Top Leaderboard Advert

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Zanzibar Diaspora

High class shops @ Fuoni

High class shops @ Fuoni

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Adsense Marquee

Friday, April 15, 2016

Muhimbili, Ocean Road zitengewe fedha za kutosha mwaka 2016/17  • KATIKA toleo letu la jana, tulichapisha habari ikieleza kuwa hali ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), ni mbaya kutokana na serikali kutoa kiasi kidogo cha fedha, tofauti na zinazoidhinishwa na Bunge.Kwamba kutokana na hali hiyo, mara kadhaa wagonjwa wamekuwa wakilalamikia kupata huduma hafifu.

Uchunguzi wetu wa siku kadhaa, umebaini changamoto nyingi zinazozikabili taasisi hizo mbili, ni ukosefu wa fedha za miradi ya maendeleo, ikiwa ni pamoja na kununua vifaa tiba na ukarabati.

Kwa mfano, kwa mwaka wa fedha 2015/16, MNH, iliomba Sh. bilioni 118.943 na Bunge likaidhinisha Sh. bilioni 1.694, lakini hadi sasa ikiwa imebaki miezi miwili kabla ya kumalizika kwa mwaka wa fedha, kiasi kilichotolewa ni Sh. milioni 538 tu.Aidha, uchunguzi umebaini kwamba licha ya Rais Dk. John Magufuli kuagiza kununuliwa kwa vitanda kwa ajili ya wagonjwa wa hospitali hiyo, MNH na taasisi zake bado zinakabiliwa na upungufu wa vitanda na wodi katika baadhi ya idara.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Profesa Lawrence Museru, alithibitisha kuwapo kwa changamoto hiyo na kueleza kuwa hali hiyo inasababishwa na serikali kupanga bajeti finyu na wakati mwingine kutopata fedha za maendeleo na kuwa mwaka wa fedha 2014/15, mahitaji ya hospitali hiyo yalikuwa Sh. bilioni 113.25 na Bunge liliidhinisha Sh. bilioni 3.8, lakini zilizotolewa ni Sh. bilioni 1.29 tu.

Kwa ujumla MNH iliendelea kupokea fedha kidogo kutoka serikalini hadi bajeti ya mwaka wa fedha 2013/14 tofauti na walizoomba na zilizoidhinishwa na Bunge, hali iliyoifanya kuwa na malimbikizo ya madeni na hadi Februari mwaka huu kudaiwa Sh. bilioni 12.7.

Ocean Road nayo imekuwa ikitengewa bajeti finyu na serikali, na fedha za miradi ya maendeleo hazitolewi kwa wakati mwafaka na wakati mwingine hazitolewi kabisa.
Takwimu za mapato na matumizi ya taasisi hiyo zinaonyesha katika mwaka wa fedha 2013/14, mahitaji yalikuwa Sh. bilioni 8.39, Bunge likaidhinisha wapewe Sh. bilioni nane (asilimia 95.3), lakini hakuna fedha zilizotolewa na hali hiyo imeathiri huduma za taasisi, ununuzi wa vifaa na vifaa tiba pamoja na uchunguzi na tiba ya saratani nchini.

Kimsingi, hali hii inadhihirisha kwamba serikali haikujali umuhimu wa kuziwezesha hospitali hizo kwa bajeti ili zitoe huduma bora za tiba kwa wananchi. Katika hali hii ni dhahiri kuwa wananchi wengi wanaathirika ikiwamo kupoteza maisha kutokana na kukosa huduma bora za tiba.

Kwa kuwa Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015-2000 pamoja na mambo mengine, inazungumzia kuboresha huduma za afya, matarajio yetu ni kuwa kuanzia mwaka ujao wa fedha 2016/17, serikali ya awamu ya tano itatenga na kuelekeza fedha za kutosha katika sekta ya afya hususan katika hospitali zetu.

Tunashauri kuwa serikali isiishie kutoa fedha hizo tu, bali jambo la msingi ni kufuatilia pia ili zitumike kwa lengo lililokusudiwa la kuwapatia Watanzania huduma bora za afya.

Ni matumaini yetu kwamba viongozi wenye dhamana wanazo taarifa kuhusiana na hali ilivyo katika hospitali za Muhimbili, Ocean Road na zingine, na bila shaka watachukua hatua haraka za kuzinusuru kwa kuzipatia fedha za kutosha kuanzia bajeti ya 2016/17.

No comments :

Post a Comment