dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Sunday, October 16, 2016

MAALIM SEIF AFUNGUKA KUHUSU PROFESA LIPUMBA!

Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye amekuwa kimya kuzungumzia sakata linaloendelea ndani ya chama hicho likimuhusisha Profesa Ibrahim Lipumba, jana aliondoa ukimya na kueleza kuwa kinachoendelea ni mpango ulioandaliwa wa kuvuruga jitihada za chama hicho za kudai haki, lakini hautafanikiwa.

Pamoja na hayo, Maalim Seif, aliyekuwa makamu wa kwanza wa Rais katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), amesema kuna jitihada alizoziita za mwendokasi za jumuiya ya kimataifa kutatua mgogoro wa kisiasa visiwani Zanzibar.

Maalim Seif alisema hayo jana wakati akitoa salamu zake fupi kwa mamia ya waumini na wananchi waliojitokeza kumsikiliza katika Msikiti wa Kihinani, Wilaya ya Magharibi A.

CUF iko kwenye mvutano wa uongozi kutokana na Profesa Lipumba kushika ofisi kuu za chama hicho zilizoko Buguruni jijini Dar es Salaam akisema kuwa ndiye mwenyekiti halali wa chama hicho baada ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kutoa msimamo na maoni ya ofisi yake kuhusu sakata hilo.Profesa Lipumba alijiuzulu uenyekiti wa CUF Agosti mwaka jana, akipinga chama hicho kuendelea kuwa ndani ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) baada ya vyama vinne vinavyounda umoja huo kumpitisha Edward Lowassa kuwa mgombea wao wa urais.

 Hata hivyo, Juni mwaka huu Profesa Lipumba alimuandikia barua katibu mkuu akitaka atengue barua yake ya kujiuzulu, lakini Mkutano Mkuu wa chama hicho ulijadili suala hilo na kuazimia kukubaliana na kujiuzulu na baadaye Baraza Kuu kupitisha uamuzi wa kumvua uanachama.

Lakini Maalim Seif, ambaye aligombea urais wa Zanzibar katika uchaguzi ambao matokeo yake yalifutwa mwaka jana, anauchukulia mgogoro huo kuwa ni njama za kuwaondoa kwenye mikakati yao ya kudai haki.

“Nasema hiyo ya Profesa Lipumba ni ajenda iliyolenga kutuparaganya ili tuondoke katika mazingira na hima ya kutetea haki yetu iliyoporwa. Lakini msijali hiyo haitafanikiwa nasi tumefikia pazuri sasa,” alisema.

Katika hadhira hiyo, Maalim Seif alilaumu juhudi alizoziita za baadhi ya watu kutumia vibaya mamlaka kutaka kumzuia asiongee na wananchi licha ya kuwa umma unayo shauku kubwa ya kuhitaji kumsikiliza kila anapopita.

 “Najua zipo kila mbinu na hila za kutaka mimi nisiongee nanyi. Wenyewe mmeshuhudia hapa msikitini baada ya kubainika nakuja, lakini nasema mimi ni binadamu na kiongozi, ninayo haki ya kuongea na yeyote popote.Nitaongea na nitaongea popote pale,” alisema. 

Mkwamo wa kisiasa 
Alisema zipo juhudi za ‘mwendo kasi’ kuelekea ufumbuzi wa mkwamo wa kisiasa Zanzibar kupitia meza ya jumuiya ya kimataifa.

“Wapi lilipofikia suala hili ambalo naweza kuliita mwendo kasi? Nasema limefikia pazuri mno, tulieni wala msiwe na shaka, tumefikia hatua ya matumaini makubwa,” alisema Maalim, mmoja wa wanasiasa wenye nguvu visiwani Zanzibar.

Maalim Seif pia alizungumzia suala la Katiba mpya, akisema kumekuwapo na juhudi za chini kwa chini za kutaka kupiku ridhaa ya wananchi kwa kuipitisha Katiba Inayopendekezwa kwa lazima.

