Marekani yatenga bilioni 15.7/- kupambana na Ukimwi nchini
13th October 2012
Shirika la kimataifa la misaada la Marekani (USAID) limetenga Dola za Marekani milioni 10 (sh bilioni 15.7) kwa ajili ya mradi wa kuziwezesha asasi za kiraia zinazopambana na Ukimwi (BOCAR) kutoka mikoa ya Tanzania bara na Zanzibar.
Mratibu wa Mafunzo hayo Sylvester Hanga, kutoka BOCAR unaofadhiliwa na USAID, alisema mradi huo unatarajiwa kutekelezwa katika kipindi cha awamu tatu kwa miaka mitano, ambapo wafanyakazi 66 wa asasi hizo wanaratarajiwa kunufaika na mafunzo hayo.
Akiongea na waandishi wa habari wakati wa mafunzo hayo yanayoendelea katika awamu ya tatu mjini Morogoro, Hanga alisema kuwa jumla ya asasi 27 kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania bara na Zanzibar zimeshapatiwa mafunzo kama hayo ya uwekaji kumbukumbu (documentation and communication).
“Tayari mafunzo kama hayo yalishafanyika kwaajili ya asasi zinazofadhiliwa na mfuko wa Ukimwi, Rapid Funding Envelope (RFE), katika Kanda ya Ziwa na Nyanda za Juu Kusini nia ikiwa ni kuwapatia stadi za uwekaji wa kumbukumbu na mawasiliano ya miradi wanayoitekeleza,”alisema Hanga.
Aliongeza kuwa madhumuni mengine ya kutoa mafunzo hayo, ni kuwapatia mbinu za kujenga haiba ya taasisi zao na namna ya kufanya kazi na vyombo vya habari.
RFE imetoa ruzuku kwa asasi 32 katika awamu ya tisa ili kutekeleza miradi ya kupunguza maambukizi ya virusi vya Ukimwi, watoto yatima wanaoishi katika mazingira hatarishi (OVC) na kupunguza ukatili na unyanyasaji wa kijinsia hasa kwa watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi.
Kwa upande wao washiriki wanaopatiwa mafunzo kwa awamu ya tatu, walieleza matarajio yao ya kunufaika na mafunzo hayo ambayo yatawezesha kuibua kwa kina yale wanayoyafanyia kazi katika mashirika hayo na jamii iweze kufahamu kinachoendelea hasa katika harakati za mapambano dhidi ya Ukimwi.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment