Rais Uhuru Kenyatta akiwasili mjini Nairobi hivi karibuni baada ya kutoka katika moja ya safari zake za nje ya nchi. Picha ya maktaba.
Nairobi, Kenya. Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ameingia katika mjadala mzito wa wananchi wa kutokana na mfululizo wa ziara zake anazofanya nje ya nchi.
Hadi sasa ripoti zinasema kuwa kiongozi huyo amefanya ziara 43 nje ya nchi tangu aingie madarakani miaka mitatu iliyopita.
Vilevile, Alhamisi wiki hii anatarajiwa kuzuru Kigali nchini Rwanda kwa ziara ya kiserikali.
Ziara hizo zimeonyesha kuwakera wananchi wengi ambao wameingia kwenye mitandao ya kijamii na kuzikosoa.
Rais Kenyatta hivi karibuni alizuru nchini Ufaransa kuhudhuria mkutano unaoendelea wa Umoja wa Mataifa (UN) kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa duniani .
Baada ya mkutano huo alielekea nchini Afrika Kusini kuhudhuria mkutano mwingine wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika, uliomalizika mwishoni mwa wiki iliyopita.
Katika kipindi cha siku mbili sasa, kumekuwa kukisambazwa ujumbe wa aina mbalimbali kukejeli safari za kiongozi huyo ambaye pia hivi karibuni alipokea wageni kadhaa wakiwamo Kiongozi wa Katoliki Duniani, Papa Francis na Rais wa Marekani , Barrack Obama.
Katika majadiliano hayo wengine wamekwenda mbali zaidi wakilinganisha ziara za kiongozi huyo na watangulizi wake.
Wamekuwa wakisema kuwa Rais Kenyatta amefanya ziara 43 tangu aingie madarakani ambazo zinazidi 33 za nje ya nchi alizofanya mtangulizi wake, Mwai Kibaki katika kipindi cha miaka 10 aliyokuwa rais wa Kenya.
Kwa mujibu wa gazeti la Daily Nation, ziara hizo za Rais Kenyatta zinakadiriwa kugharimu Sh2.1 bilioni.
Hata hivyo juzi, Ikulu ya Kenya ilitoa taarifa ikitetea ziara za kiongozi huyo kuwa zimekuwa na tija kubwa kwa nchi hiyo na wananchi wake.
/Mwananchi.
No comments :
Post a Comment