Mswada wa mafuta
Akizungumzia muswada wa mafuta na gesi uliopitishwa hivi karibuni na Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Maalim Seif alisema hicho ni kiini macho kwa kuwa hakuna mabadiliko yoyote hadi sasa juu ya sheria hiyo ndani ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wabunge wazuiwa Mtwara 
Katika hatua nyingine, wafuasi wa CUF wakiongozwa na mbunge wa Tandahimba, Katani Katani jana walizuiwa na polisi kuendelea na mkutano wa ndani kwa kile kilichodaiwa ni kuwapo kwa dalili za vurugu.

Wafuasi hao ni wale wanaompinga Profesa Lipumba ambaye anatambuliwa na Msajili wa vyama vya siasa nchini.

Tukio hilo lilitokea jana wilayani Newala wakati wafuasi hao wakiendelea na ziara yao katika wilaya mbalimbali kanda ya kusini.

Katani ambaye pia ni mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi lililomvua Lipumba uanachama, alisema amesikitishwa na kitendo cha askari kuwaruhusu kufanya mkutano na saa moja baadaye kwenda kuwatawanya bila kuwaambia sababu za msingi.

Alisema kuwa baadhi ya viongozi wa wilaya ya Newala wanaomuunga mkono Profesa Lipumba walikwenda polisi na kufanya mbinu mkutano huo usiendelee.

 “Newala kuna figisufigisu, tulitoa taarifa za kikao cha ndani polisi na waliridhia, lakini viongozi wa wilaya wakaenda polisi kwa kushtukiza kusema kikao kisiendelee kwa hiyo tukafanya   kikao cha ndani, lakini ghafla walituvamia wakiwa na bunduki na mabomu ya machozi na kututawanya,” alisema Katani.

Mbunge huyo alidai kuwa kutokana na tukio hilo, wanaamini tamko la kuruhusiwa kufanyika mikutano ya ndani lililenga kumpa nafasi Profesa Lipumba na wanatarajia kutoa tamko leo kwa kuwa walipotaka kufanya kikao walikosa ulinzi wa polisi.

“Hii imesababisha kuamini kwamba Profesa Lipumba anatumika, maana inaonyesha wazi juzi alipokuwa Newala aliruhusiwa kufanya mkutano akiwa na ulinzi wa polisi, lakini leo (jana) sisi katika ukumbi ule ule mimi nikiwa kama mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi na mbunge wa kuchaguliwa na wananchi polisi wameshindwa kutoa ulinzi,” alisema Katani

Kamanda wa Polisi wa Mkoa, wa Mtwara, Thobias Sedoyeka alisema walilazimika kuchukua hatua hiyo kutokana na kuwapo wa dalili za vurugu kutoka pande mbili, unaomuunga mkono Maalim Seif na mwingine Profesa Lipumba.

“Pande mbili zina mgogoro kwa hiyo kulikuwa na mvutano pande zote mbili za Maalim na Profesa. Mimi nimeona kuna dalili ya vurugu na vurugu zingekuwapo hata wao wangefanya nini,” alisema Sedoyeka.

Katani pia alizungumzia taarifa zinazoenea kwenye mitandao za kukamatwa kwa wabunge wa kusini.

“Ni kweli tulikuwa Nachingwea tukitokea Ruangwa wakati tukisubiri kupata chakula tukawa tunapata kahawa na wananchi waliokuwapo pale tukawa tunabadilishana, mawazo lakini kuna watu walitoa taarifa polisi kuwa tunafanya mkutano wa hadhara na polisi walipokuja tulikwenda kituoni na kufanya majadiliano na walijiridhisha kuwa kile walichoambiwa hakikuwa sahihi,”alisema.

Hivi karibuni, Profesa Lipumba akiongozana na Mbunge wa Mtwara Mjini, Maftah Nachuma alifanya ziara mkoani Mtwara na kukutana na wafuasi wake katika Wilaya ya Mtwara na Newala akisema lengo la ziara hiyo ni kuimarisha chama.

No comments :

Post a Comment