dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Sunday, April 3, 2016

Tanzania yenye neema yanukia

NA EDITOR

3rd April 2016

Inawezekana kuonekana kama ni jambo dogo, hasa linapoangaliwa kisiasa, lakini kitendo cha Rais John Magufuli kutangaza mshahara wake hadharani kina maana kubwa katika ujenzi wa nchi masikini kama yetu, na si kwa sababu ya udogo wa mshahara huo.

Rais Magufuli alitangaza juzi kuwa huwa analipwa Sh. milioni 9.5 kwa mwezi, ikiwa ni mara ya kwanza katika historia ya bara hili kwa mkuu wa nchi kutaja mshahara wake.

Aidha, Nipashe tunafahamu, ni nadra kwa viongozi wa nchi kote duniani kutaja mishahara yao hivyo kufanya ujasiri wa Rais Magufuli kuwa na maana pana zaidi, hata nje ya mipaka ya Afrika.
 
Kwa nini tumesema, Nipashe, kitendo cha Rais Magufuli kutangaza mshahara wake hadharani kina maana kubwa katika ujenzi wa nchi masikini kama yetu.Kwanza, tunaona Nipashe, kinaingiza uwazi na uwiano katika mgao wa keki ya taifa ambao utafanya malipo ya viongozi wengine wote nchini kuwa katika nafasi ya kuchunguzwa kuona kama wanalipwa kulingana na kazi wanazofanya - hivyo kustahili.
 
Tumeona mapema wiki hii kuwa baadhi ya wakuu wa mashirika ya umma wamekuwa wakilipwa mpaka Sh. milioni 40 kwa mwezi wakati kima cha chini serikalini kikiwa Sh. 315,000 kwa mujibu wa ahadi ya Rais mstaafu, Jakaya Kikwete mwaka jana.
 
Ni kiwango ambacho ni chini ya ombi la Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) la kutaka kima cha chini kiwe angalau Sh. 720,000 kwa mwezi.
 
Sh. milioni 40 zinaweza zisiwe fedha nyingi, hata hivyo, lakini ni kiwango ambacho kwa mtazamo wetu, Nipashe, ni kikubwa kulingana na udogo wa uchumi wa nchi na matatizo mengi ya kijamii ambayo yanahitaji kila senti inayoweza kuokolewa, kuelekezwa huko kuyatatua na yasiishe hata katika miaka 10 ijayo.
 
Aidha, Nipashe hatudhani kwamba ni sahihi, kwa mfano, pakawa na tofauti kubwa kiasi hicho ya malipo kati ya mkuu wa shirika na mfanyakazi wa chini zaidi wakati kimsingi, kazi kubwa hufanywa na wasaidizi ambao wanasimamiwa na mkurugenzi husika.
 
Mbali na kuleta uwazi na uwiano katika mgao wa keki ya taifa kama ambavyo tumeshasema, kitendo cha Rais Magufuli kutangaza mshahara wake hadharani, Nipashe tunaona, pia kitasaidia kuleta nidhamu ya utendaji wa kazi miongoni mwa watumishi wote wa serikali na mashirika ya umma, wakurugenzi wakiwemo.
 
Rais alishasema katikati ya wiki kuwa katika serikali yake hatarajii kuwa na mtendaji mwenye kulipwa mshahara wa zaidi ya Sh. milioni 15 kwa mwezi na kwamba ambaye anaona kuwa fedha hizo ni chache aache kazi.
 
Ni wazi, basi, watendaji wa mashirika ya umma, idara na wakala wa serikali ambao walikuwa wakilipwa Sh. milioni 40 kama mshahara, itawalazimu kuamua kusuka ama kunyoa.
 
Na ni wazi, basi, endapo watendaji wa mashirika ya umma, idara na wakala wa serikali hao wataamua kusuka hata nidhamu yao katika utendaji itabadilika na kufahamu kuwa walipewa dhamana hiyo kwa ajili ya kuondoa umasikini miongoni mwa Watanzania na si kujitajirisha kwanza.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment