Top Leaderboard Advert

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Zanzibar Diaspora

High class shops @ Fuoni

High class shops @ Fuoni

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Adsense Marquee

Friday, September 9, 2016

SARATANI ZANZIBAR: Kasi ya kutisha, madaktari 2 tu; hakuna tiba rasmi!


Zanzibar ina mikoa mitano na kila mkoa umebahatika kuwa na hospitali yake, mbali na vituo vya afya vingi vilivyopo kila baada ya kilomita tano katika maeneo ya mjini na vijijini.

Hospitali hizo zote, ikiwamo ya Rufaa Mnazi Mmoja, zinakabiliwa na changamoto moja kubwa ya kukosa tiba sahihi ya saratani.

Changamoto hiyo na nyinginezo kwa wagonjwa wa saratani, huwalazimu wafuate matibabu nje ya Zanzibar.

Mwanakhamis Mohammed Abdallah, ni miongoni wanaougua saratani kwa miaka nane sasa. Anaeleza matibabu ya ugonjwa huo kuwa ni makubwa mno kwake, akiamini ni kuliko magonjwa mengine.

Anasema mwanzoni alipogunduliwa kusumbuliwa na saratani ya titi, familia yake ilikata tamaa kwamba asingeweza kuishi tena, kutokana na Zanzibar kukosa matibabu yaKe.

“Kwanza familia yangu ilikuwa haina elimu kuwa ugonjwa wa saratani unatibika.Lakini, ilikuwa na hofu hasa pale nilipotakiwa niende nchini India kwa ajili ya matibabu,” anasimulia.Mwanakhamis anasimulia mwanzo wake ni alipoanza kuona uvimbe katika titi lake la kushoto, bila ya kuelewa kitu kilichomsumbua.

Anasema alipogundua dalili hiyo, alifika katika Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja kupata matibabu, alihisiwa kuwa na saratani, lakini hapakuwapo vifaa vya uchunguzi

Hivyo, alitakiwa kwenda katika Hospitali ya Ocean Road ya jijini Dar es Salaam, ambayo ni mahsusi kwa ajili ya uchunguzi na ndipo alipogunduliwa kuwa na saratani ya titi. Hiyo ilikuwa mwaka 2008.

“Ama kweli kabla hujafa hujaumbika. Nilikuwa na matiti yangu mawili, lakini baada ya kugundulika kuwa nasumbuliwa na saratani nilifanyiwa upasuaji nchini India, kukatwa titi langu la upande wa kushoto na hivi sasa hivi nina titi moja tu,” anasema Mwanakhamis.

Analinganisha gharama alizotumia ni kiasi anachopkadiria kumuwezesha kujenga nyumba ya kifahari.

Mwanakhamis anasema baada ya kupata matibabu nchini India, alirejea nyumbani na kuendelea na matibabu katika Hospitali ya Ocean Road, ambako kliniki yake inamgharimu Sh. miioni 1.5 kila mwezi na anatakiwa kuhudhuria kwa miaka mitano. Anasema hadi sasa ameshamaliza dozi na afya yake imeimarika.

CHANGAMOTO ZA WAGONJWA

Kuhusu changamoto zinazowakabili wagonjwa wa saratani, anasema matibabu yao ni ghali sana, hasa ikizingatiwa wagonjwa wengi wa saratani wa Zanzibar, hali zao ni duni kiuchumi.

Mwanakhamis anafafanua kuwa mgonjwa wa saratani Zanzibar anaweza kukata tamaa ya kupona na kuendedelea kuishi, kutokana na gharama kubwa za matibabu ambayo hayapatikani Zanzibar.

Anasema mbali na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kufungua kliniki ya saratani katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, bado wagonjwa wa saratani wenye hali ngumu na wako hatarini kupoteza maisha.

Mgonjwa huyo anasema, ugonjwa wa saratani ukiwa mkubwa na matibabu yake yanakuwa makubwa zaidi na ndio maana, wengi wanaougua hushindwa kumudu gharama za matibabu.

Anaiomba Serikali ya Zanzibar kutambua changamoto zinazowakabili wagonjwa wa Visiwani, kwa kuzingatia kipato chao duni.

Mwanakhamis anawageukia wagonjwa wenzake wa saratani kutokata tamaa ya kuishi, bali waendelee na tiba, kwani ni ugonjwa unaotibika iwapo itawahiwa mapema.

DAKTARI BINGWA


Mtaalam bingwa wa saratani katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, Dk. Salama Uledi Mwita, anaeleza kuna aina nyingi za saratani na zinaongezeka Zanzibar, huku wagonjwa wengi wakishindwa kumudu gharama za matibabu.

Anatoa mfano wa takwimu ya kati ya mwezi Februari na Julai mwaka huu, wagonjwa 120 wameripoti katika kliniki hiyo.

Anakiri kwamba katika tathmini ya afya, saratani hivi sasa imeingia katika orodha ya magonjwa yanayowasumbua Wazanzibari.

Kwa mujibu wa Dk. Salama, kuna saratani za aina nne zinazowapa tabu zaidi Wazanzibari. Anaziorodhesha kuwa: Satarani ya Matiti; Tezi Dume; Misuli na Nyama za Mwili; na Shingo ya Uzazi.

Dk. Salama anasema tangu kuanza
kliniki ya saratani hospitalini Mnazi Mmoja mwaka huu, kuna wagonjwa 10 waliobainika kuwa na saratani ya matiti.

Kwa mujibu wa bingwa huyo,ni ugonjwa wenye kawaida ya kuwaathiri zaidi kinamama, ingawaje wapo wanaume wachache wanaogua.

Anasema baada ya kuwafanyia vipimo wagonjwa hao, aliwaandikia rufaa kwenda katika Hospitali ya Kansa ya Ocean Road, jijini Dar es Salaam kupata kupata dawa, kuendelea na matibabu, akitaja aina zake kuwa mionzi na vidonge.

Dk. Salama anazitaja saratani nynginezo tishio kuwa ni ya damu, mifupa, kibofu cha mkojo, utumbo mdogo na mkubwa na koo.

“Wagonjwa wengi hujitokeza kufanya vipimo wakiwa wamechelewa na maradhi hayo huwa yameshafikia kiwango cha juu,” anasema.

Anaongeza kuwa tatizo lina kawaida ya kuwa kubwa zaidi, inapotokea changamoto ya ukosefu wa vifaa vya kufanyia vipimo, sambamba na gharama za dawa.

Dk. Salama anafafanua kuwa saratani ni maradhi yanayoshika nafasi katika kusababisha vifo vingi duniani.

Anatoa takwimu za dunia kuwa, mwaka 2012 kulikuwapo wagonjwa milioni 14 na kati yao, wagonjwa milioni 8.2 walifariki.

“Hali kwa kweli ni mbaya. La kusikitisha ni kwamba, asilimia 60 ya kesi (matukio) za saratani hupatikana katika nchi masikini wa kipato, ikiwamo Zanzibar,” anasema Dk. Salama.

MTIHANI WA TAKWIMU


Bingwa mwingine wa uchunguzi wa saratani Zanzibar, Dk. Msafiri Marijani, anasema maradhi hayo yanaongezeka kwa kasi, kushinda kama yake ya kuambukiza kama vile Ukimwi.

Dk. Marijani anasema hivi sasa asilimia 60 ya vifo vinatokana na maradhi yasiyoambukiza. Hata hivyo, anasema tatizo lililopo Zanzibar ni la kukosekana takwimu sahihi.

Anasema wagonjwa wengi wa saratani huenda kutibiwa katika Hospitali ya Ocean Road, kwa sababu Zanzibar imekosa matibabu ya saratani. Hata hivyo, kuna wagonjwa 1000 walikwisharipoti hospitalini Mnazi Mmoja.

Mtaalam huyo anasema hivi sasa saratani inawaathiri Wazanzibari kwa kiasi kikubwa na jitihada za kinga na ugunduzi wa awali dhidi ya maradhi hayo haziendi vizuri.

