambiwa uongo. Ninachokijua katika hili ni kwamba kuna jamii ambazo zimejenga utamaduni wa kuvumilia mambo kama hayo, na kuna jamii nyingine ambazo zimejijengea utamaduni wa kutovumilia uovu huo.

Hili ndilo alilokuwa akilizungumzia Mwalimu Julius Nyerere katika ile hotuba ambayo tunaonyeshwa mara kwa mara kwenye televisheni. Anachosema Nyerere ni kwamba msije mkadhani kwamba sisi katika utawala wetu hatukuwa na wezi na wala rushwa; tulikuwa nao, lakini kila tulipowabaini, tulishughulika nao sawa sawa, na hatukuwaacha wawe na amani.

Maana halisi ya Mwalimu ni kwamba ninyi watu wa siku hizi mnawajua wezi na wala rushwa, lakini mnawalea na kuwabembeleza. Haya maovu yanayotendeka yanatokana na mfumo mzima kujengwa juu ya misingi ya kuvumilia maovu ilhali mnayaona yakitendeka na mkijua kwamba yanayotendeka ni maovu. Hali hii inawasilisha “ufu” fulani ndani ya mifumo yetu ya utawala na uongozi wa nchi yetu.

Hapa ningependa kuwasuta wote waliomo katika mifumo hii ya utawala, na katika hili ninaweza nikajisuta hata mimi mwenyewe binafsi. Leo hii nawasikia watu waliokuwa na nafasi za dhamana katika serikali iliyopita wakiisema vibaya serikali waliyokuwa wakiitumikia kana kwamba wao hawakuhusika. Ukweli ni kwamba yeyote aliyekuwamo katika utawala mbovu anahusika na utawala huo na hawezi kuukana isipokuwa tu kwa unafiki.

Ingekuwa vyema kama tungejenga utamaduni wa kujiheshimu kuliko tunavyofanya leo. Mtu anakuwa amejenga heshima yake iwapo atajiuzulu kwa kuwa hakubaliani na mambo yanayofanywa na serikali anayoifanyia kazi kuliko kubakia humo hadi inapoondoka madarakani halafu ndipo aseme kwamba alikuwa anayatambua maovu ya serikali iliyopita; huo ni unafiki.

Nasema hivyo nikijua kwamba hata mimi mwenyewe niliwahi kufanya kazi ndani ya serikali ambayo ilifanya mambo mengi ambayo hayakunipendeza lakini ikanichukua muda mrefu kidogo “kuomba niruhusiwe” kuondoka. “Kuomba kuruhusiwa” kuondoka peke yake ni namna ya kukubali kwamba sikuchukua hatua ya kusema moja kwa moja kwamba serikali hii inazidi kuonekana akilini mwangu kama iliyojaa uozo.

Ningetakiwa niondoke mapema bila ya “kuomba kuruhusiwa,” lakini kwa sababu fulani fulani zilizotokana na utamaduni wetu, nikajikuta “naomba” na maombi yangu hayo yakaja kujibiwa takriban miezi tisa baadaye.

Kwa wengi wanaojikuta katika mazingira kama yangu, kinachowafanya wasite ni woga wa kuacha kazi wanayoiona ina “usalama” na kwenda nje wasikojua kuko vipi. Tunao ugonjwa wa akili wa kuamini kwamba hatuwezi kufanya lolote ila kwa kuajiriwa peke yake, hasa pale ajira yenyewe inapoambatana na “uheshimiwa “ feki na kupigiwa makofi kila ukiingia ukumbini.

“Uheshimiwa” wa aina hiyo, pamoja na makofi yake ni mkorogo wa ulevi mkali kuliko pombe ya gongo. Wengi waliouonja waliharibikiwa akili na wakakosa uwezo wa kufikiri sawa sawa. Hatimaye walipokuja kutemwa na mfumo waliouona kama baba na mama waliishi maisha ya majuto na kila siku kulalama. Na hao ni watu ambao kwa elimu kidogo waliyopata wangeweza kabisa kufanya kazi zao za zamani. 

Kwa bahati mbaya, mwalimu mzuri wa zamani wa shule ya msingi haoni kwamba anapopoteza kazi ya “uheshimiwa” anaweza kurejea kazi yake ya zamani na akawa mwalimu bora zaidi ya alivyokuwa awali kwa sababu kuna mambo mapya amejifunza katika huo “uheshimiwa” wake na ambayo yangewafaa wanafunzi wake.

Tumeona picha za Mahmoud Ahmedinejad, rais mstaafu wa Iran, akichukua usafiri wa umma kwenda kufundisha chuo kikuu kama alivyokuwa zamani, na sielewi ni nini kinawafanya “waheshimiwa” wetu wadharau taaluma zao. Ni hofu hiyo ya kupoteza “uheshimiwa” huo bandia ndiyo inawafanya hata wale wanaoona mambo ni ya hovyo serikalini wasipate “ujasiri” wa kutaka kuondoka.

