dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Sunday, September 18, 2016

Lipumba yamkuta mapya CUF!

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba
Christina Mwakangale – Nipashe Jumapili
18 September 2016


MGOGORO unaonukia kati ya Chama cha Wananchi (CUF) na Profesa Ibrahim Lipumba kuhusiana na nafasi ya uenyekiti wa taifa, umechukua sura mpya.

CUF, kimemtuhumu Profesa Lipumba kwa mambo kadhaa, ikiwamo kula njama za kutaka kukiangamiza na pia kumhusisha na fedha za michango kiasi cha Sh. milioni 280.


Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi Taifa wa CUF, Julius Mtatiro ndiye aliyetoa tuhuma hizo nzito dhidi ya Profesa Lipumba wakati akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam, jana:

“Tuna ushahidi…tunaweza kuweka kila kitu hadharani…Anataka kukiua chama cha CUF kilicho na wabunge 43, madiwani 300 na wenyeviti wa mitaa 1,000,” alisema Mtatiro.

Alisema, Lipumba aliwahi kuchangiwa Sh. milioni 280 na baadhi ya wabunge wa CUF, ili zisaidie mchakato wake wa kugombea urais katika uchaguzi mkuu na kwamba, inashangaza kuona kuwa sasa anaongoza njama za kukiangamiza chama na wabunge hao.

“Ni wabunge hao hao, baadhi yao ndiyo walimchangia Sh. milioni 280 ili agombee urais,” alisema Mtatiro.

Mtatiro aliyewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara) chini ya uenyekiti wa Lipumba, alisema kuwa Lipumba amekuwa akifanya vikao vya kila mara nyumbani kwake ili kupanga njama za kuiua CUF.

Hata hivyo, Nipashe haikuweza kuthibitisha ukweli wa kauli ya Mtatiro juu ya Lipumba kupitia vyanzo vilivyo huru.

Aidha, jitihada za kumtafuta Lipumba ili azungumzie tuhuma hizo na nyingine za CUF dhidi yake jana ziligonga mwamba baada ya kutopatikana.

Simu yake ya mkononi iliita muda wote bila kupokewa na pia hakukuwa na majibu kutokana na swali aliloulizwa kuhusiana na suala hilo kupitia ujumbe mfupi katika simu yake ya mkononi.

Lipumba aliyesimamishwa uanachama hivi karibuni pamoja na wafuasi wake kadhaa kutoka miongoni mwa wanachama wa CUF, anavutana na chama hicho kuhusiana na nafasi ya uenyekiti.

Aliingia katika mgogoro baada ya kuwahi kuandika barua ya kujiuzulu siku chache kabla ya kuanza kwa kampeni za uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, 2015.

Lakini baadaye, aliandika barua nyingine kutengua barua yake ya awali ili aendelee kukiongoza chama hicho. Lipumba alijiuzu uenyekiti wa CUF, Agosti 5 mwaka jana.

Hata hivyo, Profesa Lipumba anasisitiza kuwa bado yeye ni mwenyekiti halali wa chama hicho kutokana na barua aliyoiandika ya kusitisha uamuzi wake wa awali.

Aidha, uongozi wa juu wa CUF unapinga jambo hilo kwa maelezo kuwa katiba yao haina kipengele hicho. CUF ilifanya mkutano mkuu Agosti 22, mwaka huu ambao wajumbe 470 (zaidi ya 70) waliafiki kujiuzulu kwa Lipumba.

Mkutano Mkuu huo ambao ulinuilia kumchagua mwenyekiti mpya wa chama hicho ulivunjika baada ya kukumbwa na vurugu zilizoonekana kuratibiwa na wafuasi wa Lipumba.

Wakati alipotangaza kujiuzulu, Lipumba alisema sababu ya kufanya hivyo ni kutounga mkono kukaribishwa kwa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa katika muungano wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ambavyo ni Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD.

BASHANGE ASIMULIA MKASA WA KUTEKWA
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Uchumi na Fedha wa CUF, Joram Bashange alisimulia jaribio la kutaka kutekwa na kulihusisha na mvutano unaoendelea ndani ya cham chao .

Bashange alisema tukio hilo lilijiri majira ya asubuhi akitoka nyumbani kwake mtaa wa Madenge, Buguruni Dar es Salaam alishangaaa gari nyeusi aina ya Noah (namba tunazo) ikipaki mbele yake.

Alisema kuwa gari hiyo ilikuwa na watu wanne na mmoja wao alifungua mlango kabla ya kumvuta kwa nguvu ili aingie ndani ya gari hiyo.

“Baada ya kutembea hatua 20 kutoka nyumbani kwangu, Noah ilipaki mbele yangu na kunilazimisha kuingia ndani ya gari…watu hao wote ninawajua,” alisema Bashange, huku akiwataja majina watu hao ambao mmoja wao alifanikiwa kukimbia.

Alieleza kuwa, wakati vuta nikuvute ya kumuingiza ndani ya gari ikiendelea, watu waliokuwa jirani walilizingira gari hilo na hatimaye kutibua mpango huo huku wakiwezesha kukamatwa kwa wahusika kabla ya kufikishwa katika kituo cha Polisi Buguruni.

Alisema kuwa mmoja wa watu hao alipokaguliwa kituoni alibainika kuwa na pingu, na kwamba walifunguliwa jalada namba BUG/IR/5937/2016.

Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Salim Rashid aliithibitishia Nipashe kutokea kwa tukio hilo, pamoja na kuwashikilia watu watatu kwa tuhuma za kutaka kumteka Bashange.

Alisema uchunguzi kuhusu tukio hilo unaendelea na kwamba utakapokamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani.

No comments :

Post a Comment