Top Leaderboard Advert

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Zanzibar Diaspora

High class shops @ Fuoni

High class shops @ Fuoni

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Adsense Marquee

Tuesday, April 12, 2016

Elimu bure ni matokeo ya utafiti au siasa?

Rais John Magufuli, ambaye uongozi wake unatekeleza mpango wa elimu bure. Picha na Maktaba
By Idd Hamis, Mwananchi
Ahadi ya kutoa elimu bure ilikuwa moja ya ahadi moto katika ahadi za uchaguzi kwa wagombea wakuu  wawili wa kiti cha urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Hawa walikuwa ni  Edward Lowassa wa Umoja wa Katiba ya wananchi (Ukawa) na Dk John Magufuli, aliyekuwa mgombea  kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ambaye sasa ni rais.
Tofauti pekee iliyokuwa kati ya wawili hao ni kwamba mmoja aliahidi kutoa elimu bure kutoka hatua ya msingi hadi chuo kikuu, ingawa hakueleza atawezaje wakati nchi yetu ni maskini na wa pili aliahidi kutoka msingi hadi kidato cha nne.
Wote wawili walifanana katika jambo moja, ahadi zao hazikutokana na utafiti bali zilitolewa kwa malengo ya kuvutia wapigakura.
Labda walikusudia kufanya utafiti baada ya kuukwaa urais.
Kwanza nikiri mapema kwamba hakuna kitu kinachoitwa elimu bure, kwa sababu gharama za elimu zimegawanyika sehemu mbili- gharama za moja kwa moja  na zile zisizo za moja kwa moja.
Gharama za moja kwa moja za elimu ni fedha zinazolipwa moja kwa moja shuleni kwa ajili ya mwanafunzi kusoma. Hizi ni kama vile ada ya shule na malipo ya kulipia huduma kwa wanafunzi wa bweni kama vile malazi,  chakula, afya na usafiri. Wakati mwingine hulipwa kama ada ya shule.
Gharama zisizo za moja kwa moja ni pamoja na gharama za sare, vitabu, kalamu, chakula, kodi mbalimbali shuleni na kila gharama inayoingia katika kuwezesha elimu kuhawilishwa kutoka kwa mwalimu hadi kwa mwanafunzi.
Katika shule za umma, gharama hizi hulipwa na Serikali na katika shule zisizo za umma, gharama hizi zinaweza kuingizwa katika ada ya shule au kulipwa na mzazi kwa utaratibu aujuao yeye mwenyewe alimradi mwanafunzi afike shuleni.
Tunapozungumzia nadharia ya elimu bure, bila shaka tunazungumzia shule za umma au shule za Serikali. Kinachosemwa kuwa elimu bure ni kumuondolea mzazi wajibu wa kumlipia mwanaye gharama za moja kwa moja.
Gharama zisizo za moja kwa moja, bado mzazi hawezi kuzikwepa kwani Serikali hailipi gharama hizi.
Serikali imejaribu kufafanua kupitia waraka Na. 5 wa mwaka 2015 nini wajibu wake na majukumu ya wazazi katika utekelezaji wake. Gharama zinazobebwa na Serikali kimsingi zinatokana na wananchi kupitia kodi mbalimbali wanazolipa, hivyo kiuhalisia hakuna elimu bure.
Katika waraka huo, Serikali imefafanua kuwa ina wajibu wa kununua vitabu, kemikali na vifaa vya maabara, samani, matengenezo ya mashine na mitambo, kujenga na kukarabati miundombinu ya shule, kutoa chakula kwa wanafunzi wa bweni pamoja na kutoa ruzuku kwa kila mwanafunzi.
Kwa upande wa wazazi, Serikali imesema wana wajibu wa kununua sare za shule na michezo, madaftari na kalamu, kugharimia chakula kwa wanafunzi wa kutwa, pamoja na matibabu ya watoto wao, kulipia nauli ya kwenda na kurudi shuleni, kununua magodoro, shuka na vifaa vya usafi kwa wanafunzi wa bweni.
Ndiyo maana nilikiri mapema kwamba kitu elimu bure hakipo. Labda tungeambiwa elimu nafuu (subsidized education), kwa sababu Serikali inabeba gharama za ada na imeondosha michango iliyokuwa ikitozwa kwa wazazi.
Je, tulijiandaa kwa elimu bure?
Kwa kuwa tumeshaona kwamba kitu elimu bure hakipo, kuanzia hapa nitakuwa nikiandika ‘elimu bure’ kutofautisha dhana ya elimu bure iliyojengeka na uhalisia kwamba hakuna elimu bure.
