dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Thursday, April 7, 2016

Hoja ya MCC inahitaji mjadala wa kitaifa, siyo ushabiki wa kisiasa

Wakazi wa kijiji cha Chandama wilayani Chemba, Dodoma wakichota maji jana, kutokana na kukosekana kwa maji safi. Maadhimisho ya wiki la Maji yanafanyika mkoani Dodoma huku Serikali ikidai kutumia Sh589bilioni kutekeleza miradi mbalimbali ya maji hasa vijijini. Picha na Israel Mgussi
By Malisa Godlisten,Mwananchi
Tangu Serikali ya Marekani ilipotangaza kuinyima Tanzania fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Changamoto za Milenia (MCC) kumekuwa na mijadala mbalimbali kuhusiana na suala hilo.
Bahati mbaya mijadala imetawaliwa na wanasiasa zaidi, huku wasomi ambao wangeweza kutoa mwelekeo mzuri wakikaa kimya.
Kila mwanachama au kiongozi wa chama cha siasa anajadili suala hilo katika mrengo utakaokiacha salama chama chake. Wafuasi wa vyama vya upinzani wamekuwa wakitupa lawama kwa Serikali ya CCM kuwa ni chanzo cha yaliyotokea, huku wafuasi wa chama hicho wakikitetea chama chao na kukiondoa katika lawama hizo.
Mchambuzi wa masuala ya kisiasa nchini, Hamphrey Polepole alitetea suala hilo akijenga hoja zake katika misingi mikubwa miwili.
Kwanza, alionyesha MCC na Serikali ya Marekani ni vitu viwili tofauti, yaani tunaweza kuharibu uhusiano na MCC, lakini tukaendeleza uhusiano mzuri na Marekani.
Hoja hiyo ina ukakasi kwa wachambuzi wa masuala ya kisiasa na kiuchumi. Polepole ameonyesha dhahiri kukosa taarifa za kutosha juu ya kile anachojadili. Maelezo yake yanaonyesha MCC ni taasisi binafsi kama ilivyo Bill & Melinda au Ford Foundations? Yaani ni taasisi isiyo na uhusiano wa moja kwa moja na Serikali ya Marekani.
Ndiyo maana anasema uhusiano na MCC unaweza kuzorota, lakini usiathiri uhusiano na Serikali ya Marekani.
Kimsingi MCC ni mkono wa Serikali ya Marekani. Kwa mujibu wa Deo Munishi (Katibu wa zamani wa Bavicha), uteuzi wa Ofisa Mtendaji Mkuu wa MCC unapitia kwenye Bunge la Marekani (Congress) na Mwenyekiti wa Bodi ya MCC ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani na Makamu Mwenyekiti wa Bodi ni Waziri wa Fedha.
Kwa hiyo, siyo kweli kwamba unaweza kuzorotesha uhusiano na MCC bila kuzorotesha uhusiano na Serikali ya Marekani.
Kuhitilafiana na MCC hakuwezi kwa namna yoyote ile kutengwa na Serikali ya Marekani. Maana yake ni kwamba, suala la MCC limetia doa uhusiano wa kidiplomasia kati ya Marekani na Tanzania.
Hoja nyingine ambayo imetolewa na Polepole ni kujinasibu kwamba Tanzania inaweza kujitegemea kiuchumi bila kuhitaji msaada wa wahisani. Ameweka rejea za nyuma za uamuzi wa kuvunja uhusiano na Uingereza na Ujerumani. Hapa kuna shida.
Tofauti iliyopo kati ya kipindi kile na sasa ni kwamba, kipindi kile sisi ndiyo tulikataa misaada baada ya kutokubaliana na mataifa hayo kisera, siyo kwamba tuliomba wakatunyima. Kuna tofauti kubwa kati ya kukataa msaada na kunyimwa. Kukataa msaada ni heshima, lakini kuomba msaada na kunyimwa ni aibu. Sisi tumeomba tukanyimwa halafu tunajifanya kujifariji kwamba tuna uwezo wa kujitegemea kiuchumi. Kama uwezo huo tunao kwa nini tuliomba?
Tungekuwa hatutaki msaada wa MCC tungeutangazia ulimwengu siku nyingi kuwa Tanzania haipaswi kuwamo kwenye orodha ya ‘ombaomba wa MCC’. Swali ambalo kina Polepole na wenzake hawataki kujibu ikiwa kweli tuna uwezo wa kujitegemea kiuchumi ilikuwaje tukaomba? Hivyo basi hakuna ufanano wowote wa kimantiki kati ya kuvunja uhusiano na Ujerumani na Uingereza miaka ya zamani na kunyimwa msaada wa MCC leo.
Je, ni kweli kwamba tumenyimwa msaada wa MCC kwa sababu ya kukataa kuingiliwa uhuru wetu? Propaganda hizi zinazoenezwa na watu mbalimbali kwamba Marekani wanataka kuingilia mambo yetu ya ndani kwa hiyo tumekataa wakaamua kutukomoa? Je, ni kweli kwamba tunaonewa kiasi hiki?
Siyo kweli hata kidogo. Hii ni njia tu ya kutafuta huruma ya wananchi ili ionekane tumeonewa katika suala hili na tuweze kuungwa mkono na mataifa mengine. Kwanini hatutaki kusema ukweli kuwa adhabu hii ni matokeo ya ukiukwaji wa haki za binadamu na kukosa utawala bora usioheshimu demokrasia?
