Mbunge wa Jimbo la Kibamba, John Mnyika, ameomba ripoti za kamati za uchunguzi zilizoundwa na mawaziri wa Wizara ya Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe na Samuel Sitta, kuhusu Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) ziwekwe hadharani.
Amesema kuwekwa hadharani kwa ripoti hizo kutaondoa usiri na kusaidia kubaini ufisadi uliokithiri katika mamlaka hiyo ili hatua za kuwasimamisha vigogo wa TPA na wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ziwe na mafanikio.
Mnyika ambaye amekua kimya kwa muda mrefu tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu Oktoba 25, mwaka huu, alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari, jijini la Dar es Salaam jana.
“Kama kweli serikali ya awamu ya tano ina lengo la kufichua mafisadi, inapaswa kuweka wazi ripoti mbalimbali za uchunguzi ili ziwe dira ya kujua kiini cha matatizo kujitokeza katika mamlaka hiyo,” alisema na kuongeza:“Nafahamu yapo mambo mazuri kwa nchi yaliyonainishwa, lakini kutokana na ripoti hizo kuwa siri hakuna anayejua huku fedha za walipa kodi zikiwa zimetumika bila mafanikio. Dawa ya jipu siyo kulitumbua bali ni kulipasua ili kiini cha ndani kitoke, ukikiacha jipu linaanza kuvimba upya tena linakuwa hatari zaidi.”
Aidha, Mnyika alisema wakati wa kampeni, Rais Dk. John Magufuli, aliahidi kutatua tatizo la maji na kumtaka kutekeleza ahadi hiyo kwa kutembelea mradi wa maji wa Ruvu Juu ili apasuwe majipu yaliyoiva.
Alisema iwapo Rais atatembelea mtambo huo atabaini ufisadi unaokwamisha ulazaji wa mabomba ya Mchina yasitoe maji, pampu za maji kuharibika mara kwa mara na mradi wa maji kutoka Mlandizi hadi Kimara kukwama wakati fedha zimetolewa.
“Wizara ya maji ilisema bungeni kuwa ulazaji wa mabomba ya maji ulifikia asilimia 70 na ifikapo Agosti, mwaka huu mabomba yangetoa maji lakini bado wananchi wanaendelea kuteseka,” alisema.
Mnyika alisema serikali ya awamu ya tano ikishindwa kutoa ufumbuzi wa hoja hizo mbili, ataziwakilisha bungeni katika kikao cha Bunge kinachotarajia kufanyika Januari mwakani.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment