dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Tuesday, April 5, 2016

Mikutano mitano ya kimataifa aliyoikosa JPM

Rais John Magufuli
By Julius Mathias, Mwananchi 
Dar es Salaam. Siku 150 tangu aapishwe kuwa Rais wa Awamu ya Tano, Rais John Magufuli amekosa mikutano mitano ya kimataifa, ikiwamo wa kiuchumi uliofanyika Davos nchini Uswisi na ule wa mazingira wa Umoja wa Mataifa uliofanyika Paris, nchini Ufaransa.
Mikutano hiyo iliyohusisha wakuu wa nchi na serikali, miwili ilifanyika Afrika na mitatu ilifanyika Ulaya.
Hata hivyo, mkutano wa kimataifa aliohudhuria ni mmoja uliohusisha wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, uliofanyika jijini Arusha.
Miongoni mwa mikutano hiyo ni ule wa mazingira ulioandaliwa na Umoja wa Mataifa (COP21) uliofanyika jijini Paris, uliozungumzia changamoto za dunia katika suala la mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi. Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi 150 akiwamo Rais Barack Obama.
Pia, Rais Magufuli hakuweza kuhudhuria mkutano wa Wakuu wa Serikali wa nchi za Jumuiya ya Madola (CHOGM) uliofanyika Malta, uliozungumzia changamoto za umaskini, demokrasia na masuala ya ugaidi. Tanzania iliwakilishwa na balozi wake aliyeko nchini Uingereza.
Mkutano mwingine ambao Rais Magufurli hakuhudhuria ni ule wa viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), uliofanyika Gaborone nchini Botswana, uliozungumzia ushirikiano wa kisiasa, ulinzi na usalama. Mkutano huo aliwakilishwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Rais Magufuli pia, hakuhudhuria Mkutano wa Jukwaa la Uchuni Duniani (WEF) lililofanyika Davos nchini Uswisi, uliojadili masuala ya wakimbizi, bei za bidhaa, ugaidi na mabadiliko ya tabianchi. Kwenye mkutano huo taasisi za fedha za kimataifa zikiwamo Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), wakuu wake walitoa mada kuhusu mwelekeo wa uchumi wa dunia.
Pia, hakuhudhuria mkutano wa Ushirikiano wa kimaendeleo kati ya China Afrika, maarufu Focac, uliofanyika Johannesburg nchini Afrika Kusini na uliozungumzia ushirikiano wa uendelezaji wa miundombinu ya reli, barabara, bandari na umeme ambapo mdau mkubwa kwa maendeleo hayo ni Serikali ya China iliyowakilishwa na Rais wake Xi Jinping.
Gazeti hili lilizungumza na wadau wa masuala ya kimataifa kuhusu mambo ambayo Tanzania inayakosa kwa Rais kutohudhuria mikutano hiyo, ambayo licha ya ajenda za mikutano lakini inatoa fursa kwa Rais kukutana na viongozi wengine ambao ingekuwa ni gharama kubwa kuwafuata mmoja mmoja katika nchi zao.
Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), John Seka alisema ingawa Rais hafungwi na sheria yoyote asipohudhuria mkutano wowote wa kimataifa, ipo baadhi inayomhitaji ambayo ni lazima awepo.
“Kama mkutano ni wa maamuzi basi ni lazima Rais ahudhurie. Mingine ni ya kujenga mahusiano tu ambayo anaweza akamtuma mwakilishi bila kujali marais wa nchi ngapi wanahudhuria,” alisema Seka.
Aliutolea mfano mkutano wa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) uliofanyika mwanzoni mwa mwezi uliopita, ulikuwa ni wa maamuzi ndiyo maana Dk Magufuli alilazimika kuhudhuria na si kutuma mwakilishi kama alivyofanya kwa baadhi ya mikutano.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Omari Mbura alisema kuna mambo mengi yanayoweza kuwa yanachangia Rais kutoona umuhimu wa kutoka nje ya nchi kwa wakati huu, huku akiamini kuwa ipo siku atafanya hivyo.
Alitoa sababu mbili ambazo ni siasa na uhusiano wa kimataifa, kwamba ndiyo kwanza Uchaguzi Mkuu umekamilika, inawezekana kuna masuala hayajakaa vizuri na Rais anayaweka sawa. Alitahadharisha pia, Tanzania haiizuii dunia kuendelea na mipango iliyokuwepo.
Huku akiamini kuwa ipo siku Rais atatoka, alitahadhirsha kuwa: “Ulimwengu haujui kama Tanzania ina Rais mpya…inaendelea na mipango iliyokuwepo. Siyo jambo baya kutuma mwakilishi, lakini endapo mkutano husika unawahusu wakuu wa nchi wanaweza wasimpe uzito unaotakiwa yeyote anayemwakilisha.”
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Mindi Kasiga alikuwa na maoni tofauti juu ya uwakilishi wa Rais. Alisema: “Rais anayo mamlaka ya kuteua mwakilishi na huwa anafanya hivyo kila inapobidi na akabainisha kuwa hakuna mkutano wowote ambao Tanzania haikushiriki na ukawa na madhara yoyote.”
Waziri Kivuli wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa, Peter Msigwa alisema siasa za kuwaaminisha wananchi juu ya dhana ovu dhidi ya wanasiasa ndizo zinazoendelea.
“Rais anajaribu kuwaaminisha wananchi kuwa kila aliyekuwa anaenda nje alikuwa anatumia vibaya fedha za umma. Hiyo si kweli. Yeye anapaswa kwenda huko kwa faida ya taifa,” alisema.
Alizitaja sababu za Rais kufanya hivyo kuwa ni pamoja na kujitambulisha akieleza kuwa wapo baadhi ya wananchi wa mataifa ambao hawamjui Rais mpya wa Tanzania. Kujenga au kuendeleza uhusiano ni pamoja na kuitangaza nchi na kuvutia wawekezaji.
“Tumevutia wawekezaji kwa zaidi ya miaka 20. Anapaswa kuendeleza suala hilo. Akienda nje pia ataitangaza nchi na kuifaidisha kwa kuvutia watalii. Kila anachokifanya sasa hivi ipo siku kitahitaji mchango wa mataifa ya nje, hilo haliwezi kushtukizwa,” alieleza.
Profesa Samwel Wangwe, mwanaharakati na mchumi wa taasisi ya Repoa alisema kuna namna ambayo mkuu wa nchi anaweza akaendeleza diplomasia ya kimataifa kupitia vikao na mijadala inayofanyika kabla ya mkutano husika.
“Kabla ya mkutano wowote huwa kunakuwa na mijadala. Hii ni muhimu zaidi kwa mahusiano ya nchi. Unapofanyika mkutano huwa ni kuhitimisha kile kilichojadiliwa awali na hapo Rais anaweza akaamua, kulingana na nafasi yake, ahudhurie au amtume mtu,” alisema.
Alifafanua kuwa bado upo uwezekano wa kujenga diplomasia imara kwa kuwatumia mabalozi, wa ndani na nje na kufanikisha mipango yote ya kimaendeleo baina ya mataifa yenye kuelewana.     

No comments :

Post a Comment