Sababu nyingine ni “ufu” wa muda mrefu wa fikra. Mababu zetu walisomeshwa na wakoloni kwa lengo la kuajiriwa na wakoloni hao hao kama makarani wa kuendesha utawala wa kikoloni. Hakukuwa na wazo la watu kupata elimu ya kujitegemea hata pale sera zetu zilipodai kwamba ni za “Ujamaa na Kujitegemea”. Bado vijana wetu walikuzwa na mawazo ya utegemezi kwa dola, na dola iliendelea kuwa tegemezi kwa “wafadhili”.

Taratibu, tulijikuta sote tukitegemea kupata ujira wetu kutoka serikalini, hata pale tulipokuwa hatuna raha kufanya kazi serikalini kwa sababu akili zetu zote zilituelekeza kuamini kwamba hatuwezi kujiajiri, na kwa hiyo serikali na mashirika yake ndiyo kila kitu.

Ikafikia mahali ikawa sasa inakubalika kuwa katika ajira ya serikali, unayo ofisi ya serikali, unao mshahara wa serikali, unalo gari la serikali, unayo nyumba ya serikali (ambayo baadaye unaweza kugawiwa kama zawadi), una kila kitu cha serikali, lakini si lazima ufanye kazi ya serikali. Unaweza kwenda ofisini kila siku lakini kazi unayofanya huko ni kuendesha bishara zako, kwa kutumia nyenzo zote hizo za serikali, ikiwa ni pamoja na safari ghali za nje ya nchi

Katika hali kama hiyo, wewe kama mtumishi wa serikali unakuwa huna wajibu wo wote isipokuwa kuonekana kama mtu aliyemo ofisini kila siku hata kama unachofanya unakijua wewe mwenyewe. Katika mfumo uliojaa kulindana kla mmoja anamlinda mwenzake naye analindwa na wengine. Kam ni wizi, watafundishana. Kama ni kutetea maovu watateteana.

Ndiyo maana inakuwa vigumu kwa “mtumishi wa umma” kama huyo kusema anaacha kazi kwa sababu ya ufisadi, uzembe au ulaghai. Ataendelea na ajira hiyo hadi hapo atakapokuja mkuu mpya ambaye anaonekana ana mwelekeo tofauti, na huyu “mtumishi” ataanza kuimba sifa za huyu mkuu mpya na “kuponda” mambo aliyokuwa akiyafurahia chini ya mkuu wa zamani.

Hawa ni wanafiki wakubwa, na Rais Magufuli anao wengi miongoni mwa watu aliojizungusha nao. Sasa hivi kazi kubwa wanayofanya ni kumuiga katika kila analofanya. Watafanya ziara za kushitukia; watatoa maelekezo ya papo kwa papo. Watawasimamisha kazi maofisa; wataamuru uchunguzi ufanywe; wataonywa vikali na kutoa vitisho.

Na kila wanakoenda watasindikizwa na kamera za televisheni. Naomba radhi kwa wahusika, lakini hiyo si staili ya kufanya kazi serikalini. Serikali inayoendeshwa kwa kamera za TV si serikali bali ni tamthilia. Serikali huendeshwa juu ya karatasi zilizobeba maamuzi na maelekezo yanayodumu kutoka kizazi hadi kizazi. Sasa tunazo kompyuta, lakini msingi wa kutunza kumbukumbu za maamuzi na maelekezo unabaki pale pale.

Hao wanaoonekana leo wakifanya vituko, hautakuwa muda mrefu kutoka siku watakapopoteza ajira zao kabla hawajawaambia marafiki na ndugu kwamba walikuwa wanatimiza mradi wa kumpendeza mkuu lakini walijua tangu mwanzo kwamba mambo yasingeenda kokote kwa mtindo huo. Anayebisha na abishe, lakini hilo nalijua fika, na watu wa aina hiyo nawajua vilivyo.

Kwa hiyo ningemshauri Rais Magufuli kutowaendekeza hawa wanafiki, bali awajue kwa hulka yao. Kama wanao uwezo anaouhitaji, autumie huo uwezo, lakini asidhani kwamba hawa ni watu anaoweza kuwaamini.

Sasa wote wamekuwa “watumbua majipu”, lakini tumekwisha kuwaona watumbuaji hao wakitumbuliwa. Ni dhahiri, kama nilivyosema katika makala iliyopita kwamba inawezekana kwamba wote tunaowaona wakihaha huku na kule “wakitumbua majipu” hawaielewi ndwele inayotusumbua kiwiliwilini. 

Ikiwa hivyo ndivyo, ina maana kwamba tunatoa dawa kabla hatujaelewa ni ugonjwa upi tunataka kuuponya. Ingetupasa tufanye utafiti wa matatizo yanayotusibu, tuyaelewe vyema, kisha tufanye utafiti wa tiba inayofaa kwa aina ya ugonjwa tuliougundua. La sivyo kutakuwa na hatari ya kweli ya kumtia “drip” ya “glucose” mgonjwa anayeonekana dhaifu kumbe udhaifu wake unatokana na sukari kupanda. Huko ni kumuua moja kwa moja.
 - See more at: http://raiamwema.co.tz/magufuli-ajihadhari-na-%E2%80%9Cwatumbua-majipu%E2%80%9D-wa-geresha#sthash.4YU6v4hX.dpuf

No comments :

Post a Comment