dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Monday, June 26, 2017

Mizigo ya JPM kwa Ndugai njia panda!

Wakati Bunge la bajeti likielekea ukingoni, kuna uwezekano muda ukaongezwa kwa ajili ya kuwawezesha wabunge kuzifanyia mabadiliko sheria na sera ya madini ili kuziba mianya inayolikosesha Taifa mapato yatokanayo na rasilimali hiyo.

Uwezekano huo unatokana na kauli ya Spika wa Bunge, Job Ndugai aliyoitoa juzi wakati akiahirisha kikao cha Bunge, alipowadokezea uwezekano wa kurefushwa muda kwa ajili ya mambo muhimu.

“Msipaki (msifungashe) mizigo yenu. Hapa kazi tu,” akimaanisha kwamba kazi za kibunge zinaweza kuendelea hata baada ya Juni 30 ambayo ni tarehe ya kuahirishwa kwa Mkutano wa Saba.
Wakati akipokea ripoti ya pili ya uchunguzi wa mchanga wa madini ulio katika makontena yaliyozuiwa bandarini, Rais John Magufuli alimtaka Waziri wa Katiba na Sheria kuunda timu itakayopitia sheria za madini, gesi na mafuta na kupeleka marekebisho bungeni, akisema haitakuwa vibaya kuwaongezea wabunge siku chache kwa ajili ya suala hilo.

Rais Magufuli pia alimwambia Ndugai kwamba atafute muda kwa ajili ya kujadili na kuzifanyia mabadiliko sheria za madini na hata kama kutakuwa na gharama za ziada yeye yuko tayari kuzilipa ili kazi hiyo ifanyike kwa masilahi ya Watanzania.

“Nitakuletea hii mizigo (ripoti ya kamati) ili muweze kuipitia kule kwa masilahi mapana ya Taifa letu,” alisema Rais Magufuli akimwambia Spika Ndugai na kumsisitiza kwamba akawashughulikie wachache wanaokatisha tamaa waliojitoa mhanga kupigania maslahi ya taifa.

Kauli hiyo iliendeleza safari ya muda mrefu ya wapinzani ambao wamekuwa wakishinikiza Serikali ifanye mabadiliko ya Sheria ya Madini na mikataba yote inayosainiwa na Serikali ipelekwe bungeni na kujadiliwa kabila ya waziri kusaini.

Hata hivyo, Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu alisema haoni uwezekano wa jambo hilo kufanyika kwa sababu mpaka sasa Serikali haijapeleka bungeni muswada wa mabadiliko ya sheria na wala muswada huo haujachapishwa katika gazeti la Serikali.

Akizungumza na gazeti hili jana, Lissu, ambaye pia ni mbunge wa Singida Mashariki, alisema kawaida ya utungaji wa sheria au kufanya mabadiliko lazima muswada uchapishwe kwenye gazeti la Serikali hata kama ni kwa hati ya dharula.

Lissu alisema kuna sheria nyingi za madini ambazo zinahitaji kufanyiwa marekebisho, lakini Serikali haijaonyesha wazi ni sheria zipi ambazo wanataka zifanyiwe mabadiliko kwa ajili ya kulinda masilahi ya Taifa.

“Wakiongeza muda, tujiandae kujadili nini? Kama wanataka tujadili basi walete ripoti za kamati ya Profesa Mruma na Osoro, tuzijadili kisha tupendekeze marekebisho,” alisema Lissu na kusisitiza kwamba Serikali inaogopa kuhojiwa usahihi wa taarifa zilizotolewa kwenye ripoti hizo.

Mwanasiasa huyo alisema njia nyingine ambayo Serikali inaweza kufanya ni kupendekeza marekebisho ya sheria husika kwa kufuata taratibu zinazotakiwa kisheria ikiwa ni pamoja kuwasilisha bungeni muswada wa mabadiliko.

Lakini mbunge wa Mtwara Mjini, Hawa Ghasia alisema kutunga sheria ndiyo jukumu kubwa la wabunge wote, hivyo Serikali ikiamua Bunge liendelee kwa ajili ya kupitia upya sheria ya madini basi itakuwa hivyo.

“Serikali ikiagiza, hakuna wa kupinga. Spika ataleta ratiba itakayofuatwa na kila mbunge. Ni mapema kusema nitachangia nini kwa sababu sifahamu muswada utapendekeza mabadiliko gani,” alisema Ghasia ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ye Fedha ya Bunge.

Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara alitoa tahadhari akisema kwamba linaweza kuleta furaha miongoni mwa wabunge kutokana na kuongezeka kwa posho watakazopokea, lakini lisiwe na manufaa kwa Taifa.

Alisema hofu yake inatokana na mwenendo uliozoeleka wa Serikali kupeleka muswada huku kukiwa na maelekezo ya kujadiliwa na kupitishwa bila kutoa uhuru wa kutosha kwa wenye ufahamu na uelewa wa masuala mbalimbali kuchangia.

“Kati ya zaidi ya wabunge 360 waliopo, wenye uelewa na masuala ya madini hawazidi 10 lakini kwa kuwa viongozi wa CCM ndiyo huandaa maazimio yatakayopigiwa kura, kila muswada hupitishwa. Ipo haja ya kuzingatia taaluma za wabunge tofauti waliomo bungeni pamoja na kushirikisha wataalamu,” alisema Waitara.

Mbunge wa Mwanakwerekwe, Ally Salum Hamis alisema haamini kama kinachokusudiwa kufanywa kitakuwa na tija kwa Taifa kwa kuzingatia mikataba ya kimataifa ambayo Tanzania imesaini.

Alisema sheria ya uwekezaji iliyopo inawalinda wawekezaji ambao hawatakiwi kuingiliwa na sheria mpya yoyote ya madini au kodi itakayopitishwa na kupitishwa baada ya mikataba yao.

“Kungekuwa na nia ya dhati, muswada wa sheria usingeweka tozo ya asilimia moja ya ukaguzi wa madini yanayosafirishwa nje ya nchi. Vita dhidi ya madini ni dhahiri imefikia mwisho. Serikali imekusudia kuongeza mrabaha kwa asilimia moja,” alisema.

Alizipinga ripoti za kamati zote mbili za Rais kwamba hazikuzingatia ushirikishaji na hazikuwa huru kama inavyotakiwa. Alisema kutokana hilo, matokeo yake yatakuwa na maana kiushabiki ilhali zikikosa mantiki kisheria.

“Tulipaswa kujitoa kwenye miktaba ya kimataifa ya uwekezaji kabla ya kubadili sheria zetu,” alibainisha mbunge huyo.

Mbunge wa Mbinga Mjini, Sixtus Mapunda alitolea mfano nchi ya Ghana ambayo inapata mrabaha wa asilimia 40 na Afrika Kusini inapata mrabaha wa asilimia 39 lakini Tanzania ni asilimia tatu pekee.

Kuonyesha umuhimu wa kurekebisha sheria na sera zilizopo, Mapunda alisema hajui ni muda gani utaongezwa lakini yuko tayari kuchangia maboresho yanayohitajika kulinda rasilimali za Taifa.

Kwa kutambua uwepo wao kwenye mataifa mbalimbali, alisema: “wanachotupatia Watanzania sicho wanacholipa kwenye mataifa mengine wanakofanya biashara ileile.”

Alisisitiza kwamba hata kama tutawapoteza wawekezaji waliopo, bado Taifa linaweza kujipanga na kunufaika ipasavyo kwani ni asilimia nne tu ya hazina ya dhahabu iliyopo nchini ndiyo imechimbwa.

No comments :

Post a Comment