dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Wednesday, June 15, 2016

JENERALI ULIMWENGU ATAKA KIKWETE ASHITAKIWE

Mwanahabari nguli nchini Jenerali Ulimwengu amesema Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete anapaswa kushtakiwa mahakamani kwa kuisababishia hasara Serikali kutokana na mabilioni ya shilingi yaliyotumika katika mchakato wa Katiba ambayo haikupatikana.

Akizungumza katika tamasha la nane la Kigoda cha Mwalimu Nyerere katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) jana, Jenerali Ulimwengu alisema fedha nyingi zimepotea wakati wa kuunda Katiba Mpya ambayo haikupatikana. 

Mbali ya fedha zilizotumika na Tume ya Mabadiliko ya Katiba wakati wa kukusanya maoni na nyingine zilizotumika kurekebisha ukumbi wa Bunge uweze kubeba wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, jumla ya Sh24.53 bilioni zilitumika kulipa posho za wajumbe. 

Tamasha hilo lililojikita kujadili falsafa za Mwalimu Nyerere katika muktadha wa “Visheni ya Maendeleo ya Watu,” liliwakutanisha wasomi mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi, wanafunzi na wanasiasa wakiwamo Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na Waziri mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba. 
Jenerali aliyekuwa anajadili hotuba ya mgeni rasmi, Benjamin Mkapa, alisema fedha nyingi ziligharamia mchakato wa Katiba uliokuwa unaendeshwa na Tume ya Katiba chini ya Jaji Joseph Warioba, lakini ulikwama, ndiyo maana hadi leo hakuna Katiba mpya. 

“Itabidi (Kigoda cha Mwalimu) mumuite mwaka ujao, aje aeleze fedha za wananchi zilizotumika katika mchakato ule zilikuwa na sababu gani,” alisema Jenerali aliyekuwa akishangiliwa na wahudhuriaji. 

“Iwapo mawaziri wa zamani wamechukuliwa hatua na kupelekwa mahakamani kwa kusababisha hasara, Mheshimiwa Kikwete anastahili kupelekwa mahakamani kwa kusababisha hasara kwa Serikali na kuzima matumaini ya wananchi na kuachwa wanarandaranda wasijue wafanye nini na baadaye inaweza kutuletea machafuko, kama hatukuweza kutengeneza Katiba ambayo itatuwekea mustakbali wa Watanzania,” alisema. 

Jenerali alisema suala la Katiba limekwama na limekwamishwa kwa makusudi kabisa. 

Kuhusu Mwalimu Nyerere, Jenerali alisema asingekuwa anazungumzwa kwa sifa nyingi kama sasa, iwapo asingechukua uamuzi wa mwaka 1992 wa kuruhusu mfumo wa vyama vingi, licha ya kwamba waliokuwa wameukubali ni asilimia 20 ya Watanzania. 

Kuhusu Rais John Magufuli, Jenerali alisema pamoja na sifa anazopewa sasa za utendaji wake, akitazamwa kwa uwanda mpana, nchi imerudi nyuma kwa miaka 50 kwa masuala ya demokrasia. 

Akifafanua namna nchi ilivyorudi nyuma, alisema, “Kwa kufinya uhuru wa kujieleza na hususan kwa kufinya uhuru wa wawakilishi wa wananchi ndani ya Bunge.” 

Baadaye, Rais mstaafu, Benjamin Mkapa ambaye alikuwa mgeni rasmi katika tamasha hilo alifafanua kauli ya Jenerali kwa kusema yeye (Mkapa) hakuwa mshauri wa Rais, bali Jaji Warioba alimfuata atoe ushauri na hakuwa kwenye ngazi yoyote ya uamuzi. 

“Kwenye chama changu sikuwemo na kwenye Serikali sikuwemo. Siwezi kulizunguzumzia hilo na waandishi wanapenda nitoe maoni,” alisema Mkapa. 

