dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Tuesday, July 4, 2017

Serikali yakomaa na kampuni za Madini!


SASA kampuni za madini zinazofanya kazi zake nchini hazitaruhusiwa kuhifadhi fedha nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na pia mashauri ya mikataba hiyo yatafanyika ndani ya nchi na siyo katika mahakama na mabaraza ya nje, Bunge limepitisha katika kulinda rasilimali za nchi.

Aidha, Bunge limepewa nguvu ya kupitia makubaliano ya mikataba ya maliasili na rasilimali za nchi. Akiwasilisha Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Nchi kuhusiana na Umiliki wa Maliasili wa Mwaka 2017, Waziri wa Sheria na Katiba, Profesa Palamagamba Kabudi alisema sheria inaeleza kuwa mapato yote yanayotokana na rasilimali na maliasili na utafutaji, uchimbaji au umiliki na utumiaji wa rasilimali za Taifa, yanahifadhiwa katika taasisi za kifedha za ndani ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.

“Itakuwa ni kosa kuweka fedha hizo nje ya nchi isipokuwa gawiwo ambalo mwekezaji ataruhusiwa kutoa nje ya nchi kwa mujibu wa sheria za nchi za Tanzania,” alieleza Profesa Kabudi na kuongeza kuwa pia sheria inatamka kuwa mashauri kuhusu maliasili na rasilimali za nchi chini ya mamlaka ya nchi hayatafanyika chini ya mahakama na mabaraza ya nje.

Aidha, alibainisha kuwa sheria itatumika pande zote mbili za Muungano, bila kuathiri mamlaka ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar juu ya usimamizi wa rasilimali za nchi. Alisema muswada huo pia unazuia usafirishaji wa maliasili bila kuongeza thamani, lengo ni kuleta maendeleo na kutekeleza azma ya serikali ya kuwa na Tanzania ya viwanda.

Akiwasilisha Muswada wa Sheria ya Mapitio na Majadiliano kuhusu masharti hasi katika Mikataba ya Maliasili za Nchi wa Mwaka 2017, Profesa Kabudi alisema unawezesha wananchi kupitia Bunge, kupitia mikataba inayohusu rasilimali na malisiali ya nchi ambayo imefungana na Jamhuri ya Muungano kwa lengo la kujiridhisha kama masharti, makubaliano na mikataba haina masharti hasi na yanakinzana na maslahi ya wananchi na taifa kwa ujumla na kuishauri serikali.

“Sheria imeipa nguvu bunge kupitia mikataba yote inayohusiana na malisili za nchi na rasilimali zake iliyoingiwa na Jamhuri ya Muungano ili kujiridhisha masharti yaliyomo kwenye mikataba hiyo yamezingatia maslahi ya Watanzania. Na endapo mikataba haitii maslahi ya Watanzania, basi Bunge liweze kuishauri serikali kufanya majadiliano na wahusika wengine katika mikataba kwa lengo la kuondoa masharti hasi yasiyokuwa na manufaa kwa Taifa,” alifafanua.

Aliongeza “Endapo itapita kuwa sheria, serikali haitafikia makubaliano yenye tija kwa wananchi na taifa ndani ya muda utakaokubaliwa na pande zote basi masharti yote hasi yatachukuliwa kwamba yamefutwa, na si sehemu ya mikataba, na serikali haitakuwa na wajibu wowote wa kutekeleza masharti ambayo yamebainika kuwa hasi.” Profesa Kabudi alisema serikali itapitia mikataba yote ya madini ya sasa kwa kuzingatia sheria mpya zitakazopitishwa na Bunge katika Mkutano wa Bajeti unaoendelea.

Alisema mikataba yote ya madini iliyopo sasa itapitiwa upya kwa kuzingatia sheria mpya zitakazopitishwa na Bunge. Mapinduzi makubwa “Miswada hii inalenga kuleta mapinduzi makubwa katika kulinda rasilimali na maliasili ya nchi, dhana ya miswada hii ni ukombozi wetu na mapinduzi ya Watanzania wote,” alieleza Profesa Kabudi na kusisitiza umuhimu wa wabunge kupitisha miswada hiyo.

Alinukuu insha ya falsafa ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliyesema, “Mapinduzi haya yanayotakiwa ni kwa wote na si kwa wachache, tulipoonewa tulionewa wote, tuliponyonywa tulinyonywa wote, tulipopuuzwa tulipuuzwa wote, ni unyonge wetu sote kwa pamoja ndio uliotufanya tukaonewa, tukanyonywa na kupuuzwa, mapinduzi tunayoyafanya sasa, ni lazima yawe yetu kwa pamoja ili Mtanzania asiwe mnyonge, na unyonge wake ukatumiwa kumnyonya, na kupuuza.”

Miswada iliyosomwa na kujadiliwa na wabunge, kabla ya kupitisha ni Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Nchi kuhusiana na Umiliki wa Maliasili wa mwaka 2017 na ule wa sheria ya Mapitio na Majadiliano kuhusu masharti Hasi katika Mikataba ya Maliasili za Nchi wa mwaka 2017.