Marekani wametaja sababu mbili kubwa za kufuta msaada wa MCC. Moja ni Sheria ya Makosa ya Mitandao na pili ni uchaguzi wa Zanzibar. Tangu mwaka jana Marekani wamepiga kelele juu ya masuala hayo mawili.
Mbona hatutaki kujadili mambo haya na badala yake tunakimbilia kulalamika kwamba tunaonewa na kueneza uongo kuwa Marekani wanataka kutuingilia? Kwa nini tunatafuta huruma kwa wananchi kwa kutumia hoja za uongo?
Sheria ya Makosa ya Mitandao inakiuka misingi ya haki za binadamu na utawala bora. Tanzania imeridhia mikataba na sheria mbalimbali za kimataifa za kulinda haki za binadamu na utawala bora, lakini bado tukatunga sheria inayokinzana na mikataba hiyo.
Marekani wakasema sheria hiyo ifanyiwe marekebisho maana inakiuka misingi ya utawala bora. Tanzania tukakataa kufanya marekabisho hayo. Leo Marekani wanatunyima msaada tunasema tunaonewa? Hii siyo sawa.
Uchaguzi wa Zanzibar
Suala la Zanzibar vivyo hivyo. Imefanyika mizengwe mingi ya kuminya demokrasia visiwani Zanzibar kwa masilahi ya kisiasa. Uamuzi wa Wazanzibari kuchagua mtu wanayemtaka ulipuuzwa na kulazimishwa kurudi kwenye uchaguzi. Ajabu ni kuwa tume ile iliyoharibu uchaguzi wa mwanzo ndiyo iliyopewa tena jukumu la kusimamia uchaguzi wa marudio. Huu ni ukiukwaji mkubwa wa demokrasia.
Marekani wakashauri waachieni Wazanzibari waamue kwa utashi wao kiongozi wanayemtaka. Hatukusikia ushauri huo. Leo Marekani wanatunyima msaada tunasema tumeonewa? Upototoshaji! Kwa nini tusiwe wasema ukweli? Kwa nini tutafute huruma kwa kusema uongo?
Hoja nyingine inayotolewa ni madai kuwa fedha hizi ni kidogo hivyo haziwezi kuathiri uchumi wetu. Hoja hii siyo sahihi kabisa kwa sababu fedha hizi ni nyingi na zingeweza kutumika kutekeleza miradi mingi ya maendeleleo.
Ukichukua Sh1 trilioni ukaiweka kwenye noti za elfu 10 utapata jumla ya noti 100,000,000. Kila noti ina urefu wa sentimita 12. Kwa hiyo tukizidisha tunapata sentimita 1, 200,000,000 (100,000,000×12). Kilomita 1 ni sawa na sentimita 100,000. Kwa hiyo tukichukua sentimita 1,200,000,000 tukagawanya kwa 100,000 tunapata kilomita 12,000.
Umbali kutoka Johanesburg (Afrika Kusini) hadi Cairo (Misri) ni kimomita 6,259. Kwa hiyo kilomita 12,000 ni sawa na kutoka Johanesburg hadi Cairo mara mbili. Maana yake ni kwamba ukiweka Sh1 trilioni katika noti za elfu 10 unaweza kuzipanga kuanzia Johanesburg hadi Cairo mara mbili bila kuacha hata sentimita moja njiani.
Yaani uchukue noti za elfu kumi uzipange kuanzia Johanesburg upande nazo hadi Botwsana, kisha Harare, Lusaka, Tunduma, Dar, Nairobi, Khartoom, hadi Cairo bila kuacha hata sentimita moja njiani. Ukifika Cairo unaanza tena upya kuzipanga kwa kurudi hadi Johanersburg. Hizo ndiyo fedha ambazo Marekani wametunyang’anya baada ya kukiuka hadi za binadamu kule Zanzibar.
Suluhisho
Baadhi ya wanazuoni wanasema kwamba ni vizuri tukajadili namna ya kupata ufumbuzi kutoka hapa tulipo badala ya kupoteza muda mwingi kujadili chanzo. Lakini ikumbukwe siyo rahisi kupata suluhisho bila kujua chanzo cha tatizo. Tukijadili suluhisho bila kujadili chanzo ni kuruhusu tatizo kujirudia.
Ni sawa na kumpa dawa ya kutibu maleria mtu ambaye anaishi karibu na dimbwi linalofuga mbu bila kuangamiza mbu hao. Huyo mtu atakunywa dawa atapona, lakini baada ya muda ataugua tena maana mbu ambao ndiyo chanzo cha tatizo hawajashugulikiwa.
Kwahiyo tusijaribu kukimbia kivuli chetu wenyewe. Lazima tujadili chanzo ndipo tutafute suluhisho. Ni muhimu tukubaliane kuwa chanzo cha yote haya ni Serikali inayoongozwa na CCM kushindwa kuheshimu demokrasia kwa watu wa Zanzibar na kutunga sheria inayokiuka haki za binadamu, Sheria ya Makosa ya Mitandao.
Tutumie rasilimali zetu vizuri kujiimarisha kiuchumi ili hata tukinyimwa fedha za wahisani bado tuwe na nguvu ya kujitegemea. Tuna rasilimali nyingi ambazo zikitumika vizuri zitaimalisha uchumi wa nchi.
Mwandishi ni mchambuzi wa masuala la kisiasa na kijamii, anapatikana kwa baruapepe: malisagj@gmail.com na maoni@mwananchi.co.tz     

No comments :

Post a Comment