dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Wednesday, April 13, 2016

Wapongeza, wapinga na kutoa ya moyoni Kilango kutimuliwa


WAKATI Rais John Magufuli ameanza kuwatia 'matumbo joto' wakuu wa mikoa na watendaji wengine serikalini, kwa kutengua uteuzi wa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anne Kilango Malecela, wananchi wamepokea uamuzi huo kwa hisia tofauti.

Kilango alivuliwa wadhifa huo juzi, akiwa amekalia kiti hicho kwa siku 27 tangu kuapishwa kwake Machi 15, mwaka huu, hivyo kuwa mkuu wa mkoa aliyeweka rekodi ya kukaa muda mfupi katika historia ya Tanzania.

Uamuzi wa Rais Magufuli kumvua Kilango wadhifa huo, ulitokana na kutoa taarifa za uongo juu ya wafanyakazi hewa katika mkoa wake. Kilango katika kikao na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene, alisema katika mkoa wa Shinyanga hakuna hata mtumishi hewa mmoja.

Hata hivyo, Rais Magufuli juzi alisema taarifa hiyo haikuwa ya kweli kwa kuwa imebainika kuwa ndani ya mkoa huo, uchunguzi wa awali unaonyesha kuna watumishi hewa 45 waliosababisha kulipwa Sh. Milioni 339.9.Mbali na Kilango, Katibu Tawala wa Mkoa huo, Abdul Dachi, ambaye ndiye ofisa mtendaji mkuu katika mkoa, kama ilivyo kwa katibu mkuu katika wizara, naye amewajibishwa kutokana na sakata hilo.

Wakitoa maoni yao kutokana na uamuzi huo, baadhi ya wananchi waliozungumza na Nipashe katika mkoa wa Shinyanga na Muheza, mkoani Tanga wametoa maoni tofauti, wakiwamo wanaopengeza hatua hiyo na wengine kupinga.

Mkoani Shinyanga, baadhi ya wananchi walisema pamoja na kwamba kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano na bila kuiingilia mamlaka aliyo nayo Rais ya kuteua na kutengua uteuzi wa kiongozi, haijalishi anatoa sababu za utenguzi au asitoe, wamemtaka Rais kuangalia sababu za kiongozi huyo kutoa taarifa za uongo.

Sambamba na kuangalia sababu hizo, pia wameomba wale wote walioshiriki kumpatia taarifa mkuu huyo kuwajibishwa na kuwatahadharisha viongozi na watendaji wengine kutoaminiana.

Musa John, mkazi wa Ngokolo manispaa ya Shinyanga, alisema wakati Watanzania wakiwa na kiu ya kuona mabadiliko ya kweli kupitia uongozi wa Rais Magufuli, busara pia itumike kuona namna ya uwajibikaji kwa watendaji anaowateua kuwapa dhamana ya kuwatumiakia wananchi.

Alisema kilichompoza Kilango kuwaamini wasaidizi wake, wakiwamo watalaam wa sekretarieti ya mkoa, wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa manispaa, miji na wilaya.

"Wakati umefika kwa watendaji na viongozi wetu sasa kuwa na hofu ya Mungu ya kusema kweli. Japo palihitajika busara kutumika katika uamuzi wa kumtimua mkuu wa mkoa, hii inatoa funzo kwa wengine wanaowaamini watu wa chini yao,” alisema Francis Mabula wa mji mdogo wa Mhunze wilayani Kshapu.

Fredy Peter wa Mwadui, alisema wakati umefika sasa kwa viongozi na watendaji popote walipo kutoaminiana juu ya taarifa zao za utendaji wa kazi wa kila siku

Naye Elizabeth John wa Shinyanga mjini alisema watu wanapaswa kujifunza kuwa hakuna kumwamini mtu katika kazi kwa sababu ni vigumu kujua yupi ni mkweli na yupi ni mwongo.

Hatua ya kutenguliwa uteuzi wa Kilango ambaye wakati anakabidhiwa ofisi na mtanguklizi wake, Ally Rufunga, kuwa hatamwangusha Rais, ilisababisha wananchi wengi kushikwa na butwaa baada ya kusikia taatifa hizo.

Katika hotuba zake fupi mbele ya watendaji na wadau wa mandeleo wa mkoa wa Shinyanga, kupitia kikao chake cha kwanza cha Bodi ya Barabara na cha Kamati ya Ushauri ya mkoa (RCC), Kilango alisema na kuahidi kutomwangusha Rais Dk. Magufuli na kuwa ataenenda na kasi yake yenye falsafa ya "Hapa kazi tu".

Pia aliahidi kupambana na rushwa na ufisadi pamoja na kuwaondolea kero wananchi. Vile vile aliwataka wananchi, viongozi na watendaji wote kumuunga mkono ili kuharakisha maendeleo ya Shinyanga.

Huko Muheza, mkoani Tanga, baadhi ya wananchi wamempongeza Rais Magufuli kwa uamuzi wake huo, wakisema anaendeleza falsafa yake ya Hapa Kazi Tu pamoja na kasi ya kutumbua majipu.

Rajabu Selemani, mkazi wa Ubembe wilayani Muheza, alisema uamuzi uliochukuliwa na Rais Magufuli ni wa kupongezwa na hiyo ni fundisho kwa viongozi wote kwa kuwa walishazoea kusema uongo na kuwadanganya viongozi wakuu wa serikali kwa kuwasomea taarifa za uongo wanapofika katika sehemu zao za kazi.

Pia alishauri Rais kutuma watu wake kwa siri kuchunguza katika mikoa na wilaya, kwa sababu kuna mambo mengi yanafanyika ya ufisadi lakini viongozi wakubwa wanapofika wanafichwa.

Kwa upande wake, Juma Athumani alisema kuwa mbali na mishahara hewa pia kuna ufisadi mwingi katika wilaya, mikoa mpaka Taifa katika miradi ya maendeleo, kwa sababu watu wanakula fedha za serikali. Alitaka Rais afike Tanga ili aelezwe bayana maovu yanayofanyika mkoani hapa.
Imeandikwa na Anceth Nyahore, Shinyanga na Steven William, Muheza.

No comments :

Post a Comment