 Januari, Rais John Magufuli alitangaza kwamba Serikali itaanza kutoa ‘elimu bure’ kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari za Serikali na kupiga marufuku michango yote.
Shule zilipofunguliwa, mabilioni yakaanza kutolewa na Serikali kuu kwenda shule zote nchini ikiwa ni utekelezaji wa agizo na  ahadi ya Rais.
Changamoto zilizojitokeza baada ya kuanza kutekelezwa kwa ahadi hii, zimeonyesha kwamba hakukuwa na maandalizi ya kutosha, yaani utafiti haukufanyika kabla ya kuanza kuitekeleza sera ya elimu bure.
Ziko shule zilizokumbwa na matatizo mbalimbali kuanzia matatizo ya uhaba wa majengo, madawati, vifaa vya kufundishia na kujifunzia na upungufu mkubwa wa walimu kutokana na ongezeko kubwa na wanafunzi walioandikishwa kuitikia wito wa elimu bure.
Haraka haraka Serikali ikatangaza kuongeza wigo wa utoaji wa vibali vya kuchangia maendeleo ya elimu kwa hiari kwa mamlaka ya wakuu wa mikoa, ili kutoa nafasi kwa wadau mbalimbali wenye nia ya kufanya hivyo.
Huu ni ushahidi tosha kwamba hatukuwa tumejiandaa kabla ya sera ya ‘elimu bure’ kuanza. Inapokuja katika elimu, Tanzania haijabadilika kwa sababu tangu utawala wa awamu ya kwanza inaonekana siasa inapewa nafasi kubwa katika elimu kiasi cha kupuuza utafiti.
Kama utafiti ungekuwa umefanyika mapema, Serikali ingekuwa imejikita kwanza kuandaa mazingira ya kuja kutoa hiyo ‘elimu bure’ kwa kuboresha miundombinu ya shule zetu na kuongeza vifaa na walimu kukabiliana na wimbi la ongezeko la wanafunzi.
Kwa kutokuzingatia utafiti na kufanya mambo kisiasa, kuna hatari kubwa ya sera hii kuja kuleta athari kubwa kielimu kwa watoto wa Kitanzania kama ilivyokuwa kwa sera ya Elimu kwa Wote (UPE) enzi za Mwalimu Nyerere.
Enzi za UPE, Serikali iliwachukua wanafunzi waliofeli darasa la saba kuhudhurua mafunzo ya ualimu kisha kurudi kufundisha katika shule zilizokuwa zinaongezeka kwa kasi kufuatia sera hiyo.
Madhara yake ingawa idadi ya uandikishaji wanafunzi shuleni iliongezeka,  kiwango cha ubora wa elimu kilikuwa duni. Hapo ndipo hata kinachoitwa ‘janga la Hisabati’ kitaifa kilipoanzia.
Tunarudia makosa yale yale
Wakati wa Serikali ya Awamu ya Nne, tulishuhudia juhudi za kuziba pengo la walimu kwa kuzalisha walimu wa harakaharaka. Mpango uliofanya walimu hao kujulikana kama ‘Walimu wa Vodafasta’.
Kabla ya hapo siasa katika elimu ilifikia kiasi cha kufanyika madudu ya ajabu pale aliyekuwa Waziri wa Elimu, Joseph Mungai, alipobadili mitalaa na kufuta baadhi ya masomo kama vile somo la biashara na uhasibu na kuunganisha mengine.
Uanzishwaji wa shule za kata nao ni ushahidi mwingine kwamba maamuzi ya kisiasa katika sekta ya elimu hayafanyiki baada ya utafiti bali yanafanyika kwa kukidhi matakwa ya kisiasa.
Kilichoanza kama sera nzuri kwa kuhakikikisha kwamba kila kata inakuwa na shule ya sekondari kimekuja kugeuka kuwa dimbwi la matatizo ya kielimu kwa kutotanguliza utafiti kabla ya kutengeneza na kutekeleza sera husika.
Sera ni nzuri, tatizo siasa kuburuza elimu
Sera ya elimu bure pamoja na upungufu wake, ni sera nzuri kwani  inaisukuma Serikali kuwapa wananchi wake elimu. Tatizo ninaloliona hapa ni kupuuzwa kwa kanuni isemayo; “Bila utafiti hakuna haki ya kuzungumza”.
Kama kanuni hii inaweza kupuuzwa katika maeneo mengine, katika sekta ya elimu ikipuuzwa utakuwa msiba mkubwa kwa Taifa kwa sababu jinsi taifa lilivyo ni matokeo ya elimu inayotolewa kwa wananchi wake.
Iddi Hamis ni mchambuzi wa masuala ya maendeleo na jamii. dinyampuntaz@yahoo.com

No comments :

Post a Comment