dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Friday, May 31, 2013

Dk Shein : Zanzibar inathamini mchango mkubwa wa China kwa sekta ya afya

CHINA-BEIJING-XI JINPING-ZANZIBAR-MEETING (CN)

Na Said Ameir , Nanjing China
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema Serikali na wananchi wa Zanzibar wanathamini na kujivunia mchango mkubwa ambao umekuwa ukitolewa na wataalamu wa afya kutoka Jamhuri ya Watu wa China.
Dk. Shein ametoa kauli hiyo jana wakati alipokuwa akizungumza na baadhi ya wataalamu wa afya wa China waliowahi kufanya kazi Zanzibar pamoja na madaktari na watumishi wa hospitali ya Drum Tower ya mjini wa Najing katika jimbo la Jiangsu, China.
“Timu za wataalamu wa kichina zinastahiki heshma ya pekee kutoka kwetu Serikali na wananchi wa Zanzibar kwa mchango wao waliotoa wakati wote wa ushirikiano wetu katika sekta hiyo tangu mwaka 1964”alieleza Dk. Shein.
Dk. Shein na ujumbe wake ulipokelewa kwa shangwe na bashasha ulipowasili katika hospitali hiyo ambako alikutana na wataalamu ambao baadhi yao yeye na Mke wake Mama Mwanamwema Shein waliwahi kufanyakazi nao katika utumishi wao kwenye sekta ya afya.
“Nilipomuona Bibi Yang nimekumbuka enzi zangu nilipokuwa katika hospitali ya Mnazi Mmoja halikadhalika Bibi Lin ambaye nilikuwa nikikutana nae mara kwa mara nilipokwenda Pemba katika hospitali ya Abdalla Mzee Mkoani”alieleza Dk. Shein na kuvuta hisia za kila aliyekuwepo katika mkutano huo.
Aliwaeleza wataalamu hao kuwa Serikali na wananchi wa Zanzibar inawathamini sana na kuwa wameacha kumbukumbu nzuri kuwa ni watu wachapakazi na wenye upendo kwa wagonjwa.
“Mlifanyakazi bila ya kusita kila mlipohitajika na kuonyesha umahiri mkubwa katika kazi yenu na kuokoa maisha ya watu wetu wengi na wakati mwingine mlifanya mambo hayakuwahi kufanywa kabla ya Mapinduzi…tunawashukuru sana” Dk. Shein aliongeza.
Alifafanua kuwa utendaji wao makini katika kuwahudumia wagonjwa na kufanya tafiti za afya kumeacha utaalamu na maarifa kwa wataalamu wa Zanzibar na kwamba hiyo ni mojawapo ya kumbukumbu nzuri ya utendaji wao katika hospitali za Zanzibar.
Dk. Shein ameeleza kuwa miaka 49 ya wataalamu wa China kutoa huduma za afya Zanzibar imepitia changamoto mbalimbali lakini hilo halikuzuia nchi hizo kusaidiana.
“Mlitusaidia hata katika kipindi kigumu kwenu  hivyo nyinyi ni ndugu zetu. Miaka 49 ya utoaji huduma imeleta matokeo mazuri hivyo tuna kila sababu kuendeleza na kuimarisha ushirikiano wetu” Dk. Shein alieleza.
Akizungumza kwa niaba ya wataalamu hao Professa Li Dongsheng ambaye aliwahi kufanyakazi Zanzibar kati ya mwaka 1977 na 1979 na ambaye sasa ana umri wa miaka 82 amesema kuwa kufanyakazi kwao Zanzibar ni sehemu ya kumbukumbu ya maisha yao ambayo hawawezi kuisahau.
“Wote tumeguswa na urafiki, upendo na wema wa Serikali na wananchi wa Zanzibar   wakati wote tuliokuwepo kule.Tuna kumbukumbu nzuri ambayo hatuwezi kuisahau” alieleza Profesa Li na kutoa shukurani zake kwa Serikali na wananchi wa Zanzibar.
Alieleza kuwa baada ya kurejea nchini kwake alipewa jukumu katika Idara ya ushirikiano wa masuala ya afya na aliweza kutembelea Zanzibar mara nyingi kuangalia maendeleo ya wataalamu wa kichina huko.
Rais ambaye yuko nchini China kwa ziara ya siku saba aliwaeleza wataalamu hao kuwa ziara yake nchini China iliyomuwezesha kukutana na baadhi yao ni kitendo cha kihistoria na kuahidi kuenzi mchango wa wataalamu hao.
Hadi sasa China imeshapeleka timu 24 za madaktari Zanzibar na timu ya 25 inatarajiwa kwenda huko hivi karibuni. Madaktari hao hufanya kazi katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja na Hospitali ya Abdalla Mzee huko Mkoani Pemba. Miongoni mwa watakaokwenda huko ni daktari bingwa wa maradhi ya moyo Dk. Liu Yaping na daktari bingwa wa upasuaji Dk. Yu Zhongjie ambao walikuwepo katika mkutano huo.
Katika ukumbi wa mikutano wa hospitali hiyo kuna picha kubwa ya kuchora inayoonyesha timu ya kwanza ya wataalamu kutoka china mwaka 1964 ambayo inawaonyesha wakiwa na Rais wa Kwanza wa Zanzibar Mzee Abeid Amani Karume, Mzee Thabit Kombo Jecha na Mzee Rashid Mfaume Kawawa.
Dk. Shein anamaliza ziara yake katika jimbo la Jiangsu leo kwa kutembelea kumbukumbu ya Dk. Sun Yat-sen na baadae atasafiri hadi Xiamen kwa ziara ya siku tatu kukamilisha ziara yake ya siku saba nchini China.

Chanzo: Zanzinews

No comments :

Post a Comment