Alisema ipo haja ya kujiuliza kwa nini Katiba hiyo ilikwama na hadi sasa hajasikia uchambuzi wa kina kuhusu jambo hilo.

“Kuna haja ya kuwa na mjadala mkubwa lakini siyo kulaumiana tu. Siyo kudai tu. Kuwezesha uhuru wa kuzungumza ni jambo moja na kutumia uhuru huo ni kujadili, kuchambua na kupima na kufanya uamuzi sahihi kitu kingine kabisa,”alisema Mkapa. 

Alisisitiza kuwa badala ya kumlaumu mtu mmoja mmoja, mjadala mpana wa kitaifa unahitajika ili kujua kilichosababisha Taifa kukosa Katiba Mpya. 

“Hakuna anayeandika ni wapi tulipokwama, tunalaumu na kumjadili mtu, wengine wanasema Katiba imekwamishwa na watu wachache kwa sababu za kimaslahi…tunapaswa kuwa na mjadala wa kina kujua ni wapi tulipokwama,” alisema Mkapa. 

Aidha, Jenerali aliwananga viongozi wastaafu akisema amebaini sasa kuwa kwa bahati mbaya wanapata busara baada ya kuacha nafasi za uongozi. 

Alisema ili kuwa na busara wakati mtu akiwa madarakani, anatakiwa awasikilize wale anaowaongoza na njia moja ya kufanya hivyo ni kuwapa Katiba ambayo ndiyo mwongozo utakaosimamia mustakabali wao. 

Awali, akiwasilisha mada katika tamasha hilo, Mkapa alisema si kana kwamba Mwalimu Nyerere hakupenda kampuni binafsi zije kuwekeza nchini bali alipenda biashara na uwekezaji vifanyike kwa haki, usawa na kuchangia maendeleo ya nchi. 

Kuhusu sukari, Mkapa ambaye alijitetea kwa kuanzisha sera ya ubinafsishaji, alisema wakati anaingia madarakani, viwanda vya sukari vikiwamo Kilombero na Mtibwa vilikuwa havizalishi kabisa au kuzalisha kidogo, hivyo kulikuwa na tatizo la sukari. 

Alisema baada ya ubinafsishaji, sukari ilianza kuzalishwa kwa wingi lakini akahoji ni nini hakikufanyika hadi nchi ikafikia mahali ilipo sasa.

Ugawaji mikoa 
Akichangia mjadala huo, mhadhiri mwandamizi wa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (Tataki) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Martha Qorro alisema Serikali imeendelea kuongeza idadi ya mikoa, jambo ambalo linazidi kuwagawa wananchi. 

Pamoja na kuathiri umoja wa kitaifa, mhadhiri huyo alikuwa na maoni kuwa, fedha nyingi kwa sasa zinatumika kuendesha mikoa inayoongezwa badala ya kuleta maendeleo kwa wananchi. 

Hata hivyo, Mkapa alisema wakati wa uongozi wake aliongeza mkoa mmoja tu wa Manyara, ambao aliumega kutoka Arusha baada ya kuona uhitaji na kufanya vikao. 

Rais huyo mstaafu alisema suala la kuzingatia wakati wa ugawaji wa mikoa ni kutowagawa wananchi kwa misingi ya ukabila na udini. 

Mstaafu huyo aliyeiongoza nchi kipindi cha mwaka 1995-2005, alisema suala la kuangalia ni mahitaji ya watu ndiyo maana alikaa na viongozi wa maeneo yote hayo na hatimaye kufanikiwa kuigawa Arusha. 

Alisema Watanzania wengi wamekuwa na desturi ya kutumia muda mwingi katika kuilaumu Serikali badala ya kufanya kazi kwa maendeleo ya nchi. 

“Watanzania tunatakiwa tufanye kazi kwa bidii ili tuifikishe nchi yetu kwenye maendeleo na si kutumia muda mwingi katika kuilaumu Serikali,” alisema Mkapa. 

No comments :

Post a Comment