Viongozi wa Serikali na wale wa Kisiasa wanapaswa kuzielewa vyema sheria za Utawala ili waweze kutumia vizuri madaraka yao na kwa uadilifu katika kuwahudumia wananchi wanaowasiamia na wale wanaowaongoza.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akiifungua Semina ya siku mbili ya kuimarisha uhusiano baina ya Viongozi wa Kisiasa na watendaji kutoka Serikalini na Baraza la Wawakilishi inayofanyika katika ukumbi wa Zanzibar Beach Resort uliopo Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Balozi Seif alisema ufahamu mzuri wa Sheria za Utawala utawezesha kuelewa kuwa madaraka yoyote waliyonayo Viongozi hao wanayatumia kwa maslahi ya umma na kwa mujibu wa Sheria.
Alisema utekelezaji wa shughuli za kila muhimili unaweza kudhoofisha uhusiano mzuri baina ya mihimili iliyopo Nchini endapo utakosekana ufahamu wa sheria na kupelekea migongano na mivutano kati ya Baraza la Wawakilishi na Taasisi za Serikali.
Balozi Seif alitahadharisha kwamba hatua hiyo kwa kiasi kikubwa inaweza kupotosha lengo la mgawanyo wa madaraka ambalo ni kuwapatia mafanikio na maendeleo Wananchi walio wengi hapa Nchini.“ Haitakuwa jambo la busara endapo Kiongozi yeyote yule atachukua msimamo wa kutekeleza majukumu yake kwa namna itakayohatarisha amani ya Nchi au kuvuruga Umoja tulionao “. Alisisitiza Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwanasihi washiriki wa semina hiyo kuzingatia daima kuwa Uongozi ni dhamana ambayo inapaswa kutumika kwa faida ya Nchi na Wananchi.
“ Viongozi tusitumie vibaya dhamana tulizopewa kwa kuvuruga mahusiano mazuri yaliyopo baina yetu au kwa kutumia vibaya vyeo vyetu dhidi ya watu wasiostahiki kufanyiwa dhulma hizo “. Aliongeza Balozi Seif.
Alilishukuru Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa { UNDP } pamoja na Uongozi wa Baraza la Wawakilishi kwa kuridhia semina hiyo ifadhiliwe kupitia program ya kufadhili Mabunge licha ya kuwa semina hiyo haikuwemo katika shughuli zilizopangwa kwa robo ya Mwaka.
Alisema Serikali imejiwekea utaratibu wa kufanya semina mbali mbali kwa Viongozi wa Kisiasa na Kiutendaji kwa shabaha ya kukumbushana kuhusu majukumu na wajibu wa msingi walionao Viongozi katika kuwatumikia Wananchi.
Naye Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mh. Pandu Ameir Kificho alisema kwamba mamlaka ya kuendesha Nchi yako kwenye dhamana ya Wananchi wenyewe na Kiongozi au Mtu aliyepewa jukumu la kusimamia ya Jamii aelewe kuwa amebeba dhima hiyo.
Mh. Kificho ambae ni Mwenyekiti Mwenza wa Semina hiyo aliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa wazo lake la kuandaa semina iliyowakutanisha Viongozi wa Serikali na Siasa ambayo ni muhimu kwa hatma njema ya Wananachi wa Zanzibar.
Akitoa salamu za Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mtaifa { UNDP } lililodhamini Semina hiyo Naibu Mkurugenzi wa Shirika hilo Nchini Tanzania Bibi Andisa Mashologu alisema Shirika hilo litaendelea kuunga mkono harakati za Kijamii katika kuwajengea uwezo Wananachi katika mipango yao ya Maendeleo.
Bibi Andisa alisema hatua hiyo itasaidia kujenga utulivu miongoni mwa Wananchi na viongozi wao na hatimae kutanuka zaidi kwa Demokrasia kati ya makundi ya watu wa rika na itikadi tofauti Nchini.
Semina hiyo ya siku mbili ya kuimarisha uhusiano baina ya Viongozi wa Kisiasa na watendaji kutoka Serikalini na Baraza la Wawakilishi imebeba mada nane ikiwemo jukumu la Baraza la Wawakilishi katika kusimamia Serikali.
Chanzo: ZanzibariYetu
No comments :
Post a Comment