dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Friday, April 8, 2016

CAG Utouh: Mambo matatu yalinikera

Aliyekuwa Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh. Picha ya Maktaba

By Florence Majani na Tumaini Msowoya, Mwananchi
Dar es Salaam. Ludovick Utouh, aliyekuwa Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG), ametaja mambo matatu ambayo yalimkera wakati akiongoza ofisi hiyo, ukiwamo ubinafsishwaji wa Shirika la Usafiri la Dar es Salaam (UDA) ambao kesi yake iliondolewa mahakamani bila ya sababu za msingi.
CAG Utouh alisema hayo jana katika mahojiano na Mwananchi kuhusu hali ilivyokuwa kwenye ofisi hiyo nyeti wakati akiiongoza.
Utouh, ambaye alistaafu mwaka 2014, alitaja mambo mengine kuwa ni uamuzi wa kusimamisha mita za mafuta kwenye Bandari ya Dar es Salaam na Tanga na badala yake kutumia upimaji wa kijita, na suala la wafanyakazi hewa.
Akizungumzia suala la ubinafsishwaji wa Uda, ambao umekuwa ukipigiwa kelele na wabunge kiasi cha kurushiwa maneno ya kashfa, Utouh alisema hajui sababu za suala hilo kutoshughulikiwa ipasavyo wakati kila kitu kiliwekwa bayana.
Alisema katika ukaguzi huo, kila kitu kilikuwa dhahiri na kesi ikafunguliwa mahakamani, lakini baadaye ikaondolewa na suala hilo likakoma.
“Ukweli ukiniambia kwa nini kesi ilitolewa mahakamani sijui. Utekelezaji (wa mapendekezo ya CAG) ulifanywa nusu, lakini naamini ni jambo ambalo serikali italifanyia kazi,” alisema.
“Na pengine ukweli wa mambo utafahamika,” alisema Utouh lakini alipoulizwa ukweli ni upi, alisema taarifa zote aliziweka kwenye ripoti yake ya ukaguzi.
Katika ripoti ya mwaka 2013, CAG anabainisha kuwa tathmini ya hisa na mali za shirika wakati wa kulibinafsisha mwaka 2009 haukufanywa kikamilifu.
“Ripoti ya tathmini ya hisa iliyoandaliwa Oktoba 30, 2009 na Novemba 15, 2010 inahusisha uthaminishaji upya wa mali, karakana na vifaa uliofanywa Agosti 2009, lakini haukuzingatia ukokotoaji wa mali halisi; mali ambazo jumla yake ni Sh473,241,498 ambazo ziliripotiwa kuwa zilichukuliwa na Msajili wa Hazina,” inasema ripoti hiyo.
Pia ripoti hiyo inazungumzia uthibitisho wa fedha zilizolipwa na mnunuzi ambaye ni kampuni ya Simon Group.
“Mkataba wa mgawanyo wa hisa wa Februari 11, 2011 unaeleza kuwa mwekezaji (mnunuzi) alitakiwa alipe jumla ya Sh1,142,643,935 kwa kuzingatia ununuzi wa hisa ambazo hazikutengwa za Uda; ingawa mkataba haukubainisha namba ya akaunti ya benki ambayo malipo hayo yalitakiwa yafanyike,” inaeleza ripoti hiyo.
“Mwekezaji alilipa jumla ya Sh285 milioni kwenye akaunti namba 01J1021393700 ya CRDB inayomilikiwa na Uda.
“Hakukuwapo na malipo zaidi yaliyofanywa na mwekezaji kwa ajili ya ununuzi wa hisa za Uda. Malipo haya ni sawa na asilimia 24.9 ya bei iliyokubaliwa. Mwekezaji anadai alimlipa mwenyekiti wa Bodi ya Uda jumla ya Sh320 milioni kama ada ya ahadi yake mwishoni mwa mwaka 2009.”
Ripoti hiyo inasema kuwa mwenyekiti huyo alikiri kupokea fedha hizo, akidai ni malipo ya ada ya ushauri kutokana na huduma aliyompa mwekezaji, jambo ambalo ni mgongano mkubwa wa kimaslahi.
Suala la Uda bado ni gumzo kwenye vikao vya wabunge na wiki iliyopita suala hilo liliahirishwa kwenye kikao cha kamati ya Bunge inayoshughulika na serikali za mitaa kutokana na kutokuwapo kwa mwenyekiti.
Wakati fulani wabunge wa Dar es Salaam walipohoji sakata hilo, walijibiwa kuwa “wanafikiri kwa kutumia makalio”.
Utouh pia alitaja jambo la pili lililomkera kuwa ni mishahara ya wafanyakazi hewa, akisema alilipigia kelele wakati akiwa CAG na hata CAG wa sasa, Musa Asad amelipigia kelele lakini halikufanyiwa kazi ipasavyo.
CAG Utouh alirejea taarifa ya hivi karibuni ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Angela Kairuki iliyoeleza kuwa katika kipindi cha miezi mitatu, wafanyakazi hewa 7,795 wamebainika na wangesababisha upotevu wa Sh7.5 bilioni.
“Ukiangalia ukubwa wa pesa zinazopotea na mahitaji ya wananchi, kama kweli mtu ni mzalendo unaumia rohoni, unaumia rohoni,” alisema.
Kadhalika CAG Utouh alilitaja jambo la tatu ambalo lilimuudhi kwa kuwa halikufanyiwa kazi katika uongozi wake kuwa ni ripoti yake ya matumizi ya ‘flow meter’ za bandarini ambayo aliitoa 2012 na kubaini upimaji mbovu wa mafuta kwa kutumia mfumo huo.
“Madhara yake ni makubwa kwa sababu unapotumia mfumo wa kijiti kupima mafuta, ni subjective (dhahania). Nchi inapoteza fedha nyingi za kodi kwa sababu ni underdeclaration. Vitu hivi vilionekana na viliripotiwa, lakini havikufanyiwa kazi,” alisema.
Suala la wafanyakazi hewa ni moja ya mambo ambayo Utouh alisema yanaisumbua sana Serikali na ambayo yamelifikisha Taifa katika “utumbuaji majipu”.
Alisema suala la ufuatiliaji matatizo makuu ya ufuatiliaji wa mapendekezo ya ripoti za CAG, Utouh alisema chanzo cha mapendekezo hayo kutofanyiwa kazi ni kukosekana kwa msukumo wa nguvu ya asili na kupuuza.
“Kutekelezwa au kutokutekelezwa kunasababishwa na vitu viwili. Pasikupokuwa na msukumo wa nguvu ya asili, mara nyingi hulka ya mwanadamu ni kupuuza. Sasa mimi nasema, of course kulikuwa na mambo yaliyotekelezwa na ambayo hayakutekelezwa,” alisema.
“Ni vizuri Serikali kusema kuwa hili halijatekelezwa kwa sababu gani, na kulifanyia kazi,” alisema.
Alisema taasisi za serikali zinategemeana katika kufanya kazi, kwa hiyo ripoti ya CAG inapotolewa, Bunge hufanya kazi yake, mapendekezo huweza kupelekwa Takukuru, kwa Mkurugenzi wa Mashtaka, (DPP) na mahakamani kwa ajili ya kufanyiwa kazi.
Alisema ingawa yapo mapendekezo yaliyotekelezwa, baadhi hayakufanyiwa kazi hata hivyo anaamini yatafanyiwa kazi na Serikali ya Awamu ya Tano.