“Mimi nafanya uchunguzi wa saratani, lakini mpaka sasa hivi nipo peke yangu. Kwa hiyo, nikiwa na dharura uchunguzi wa maradhi inachelewa na wagonjwa wanakaa zaidi ya mwezi hawajafanyiwa uchunguzi na saratani ukiipa zaidi ya mwezi, inasambaa katika mwili na mgonjwa hawezi kupona tena,”anasema Dk. Marijani.

Anafafanua kuwa, upande wa saratani ya tezi dume ni hatari zaidi, kwani Zanzibar haona daktari wa upasuaji tezi dume.

Dk. Marijani anasema licha ya kuwapo hali hiyo, saratani inashika nafasi kubwa zaidi katika kuwaathiri Wazazibari, wanaolazimika kupata matibabu nje ya visiwa hivyo.

“Wagonjwa wengi wa saratani wasio na uwezo, huwa wanakata tamaa na wengi huwa wanafia majumbani kutokana na gharama kubwa za matibabu,”anasema.

”Upasuaji wa saratani unatakiwa ufanyike mapema, kabla saratani haijasambaa zaidi katika maeneo mengine ya mwili.

“Lakini wagonjwa wengi huwa hawafanyiwi kwa wakati na tunaishia kuwalaumu kuwa hawafiki kwa wakati hospitalini wanapohisi dalili,” anaeleza Dk. Marijani.

Ushauri wake ni kwamba, ni lazima serikali ijipange kutoa huduma bora, hasa ikizingatiwa idadi ya wagonjwa imeongezeka na wanaopewa tiba ni wachache.

Anataja miongoni mwa vitu vinavyowakwamisha tiba ni ukosefu wa wafanyakazi wa afya wanaohudumia maradhi sugu yasioambukiza, ikiwamo saratani.

Anataja Changamoto nyingine ni kasi ya madaktari bingwa wazalendo wanaoenda kufanya kazi nje ya nchi, kusaka maslahi bora, wakikimbia maslahi duni nyumbani.

Pia anataja ukosefu wa vitendea kazi na ukosefu wa dawa hasa za saratani.

WAGONJWA WANENA


Zuhura Salum Amour, ni Meneja wa Jumuiya ya Wanaoishi na maradhi yasiyoambukiza ikiwemo saratani. Anaumga mkono kuwa tiba za saratini ni ghali sana, ikianzia hatua ya uchunguzi.

Anasema wagonjwa wa saratani wanapata maumivu makali, jambo linaloleta umuhimu wa haja ya kuhudumiwa haraka.

Kwa mujibu wa meneja huyo, jumuiya hiyo inafanya kazi kwa kushirikiana na Wizara ya Afya Zanzibar na wamekuwa wakitoa elimu mbalimbali kuhusiana na maradhi yasiyoambukiza.

Anakiri kwamba kinamama hivi sasa wamepata mwamko wa kutaka kuchunguzwa afya zao dhidi ya saratani.

Ushauri wake ni kwamba, wanawake wanapaswa kuendelea kujitokeza kuchunguza afya zao, hasa wakifikia umri wa miaka 40, ambao ndio upo hatarini zaidi dhidi ya saratani.

Zuhura anataja baadhi ya sababu za saratani ni: Tendo la ngono katika umri mdogo inayochangia saratani ya kizazi; mwanamke au mwanaume kuwa na wapenzi wengi; uvutaji sigara; lishe mbaya na uzito mkubwa wa mwili.

Anawataka wagonjwa wa saratani wasitishike na badala yake kuwa makini na wale wanaodai kutoa tiba mbadala, kwani ni ugonjwa unaohitaji tiba sahihi.

Pia rai yake kwa jamii, ni hospitali kuwrka ukaribu na wagonjwa wa saratani na serikali kuwasaidia, kwa sababu tiba yake ni kubwa na yenye gharama.

/Source:www.ippmedia.com

No comments :

Post a Comment