NA MHARIRI
6th December 2015.
Wafanyabiashara mbalimbali waliokuwa wamekwepa kulipa kodi kwa kupitisha kinyemela mizigo bandarini wamelipa jumla ya bilioni 5/- kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ikiwa ni siku moja tu baada ya mkutano wa Rais Dk. Magufuli na wafanyabiashara wakubwa nchini uliofanyika katikati ya wiki hii jijini Dar es Salaam.
Wakati wa mkutano huo, Rais Magufuli aliwapa siku saba za kulipa kodi kwa bidhaa zote walizopitisha bandarini hapo bila kulipia ushuru, akisisitiza kuwa baada ya muda huo kupita, wote waliokwepa kulipa kodi watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.
Kaimu Kamishna Mkuu wa TRA, Dk. Philip Mpango alisema kampuni nne ziliwasilisha fedha hizo ikiwamo kampuni ya Said Salim Bakhresa and Company Ltd ambayo iliyolipa bilioni 2.1/-, alitaja kampuni nyingine kuwa ni Tuff Tyres Centre Co. Ltd ambayo ililipa bilioni 1/-, Binslum Tyre bilioni 2.5/- na makampuni mengine yalikuwa yakiendelea kulipa.Huo nI mwitikio mzuri, na tunaamini wafanyabiashara werngine wataendelea kulipa kodi walizozikwepa kwa uaminifu na kwa kuthamini wajibu wao wa msingi wa kulipa kodi kwa hiari.
Tunaamini kuwa utaratibu wa kuorodhesha wafanyabiashara wote waliokwepa kulipa kodi unaendelea kwa idara na taasisi zote nchini, nia kubwa ikiwa ni kuhakikisha wote wanalipa ushuru unaotakiwa kwa mujibu wa taratibu na sheria za nchi.
Kazi kubwa ya operesheni hii ya ufuatiliaji wa kodi za serikali imeanza kwa maeneo ya hapa Dar es Salaam, tunaamini vipo vituo vingi nchini ambavyo vinakusanya ushuru wa kodi mbalimbali, zikiwamo ofisi za forodha ndani ya mipaka ya nchi tunazopakana. Tunaamini pia kuwa ni kutokana na fedha zitokanazo na kodi mbalimbali ndipo serikali inapokuwa na uwezo mkubwa kiuchumi kujiendesha katika miradi mingi yenye faida kwa jamii ya Watanzania.
Kimsingi uchumi wa nchi unategemea kwa kiasi kikubwa makusanyo ya kodi mbalimbali kutoka idara na sekta zote, watendaji wake wanatakiwa kuwa waadilifu na wanaoelewa kuwa dhamana waliyo nayo inabeba majukumu makubwa ya maendeleo ya uchumi wa taifa.
Imedhihirika kuwa kwa kipindi kirefu sasa, baadhi ya watumishi wamekuwa siyo waaminifu, wamekuwa wakijilimbikizia mali iliyotokana na rasilimali za umma kwa faida yao binafsi, na ndio maana ukwepaji wa kodi katika vyanzo mbalimbali vya mapato ya taifa limekuwa jambo lililozoeleka.
Kwanza tunapongeza jitihada za serikali hii ya awamu ya tano kwa kujitoa katika operesheni hii kubwa ya kubana mianya ya rushwa pamoja na ufisadi katika sekta nyeti kama bandari na Mamlaka ya Mapato Tanzania ambako fedha nyingi za umma zimepotea katika mazingira ya kifisadi na rushwa iliyokithiri. Rais Magufuli alipotangaza kuwa kazi yake ya kwanza akiingia Ikulu itakuwa ni kazi tu ya kusafisha uovu wote wa wafuja fedha za umma na kuhakikisha mapato ya serikali yananufaisha wananchi wote hasa wale maskini wa kipato cha chini kabisa, wengi walidhani ni siasa, lakini sasa wanaamini kuwa dhamira aliyojiwekea inatekelezeka.
Hatua zinazochukuliwa sasa ni kielelezo cha dhamira madhubuti ya Rais Magufuli ya kurejesha uchumi wa nchi utakaowanufaisha wananchi wote, tunaamini kila idara ya serikali pamoja na taasisi binafsi zitatoa ushirikiano katika kazi hii kubwa ya kutumbua ‘majibu’ yaliyojaa ufisadi unaoangamiza uchumi wa nchi yetu.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments :
Post a Comment