Maeneo yenye matatizo makubwa
Katika mahojiano hayo, CAG Utouh alisema halmashauri ndizo zina matatizo makubwa na kubainisha matatizo hayo kuwa ni malipo ya wafanyakazi hewa, usimamizi mbovu, mifumo mibovu ya udhibiti wa ndani na udhaifu wa ukusanyaji wa mapato wa Serikali.
Alisema mambo hayo ndiyo yanayoitingisha Serikali hadi kufikia hatua ya kutumbua majipu.

Mifuko ya Hifadhi ya Jamii
Akizungumzia suala la mifuko ya hifadhi ya jamii kukopesha fedha nyingi taasisi za Serikali ambayo pia hailipi kwa wakati, CAG Utouh alisema ni kweli aliandika hayo katika ripoti yake.
“Nilipoandika kwa wakati ule nilikuwa sahihi, lakini kwa sababu sipo sijui maboresho yaliyotokea. Kwa wakati ule nilichoandika nilikuwa sahihi na hakuna aliye ni challenge (aliyekosoa),” alisema.

‘Kazi ya CAG ni mbaya’
Utouh pia alisema kazi ya ukaguzi na udhibiti ni ngumu na anashukuru amemaliza salama.
“Kwanza niseme kazi ya CAG ni kazi moja mbaya, si nzuri, ni kazi ambayo haifurahishi watu, ni kama hii ya utumbuaji majipu. Baadhi wanaumia, wengi wanafurahia,” alisema.
Alisema kazi ya CAG ni kazi ambayo unachokonoa vitu ambavyo watu walitaka vizikwe kwenye makaburi yaliyojengewa na hivyo suala hilo humuweka mkaguzi katika wakati mgumu.
“Kwa hiyo unapoibua unasababisha vitu vingi. Unaleta uhasama na chuki. Kuna kazi nyingine majaribu kama hayo na vitisho ni lazima vinakuwepo,” alisema.
Kuhusu kutishiwa maisha alisema yote hayo ni mambo ya kawaida ya kibinadamu, kwani wakati mwingine unaona kabisa mtu anakufuata ana dalili ya kukuhonga lakini unatafuta namna ya kumtoa.
“Namshukuru Mungu kusurvive (kuwapo) mpaka leo tunazungumza hapa,” alisema na kufafanua kuwa hawezi kuzungumza kwa undani kwa sababu ya kiapo.
“Kwa kweli kiapo nilichoapa bado kinanitesa na kitaendelea kunitesa mpaka naingia kaburini,” alisema akimaanisha kuwa kuna mambo hayawezi kuyasema.

No comments :

Post a Comment