dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Saturday, August 24, 2019

MHE. ISMAIL JUSSA AMLILIA AUNTY KHADIJA!

Zanzibar imeondokewa. Kwa hakika Bibi Khadija Omar Baramia, ambaye wengi wetu wa rika letu tulizoea kumwita Aunty Khadija, alikuwa ni alama (icon) miongoni mwa alama za Zanzibar. 

Aunty Khadija alifahamika zaidi kwenye sanaa ya muziki wa Taarab, tena ile Taarab khasa siyo hizi za sasa zinazolazimishwa kuitwa Taarab wakati hazina hata moja katika ladha za Taarab. Alikuwa gwiji katika utunzi wa mashairi ya Taarab, utiaji muziki na uimbaji wa Taarab aliyelimudu vyema jukwaa. Unaweza kusema jukwaa likijiona limepata heshima linaposimamwa na muimbaji wa hadhi ya Aunty Khadija. Ukiliona hilo kwa jinsi muda wote anavyokuwa na bashasha na kuwasiliana na hadhira yake kwa tabasam wakati akiwatumbuiza.

Jina la Aunty Khadija katika ulimwengu wa Taarab liling'ara kuanzia kwao Zanzibar, Mwambao wa Pwani ya Afrika Mashariki, Oman, Dubai hadi Ulaya alikopata nafasi za kualikwa. Lakini licha ya kujenga jina kubwa, hilo halikumpa majivuno wala kujikweza. Alikuwa mtu wa watu khasa; wa rika zote, wa daraja zote, wa kabila zote, wa rangi zote na wa dini zote. 


Kitu kingine kilichokuwa dhahiri kwake kilikuwa ni kipaji cha uongozi alichokuwa amejaaliwa na Mola wake. Popote alipokuwapo alijitokeza na kukubalika kama kiongozi, kwa ile sifa ambayo wengine husema ni kiongozi kwa maumbile (natural leader). Amelisema hili gwiji mwengine wa fani za sanaa ya Taarab na Habari hapa Zanzibar, Bi Maryam Hamdan na bila shaka litathibitishwa na kila aliyemjua Aunty Khadija.

Mimi nikimkumbuka miaka yake ya mwisho mwisho kabla ya kustaafu kazini alipokuwa akifanya kazi Wizara ya Kilimo Zanzibar katika miaka ya mwishoni ya 80 na hata huko waliokuwa wafanyakazi wenziwe wakiutaja uwezo wake ambao katika zama hizo zilizokuwa bado masuala ya nafasi ya mwanamke ikionekana ni ya kuongozwa tu, basi yeye alijichomoza kwamba ni mwenye uwezo wa kuwaongoza wenziwe.

Ukiwachilia hayo, Aunty Khadija alikuwa mzalendo wa kweli wa nchi yake Zanzibar ambayo akiipenda ndani ya roho yake. Katika hili nisingependa kuandika zaidi.

Kuna jambo moja ambalo sisi wa rika letu mwanzoni tukilisikia kwa wazee ambalo lilikuwa daima katika nafsi yake lakini baadaye akaja akalisema mwenyewe - ni kuhusu uchungu na huzuni aliyokuwa nayo kwa kuondokewa na mumewe, Marehemu Mikidadi Abdalla Ali Kayaya (Meki) ambaye aliuawa kikatili akiwa gerezani katika miaka ya mwanzoni ya 70.

Tulikuja kulijua hili kupitia makala aliyoandika mzee wetu Al Marhum Ali Nabwa katika gazeti la Dira kuhusu wasfu wa mama yetu, Aunty Khadija. Katika makala yale ambayo aliyaandika baada ya kumfanyia mahojiano, Marhuma Aunty Khadija alieleza kwamba mara ya mwanzo alipoimba nyimbo ya 'Madhulumu Moyo' ambayo aliitunga mwenyewe ilikuwa ndani ya Ngome Kongwe na alishindwa kuimaliza baada ya kujawa na huzuni na kulia kwa kwikwi akiwa jukwaani alipomkumbuka mumewe. Katika nyimbo hii anazungumza na dunia kuhusu masaiba yaliyompata huku akimuomba Mola amjaalie awe mwenye kumtii licha ya mtihani huo.

Haitakuwa kumtendea haki Marhuma Aunty Khadija ikiwa nitamaliza kuandika haya machache nilojaaliwa kuyaandika ikiwa tutawacha watu wadhani kwamba Marhuma alikuwa wa haya tu yaliyojulikana na kila mtu. Jambo moja ambalo amelifanya sana na tunapaswa kumkumbuka nalo pia ni khairati nyingi alizotenda. Alisimamia ujenzi wa misikiti, madrasa na pia sehemu za kukoshea maiti. Mwenyezi Mungu Amlipe jaza ya kheri na hayo na mengine ya kheri yawe sababu ya kumuingiza katika rehema zake na Pepo yake tukufu.

Tunamuomba Mwenyezi Mungu Amsamehe yeye na wazee na ndugu zetu wote waliotangulia mbele ya haki na Atusamehe na sisi na Awalaze wote mahali pema Peponi, na sisi Atujaalie husnul khatima. Amin.

Tangulia Aunty Khadija. Na sisi tuko nyuma. Kwani sote tumetoka kwa Mwenyezi Mungu na Kwake Yeye ndiyo marejeleo yetu.

Inna Lillaahi wa Inna Ilayhi Rajiu'n. 

By Ismail Jussa Ladu

No comments :

Post a Comment