NIONAVYO…............
Written by Stonetown (Kiongozi) // 12/10/2012
Zanzibar ya vyama vingi imepitia hatua na nyakati tafauti za mashakili na majaribu yasiyoelezeka. Majaribu hayo yliyoandamana na madhila, mateso, manyanyaso, mapigo, masusiano, na hata utengano wa familia kadhaa ukihitimishwa na vifo vya watu ni matokeo ya mapambano na msigano kati ya vyama viwili vikuu vya kisiasa hapa nchini yaani CCM na CUF.
Ifahamike Kuwa mashakili na majaribu yote hayo walioathirika na wanaoendelea kuathirika ni wananchi na hasa hasa waumini wa chama cha CUF. Sioni ubaya kuwakumbusha baadhi ya madhila ambayo yamewapata wananchi katika kuitetea CUF na kudai maendeleo ya nchi yao ambayo kwa muda sasa imekuwa ikibanangwa na kuliwa na wenye mumluku pamoja na familia zao huku akina sisi tukibaki kutia viraka juu ya vihasho kwa dhiki na shida za maisha zisizokwisha.
Ikumbukwe mara tu baada ya kuanzishwa chama cha CUF, mwaka 1992 amani ya nchi hii ilitoweka. Tukianza na mauwaji ya watu wawili kule Shumba mjini, wilaya ya Micheweni Pemba, tukaja na miaka ya 1995 ambapo jeshi la polisi FFU (Wakati huo Melody) walivyovihanikiza kwa kipigo vijiji vya kiungoni na Pembeni Shengejuu kwa muda wa miezi huku watu wakihama majumba yao na kuacha mali zao zikienda na maji.
Tukumbuke watu waliojifia siku matokeo yalipotoka ya Urais 1995, na wale waliofikwa na haja kubwa mbele ya kadamnasi ya watu wakapata kibuhuti na hizaya hadi wamekata roho, kwa ajili ya CUF.Tuangalie kaumu ya wanafunzi kutoka Pemba 1996, iliyofukuzwa masomo kwa kugoma huku wakidai haki yao ya kupiga kura. Wengi wao walipata tabu mno na ikawa hasara kubwa kwa taifa lisilo kuwa na dira wala huruma ya raia wake dhaifu.
Ifahamike kuwa kaumu kubwa ya nguvu kazi ya Zanzibar ilikimbia nchi baina ya mwaka 1995-2000 kulekea ughaibuni baada ya kukatishwa tamaa na nchi yao. Tukumbuke kuwa viongozi 18 wa CUF walitiwa ndani kwa miaka miwili lakini kwa bahati nzuri ‘hawakuoza kwani si mapapai’. Tukumbuke roho zilivyosaga mwaka 2001 baada ya maandamano ya amani kuvurugwa na jeshi la polisi. Tukumbuke madhila na idhilali iliyofanya na ‘Janjaweed’ katika uchaguzi wa 2005, na wana CUF kutolewa makazini, kubaguliwa na hata kunyimwa haki yao ya kura. ‘Wao haya wana mji wao’ pia msiisahau.
Mungu akaleta shufaa. Yakaletwa maridhiano ya kwanza ya ukweli ( baada ya mawili ya kinafiki kutofanikiwa). Uchaguzi wa 2010 ukawa afadhali na karibu ya kusema tushukuru. Tukumbuke kuwa zamani Baraza la wawakilishi ilikuwa hoja yoyote ya CUF hata iwe imetoka ‘Bait’l’muqaddas’ basi CCM wakiipinga na CUF ndio hivyo hivyo. Hapakuwa na jambo, ni vurugu mechi tu.
Leo hii kule bondeni Chukwani, wawakilishi wote lao moja. CCM na CUF msimamo mmoja. Viongozi na wananchi wako karibu na wananchi si kama zamani.Hakuna mambo ya U-CCM na U-CUF kama ilivyokuwa zamani. CCM na CUF waombana moto na chumvi, hili ni jambo adhimu na adimu sana katika medani za siasa za hapa kwetu.Haya ni mambo yaliyokuwa hayakionekana sana hapa wala kufikiriwa kuwa yangetokea kwa tulikotoka.
Cha ajabu, katika zama hii ya maridhiano ambapo wenzetu wa CCM wanakubaliana na wenzao kwa mambo hata yasiokubaliana kisera na kiitikadi, inashangaza sana kuona kuwa wawakilishi wa CUF wamefanya tena jaribio la kitoto kabisa na kuirudisha tena nchi hii nyuma. Bila shaka kitendo cha wawakilishi wa CUF kutoka barazani kinachukuliwa kama ni cha hekima na busara na waumini madhubuti wa CUF, lakini si hivyo kabisa. Tukio hili limeishushia hadhi CUF na viongozi wake na hata maridhiano kwani limeoneshea wazi kuwa hakukuwa na maridhiano ya ndani ya moyo.Ni mdomoni tu na ya kinafikinafiki.
Nasema hivi kwa sababu sasa wale wenzao wa CCM hawatakubali tena kuwaunga mkono kwa hoja zozote kwani wanaonekana kuwa hawajawa tayari wala hawajawa na kifua cha kuyabeba yote ‘mabaya na mema’. Maridhiano ni kama ndoa, tena pengine ya uke wenza, ina mazuri na mabaya lakini tunasema mambo ya nyumba kunga, makuti kuunga unga. Ustahamilivu ni lazima katika mahusiano na makubaliano kama haya. CUF ilikuwa itazame mbele na isahau kabisa kutumia gia ya ‘reverse’ wakati kama huu wa kupandisha kilima, kilima chenye tope za udongo wa mfinyanzi, tena uliorowa, udongo wa kujipapatuwa na Muungano.
Naamini kitendo hichi kinaturudisha kule kwenye baraza la wawakilishi la 1995, ambapo wana CUF walisusia vikao vyote mpaka wakafukuzwa wala hatukuona kilichopatikana. Na kwa hili ni yale yale ya njweo, kaskazi kuvumia machweo.Tusema iwe kweli uchaguzi wa Bububu uliomuweka madarakani Mh. Hussein Makungu (BHAA STYLE) ulijawa na mauzauza na machapa kungu mengi kutoka kwa wapinzani wao CCM, lakini tujiulize kwani hali kama hio imefanyika mara ngapi? Tutasema nyingi. Na jee CUF iligoma mara ngapi? Nyingi! Wamepata lipi? Kuingia umoja wa Kitaifa labda.
Nionavyo, CUF hapa imeteleza! Na nina hofu kubwa ya kwamba tunaweza kurudi nyuma hatua mia au zaidi kwa hili. Isitoshe, tuko katika wakati mgumu wa vita. Mapambano ya kitaifa dhidi ya Muungano, leo ikiwa yale ya wakti wa Fadau yanarudishwa tena na CUF, tutafika? Ifike wakati ndugu zangu wa CUF mpevuke kiakili, kisiasa na kidiplomaisia.
Kitendo hichi kusema kweli hakiiisaidii sana CUF, nchi yetu wala wananchi ambao wengi wanaamini kila wanachofanya CUF ni sawa tu! Kwa hili mmekanyaga msoo! Acheni utamaduni huu, na rudisheni kauli yenu ya kutompa mashirikianao mwakilishi mpya wa Bububu, kwani malipo na matokeo yake ni wenzenu wa CCM kusema hawatawapa ushirikiano wowote katika baraza la wawaikilishi. Sasa je hapo mtakuwa mmejenga au mmevunja? Mmetuunganisha au mmetutenganisha?La Muungano halijesha, mumeshika la migongano. Langu jicho!
Chanzo: Mzalendo
No comments :
Post a Comment