dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Wednesday, April 6, 2016

Magufuli aja na bajeti ya viwanda ya Sh. trilioni 26

  • NI ukomo wa bajeti ya serikali 2016/ 17, umejikita kwenye viwanda, elimu, afya. Wasomi wataka serikali itafute suluhu na wahisani, waanisha vitu vya msingi vya kutilia mkazo...Ukurasa 12.
  • WIZARA ya Fedha na Mipango leo inatarajia kuwasilisha mbele ya wabunge wote ukomo wa Bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2016/17, inayokadiriwa kuwa takribani Sh. trilioni 26.
Taarifa ambazo Nipashe ilizipata jana kutoka Wizara ya Fedha, ukomo wa bajeti ijayo unakadiriwa kufikia Sh. trilioni 26, huku kipaumbe kikubwa kitakuwa viwanda.

Vipaumbele vingine vitakuwa ni elimu na maji na suala la miundombinu ya umeme na barabara pia vitakuwa jambo la muhimu kwenye bajeti hiyo, lengo likiwa ni kusaidia viwanda viweze kufanya kazi ipasavyo.“Viwanda vitakavyopewa kipaumbele ni vile vinavyotokana na rasilimali ambazo tunazo kama vile mazao ya kilimo, ngozi, pambana na vitu vingine, lakini kumbuka huwezi kuwa na viwanda bila umeme wa uhakika na rasilimali watu, vyote hivi ni vitu muhimu ambavyo vitaangaliwa kwa makini kwenye bajeti hii inayokuja ili kusaidia msukumo wa viwanda ambayo ndiyo ahadi kubwa ya Rais tangu kwenye kampeni,” kilisema chanzo cha habari kwa gazeti hili.

Bajeti hiyo ambayo itakuwa ya kwanza kwa serikali ya Rais John Magufuli tangu aingie madarakani, inazidi ile ya mwisho ya Rais Mstaafu Jakaya Kikwete iliyokuwa ya Sh. trilioni 22.5, ambalo ni ingezeko la takribani Sh. trilioni nne.

Mbali na bajeti hiyo ya mwisho ya Rais Kikwete ambayo ilijikita zaidi kufanikisha uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, bajeti ya mwaka 2014/15 ilikuwa Sh. trilioni 19.85 na mwaka 2013/14 ilikuwa Sh. trilioni 18.2.

Wakati wa Mkutano wa Bunge uliopita, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, aliwasilisha mwelekeo wa mpango wa maendeo wa mwaka 2016/17, ambao ulionyesha kuwa bajeti ya serikali itakuwa wastani wa Sh. trilioni 23.

Bajeti hiyo inakuja wakati ambapo baadhi ya wahisani wametangaza kukata misaada yao kwenye bajeti ya Tanzania, huku wengine wakiondoa fedha zao kwenye miradi mbalimbali waliyokuwa wakiifadhili kutokana na kutoridhishwa na uchaguzi wa Zanzibar.

Kwenye bajeti ya serikali ya 2014/15 wahisani walitarajiwa kuchangia Sh. trilioni 1.09, lakini wengi walikataa kutoa fedha kutokana na kashfa ya akaunti ya Tegeta Escrow.

Marekani imeshatangaza kuifuta Tanzania kwenye nchi wanachama wa Shirika la Changamoto za Milenia (MCC), hivyo nchi kukosa Sh. trilioni 1.03 ilizokuwa ipewe na shirika hilo kusaidia ujenzi wa barabara za pembezoni na kusambaza umeme vijijini.

Umoja wa Ulaya (EU) nao upo kwenye hatihati ya Sh. trilioni 1.56, unaendelea kusubiri hatima ya mazungumzo na hali ya Zanzibar itulie kabisa.

Pia baadhi ya mawaziri wa Uingereza nao wanaishauri serikali yao kumyima Tanzania msaada wa Sh. bilioni 622 kutokana hali ya Zanzibar.

