Top Leaderboard Advert

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Zanzibar Diaspora

High class shops @ Fuoni

High class shops @ Fuoni

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Adsense Marquee

Saturday, September 24, 2016

2021 Vijiji vyote kuwa na umeme!


PROFESA SOSPETER MUHONGO
Serikali imesema vijiji vyote nchini vitakuwa vimepatiwa huduma ya nishati ya umeme katika kipindi cha miaka mitano kuanzia sasa kupitia mradi wa umeme vijijini unaoendeshwa na Wakala wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA III).

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, alisema hayo juzi alipokutana na wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoani Kagera wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za utafiti wa tetemeko mkoani humo.

Akizungumzia mradi huo wa REA III, Waziri Muhongo alisema ni mkubwa na wa kipekee na kwamba fedha za kutosha zimetengwa ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na kama ilivyokusudiwa.

Alisema fedha zilizopo kwa ajili ya mradi huo ni zaidi ya Sh. trilioni moja na kwamba kasi ya usambazaji umeme itaongezeka maradufu kuzidi awamu zilizotangulia.Aidha, Waziri Muhongo alibainisha kuwa makandarasi wanane hawataruhusiwa kufanya kazi kwenye Mradi wa REA III kwa vile walishindwa kufikia malengo na makubaliano waliyokuwa wamewekeana katika utekelezaji wa Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Pili (REA II).

“Tunayo majina ya Wakandarasi Nane ambao kazi zao hazikuturidhisha; walishindwa kufikia malengo yaliyokuwa yamewekwa na hivyo hatutoendelea nao,” alisema Profesa Muhongo.

Vilevile Waziri Muhongo aliwaasa wafanyakazi hao wa TANESCO kujiepusha na vitendo vya rushwa ikiwemo kuepuka mazingira yanayoweza kusababisha kuwepo kwa rushwa ili kuwa na ufanisi katika shughuli zao.

Katika kuonesha dhamira hiyo ya kuepuka rushwa, wafanyakazi hao walikula kiapo mbele ya Waziri na kuahidi kwamba hawatajihusisha na vitendo vya rushwa na kuwa watahakikisha wanatekeleza wajibu wao kwa kufuata sheria, taratibu na kanuni zilizowekwa.

Wakati akiendelea kuzungumza na wafanyakazi hao wa TANESCO, Profesa Muhongo aliwaagiza kuhakikisha wanashughulikia matatizo na malalamiko ya wateja kwa wakati ili kuepusha hali ya kutoelewana na wateja husika.

Profesa Muhongo aliwaagiza kuhakikisha wanatatua matatizo ya wateja. Alisema kumekuwepo na malalamiko mengi ya wateja kuhusiana na utendaji mbovu wa shirika hilo kote nchini na moja ya malalamiko hayo ikiwa ni ucheleweshwaji wa kuunganishwa na huduma ya umeme jambo ambalo amelikemea vikali.

Mbali na hayo, vilevile Waziri muhongo aliliagiza shirika hilo kufungua ofisi katika maeneo ya vijijini hususan pale penye watumiaji wengi wa huduma ya umeme ili kuwaepushia usumbufu wa kusafiri umbali mrefu kufuata huduma kwenye ofisi za TANESCO ambazo ziko katika makao makuu ya wilaya na mikoa pekee.

“Hatumtendei haki mwananchi kusafiri umbali mrefu kufuata huduma ambayo angeweza kuipata maeneo anayoishi; ni vyema mkaangalia namna ya kuwa na Ofisi maeneo mbalimbali nje ya makao makuu ya wilaya na mikoa,” alisema.

No comments :

Post a Comment