ALIYEKUWA Mkurugenzi wa Intelijensia ya Makosa ya Jinai, Kamishna wa Polisi Valentino Mlowola, ameteuliwa kuwa Naibu Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Ofisa Uhusiano wa Takukuru, Doreen Kapwani, ilieleza kuwa uteuzi huo ulioanza Oktoba 23 umejaza nafasi ya Lilian Mashaka ambaye aliteuliwa kuwa Jaji ya Mahakama Kuu kuanzia Agosti 8.
Mlowola ambaye alikuwa makao makuu ya polisi anaingia Takukuru kurithi nafasi iliyoachwa na Mashaka huku kukiwa na changamoto lukuki zinazoiandama taasisi hiyo, kubwa ikiwa malalamiko ya kesi ya vigogo wa ufisadi kuchukua muda mrefu kuchunguzwa kabla ya kufunguliwa mashtaka mahakamani.
Aidha, Mlowola atakabiliana na changamoto ya kuendana na kasi ya utendaji kazi wa Rais John Magufuli ambaye amekwishaanza kutekeleza kwa vitendo ahadi alizozitoa wakati wa kampeni za kupambana na mafisadi kwa kuunda mahakama maalumu itakayowashughulikia mafisadi.
Kabla ya kushika wadhifa wa Mkurugenzi wa Intelijensia, Mlowola alikuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza uteuzi ambao uliishia Mei, 2015 na aliteuliwa na Rais wa Awamu Nne, Jakaya Kikwete kuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Oktoba 23.
No comments :
Post a Comment