Wizara ya Fedha na Mipango imeshatangaza wahisani 10 kati 14 wanaosaidia bajeti kuu ya serikali kujitoa, ambapo Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk. Servacius Likwelile, alisema waliobaki ni Benki ya Dunia (WB), Umoja wa Nchi za Ulaya (EU), Dernmark na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB).

Wahisani wengine ambao wamekuwa wakisaidia bajeti kuu ya serikali ni Uingereza, Canada, Finland, Ujerumani, Ireland, Japan, Norway na Sweden.

VIPAUMBELE VYA SERIKALI
Kwenye mkutano wa Bunge uliopita, Dk. Mpango alisema vipaumbele vya serikali kwa mwaka 2016/17 itakuwa ni pamoja na kukamilisha utekelezaji wa miradi inayoendelea ya awamu ya kwanza ya Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP I) na Mkakati wa Kukuza Uchumi awamu ya pili (Mkukuta II).

Alisema kipaumbele kingine kitakuwa ni uendelezaji wa viwanda vya kuimarisha ukuaji uchumi, utekelezaji wa miradi mikubwa ya kielelezo, kuboresha maeneo wezeshi kwa maendeleo ya viwanda yakiwemo nishati, ardhi, kilimo na miundombinu.

Vipaumbe vingine ni kuendeleza Teknolojia ya Habari na Mawasiliano na maendeleo ya ujuzi maalum ili kuongeza upatikanaji rasilimali watu wenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya uchumi wa viwanda, kuendeleza huduma za fedha, biashara na masoko na uendelezaji wa huduma za jamii kama vile elimu, afya na maji.

MATUMIZI YA SERIKALI
Alisema pia matumizi ya serikali yanatarajiwa kupungua kutoka asilimia 23.9 ya pato la taifa mwaka 2015/16 hadi kufikia asilimia 21.5 mwaka 2016/17, kufuatia kukamilika uchaguzi mkuu mwaka jana.

Kupunguza nakisi ya bajeti (ikijumuisha misaada) kutoka asilimia 4.2 mwaka 2015/16 na kuendelea kupungua hadi chini ya asilimia 3 katika kipindi cha muda wa kati.

WACHUMI WANENA
Dk. Wilhelm Ngasamiaku, ambaye ni mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDS), aliliambia Nipashei kuwa, ili bajeti iweze kuwa na tija lazima rasilimali watu iwe moja ya kipaumbele.

Alisema rasiliamali watu ndiyo kila kitu na itaweza kuhakikisha ndoto ya Tanzania ya viwanda inafanikiwa.

Alisema pia kwamba, viwanda hivyo vinatakiwa kuwa vile vinavyogusa rasilimali zilizo ndani ya nchi na pia miundombinu ya umeme na barabara iangaliwe ili kufanya viwanda hivyo vifanye kazi na siyo kuwa mzigo kwa taifa.
Naye Mhadhiri na Mtafiti wa Masuala ya Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Prof. Haji Semboja, alisema kuwa bajeti itengenezwe kulingana na kiwango cha fedha kilichopo.

“Unashona suti kulingana na kitambaa ulichonacho, hivyo kama fedha ipo ndogo tutegemee bajeti ndogo,” alisema na kuongeza:

“Lakini kuna njia mbili inategemea Wamerekani walitoa fedha kwa ajili ya matumizi gani, kama fedha hizo zilikuwa zinatolewa kwenye bajeti ni za maendeleo na inajulikana zilikuwa zinakwenda kwenye maeneo muhimu.”

Alisema kutokana na suala hilo anaishauri serikali kutafuta utaratibu wa kukopa kwenye taasisi za fedha za ndani ama za nje ya nchi zenye riba nafuu ili kuendeleza miradi hiyo bila kusimama.