Maoni ya Kamati Mwenyekiti wa Kamati ya Pamoja, Dotto Biteko akitoa maoni yao kuhusu miswada yote miwili, waliitaka serikali kuboresha zaidi mifumo na uwezo wa Mahakama na vyombo vingine vya utoaji haki nchini ili vishughulikie mashauri yanayojitokeza na yatakayoweza kujitokeza kutokana na masharti ya uwekezaji yaliyomo katika miswada hiyo.

Mbunge huyo wa Bukombe alisema pia serikali ianze haraka mchakato wa ujenzi wa mitambo ya kuchakata au kuchenjua malighafi za rasilimali nchini ili kuwezesha wavunaji na rasilimali hizo kupata huduma hiyo nchini. Aidha, alisema serikali iimarishe mfumo wa utendaji wa benki na taasisi za kifedha ili kuongeza ufanisi katika kuhudumia taasisi mbalimbali na kampuni kubwa za uwekezaji nchini.

Aliishauri serikali kuhakikisha utungaji wa kanuni unafanyika mapema ili kuwezesha utekelezaji bora na wa haraka wa sheria itakayotokana na muswada. Kambi ya Upinzani Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imepinga kitendo cha Serikali au Bunge kutumia kifungu cha 5 (2) cha muswada muswada wa sheria ya mamlaka ya nchi kuhusiana na umiliki wa maliasili wa mwaka 2017 ambacho kimeweka umiliki wa rasilimali na maliasili za nchi mikononi mwa Rais kwa niaba ya wananchi wa Tanzania.

Kambi rasmi bungeni imesema kuwa kifungu hicho ni hatari ambacho kinaweza kuleta madhara makubwa kwa taifa kisipoangaliwa kwa nidhamu ya hali ya juu na kwa uzalendo uliotukuka kwani endapo anaweza kupatikana rais ambaye si mzalendo nchi inaweza kutumbukia pabaya.

“Mikataba hii imezipa kinga kubwa sana kampuni za madini ambazo zimesaini mikataba na serikali na ikiwa ni pamoja na kuzuia kutumika kwa sheria mpya ambazo zinapitishwa na Bunge kwa kampuni hizo kuanzia mikataba hiyo inaposainiwa,” yalikuwa maoni ya Upinzani yaliyosomwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Cecilia Paresso.

Naye John Heche akiwasilisha maoni ya Wizara ya Katiba na Sheria kuhusu Muswada wa Sheria ya Mapitio na Majadiliano kuhusu masharti hasi katika mikataba inayohusu maliasili za nchi wa mwaka 2017, alieleza kuwa Upinzani umekuwa ukikemea suala la kupeleka bungeni miswada ya sheria Bungeni kwa hati ya dharura.

Akichangia, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema) alisema Bunge linapotunga sheria ni wakati muhimu wa kuwa makini na kwamba miswada hiyo ilihitaji muda wa kutosha.

Alisema anataka kuamini kuwa Rais aliyepo ni mzalendo na anapenda watu. “Najiuliza kwa mamlaka aliyopewa Rais siku akija mtu si mzalendo kama Magufuli nataka kuamini hivyo akatokea hata upande huu hata Chadema kwa sababu huku hakuna malaika au akitokea CUF nako hakuna malaika, akatokea rais sio mwaminifu na amepewa mamlaka kubwa ya kusimamia rasilimali basi atauza taifa hili,” alieleza Lema.

Mbunge wa Geita Vijiji, Joseph Msukuma (CCM) aliwashangaa wabunge wanaopinga miswada hiyo kuletwa kwa hati ya dharura na kuhoji kuwa mbona mgombea wa urais kupitia Ukawa, Edward Lowassa alipatikana kwa hati ya dharura.

“Hata mgombea urais wa upande mwingine (Chadema) walipata mgombea kwa hati ya dharura, walimuona anafaa kwa dharura waliokuwa nayo, walimpata bila kumchunguza huku wakijua kuwa walileta mtu ambaye wanataka akabidhiwe nchi, na hajui chochote kuhusu Chadema na wananchi hawakuwahoji,” alisema.

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), alisema “sheria hizi mbili za kimapinduzi kwamba chochote kilichopo juu na chini kwenye nchi yetu ni mali yetu, lakini mfumo wa uzalishaji, mfumo ni uleule, sheria iliyopita ina umiliki, sheria ya mwaka 1979 ilikuwa na umiliki, si jambo jipya, jambo jipya tubadilishe mfumo wa uwekezaji.”

Alipendekeza kuwa badala ya kuwapa uwekezaji, serikali imiliki rasilimali hizo na kutoa ukandarasi kwa kampuni kutoka nje ili wakichimba faida igawanywe kulingana na makubaliano.

No comments :

Post a Comment