Aidha, alisema katika mtazamo wa pili ni kwamba kusitishwa kwa msaada huo wa fedha hakujaelezwa ni adhabu ya kudumu au la, jambo la msingi ni serikali kujiuliza ilipokosea mpaka wameamua kusitishiwa msaada huo.

“Serikali inatakiwa kujiuliza ilipokosea mpaka wenzetu wakatukosesha fedha hizo, tunaweza kuzungumza na wenzetu katika hali ya kibinadamu kwani suala la misaada linatoka kwa watu wanakatwa kodi zao kutoka Marekani ambao ni wafanyakazi wa kawaida na wengine ni masikini na fedha hizo zinaletwa kufanya shughuli za maendeleo,” alisema.

Hata hivyo, alisema haamini kama Wamarekani wapo tayari kuwaadhibu masikini kwa ajili ya mfumo wa kiurasimu wa serikali ya Kitanzania ambao wanaususia.

Alisema suala la vipaumbele tayari vimeorodheshwa, hivyo haviwezi kupata usumbufu na kukosekana kwa fedha hizo.
Prof. Semboja alisema vipaumbele vya serikali havijabadilika ni vile vile ikiwamo afya, barabara, elimu miundombinu na maji, vingine vitakavyopatikana ni vile vilivyopo katika sekta zote za maendeleo.

Mchumi na Mhadhiri Mwandamizi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Donath Ulomi, alisema vipaumbele anavyoviona kulingana na hali ya nchi ilivyo vinavyohitaji kuwekezwa katika maeneo ambayo yatafanya nchi iondoe matatizo ya msingi yaliyopo ni pamoja na upatikanaji wa fedha.

“Tatizo moja wapo ni upatikanaji wa fedha kwa sababu unapozungumzia bajeti sio pesa pekee, bali ni programu ya kazi ya mwaka wa serikali inayotakiwa kuainisha ni jinsi gani itasimamia vyanzo vya mapato sambamba na kutafuta vyanzo vipya,” alisema.

“Ili bajeti ijitosheleze bila kutegemea wafadhili ni lazima serikali ikubali kuwa chanzo kimojawapo cha kuchangia pato la taifa ni kodi ya majengo ambalo ni eneo halijafanya vizuri. Majengo mengi Dar es Salaam hayajafanyiwa tathmini hivyo serikali ikiamua kufanyia kazi eneo hilo itaongeza mapato,” alisema.

Pia alitaja eneo jingine ni umiliki wa ardhi ambayo sehemu kubwa haijapimwa na hata ile iliyopimwa hakuna motisha ya upatikanaji wa hati.

“Eneo la tatu ni la ukusanyaji wa kodi na jingine ni lazima tuboreshe utendaji hasa katika sekta ya umma, sasa tunaona majipu yanatumbuliwa lakini ukiingia katika taasisi na wizara hata sekta binafsi ukiangalia mpangilio wa kazi wa majukumu, ufuatiliaji na uwajibishaji kwa ngazi zote upo dhaifu,” alisema na kuongeza:

“Matokeo yake mfumo wa usimamiaji wa watumishi wa uwajibishaji na uwajibikaji kama sio imara utajikuta unalipa gharama kubwa sana, gharama za watumishi wa serikali ni karibu nusu ya pato la taifa, karibu nusu ya kodi inaenda kulipa watumishi, kwa hiyo kama huwasimamii vilivyo inaleta tatizo kubwa kwenye uchumi,” alisema.

Dk. Ulomi alitaja eneo jingine linalohitaji kushughulikiwa kuwa ni elimu, ambayo inatakiwa iboreshwe kuanzia shule za chini, za sekondari hadi vyuoni kwa sababu bado ni janga linaloumiza kiutendaji.

Pia alisema sekta ya kilimo inahitaji nguvu ya uwekezaji katika kilimo cha umwagiliaji badala ya kile kinachotegemea mvua ili kuchangia pato la taifa.

/NIPASHE.

No comments :

Post a Comment