Akaunti za shirikisho hilo zinadaiwa kuzuia na TRA zaidi ya wiki moja sasa, huku taarifa zisizo rasmi zikidai kuwa TFF inadaiwa kodi na TRA kiasi cha Sh. bilioni 1.6.
Kiasi hicho kikubwa cha fedha kinatokana na kodi ya lipa kadri upatavyo (Paye) kwa makocha wa timu ya Taifa (Taifa Stars) kati ya mwaka 2010 na 2014.
Aidha, taarifa hizo zilidai pia kuwa TFF haikulipa VAT TRA kwenye mchezo wa kirafiki wa kimataifa kati ya Taifa Stars na Brazil.
Mmoja wa maofisa wa TFF bila kutaka jina lake kuandikwa gazetini kwa kuwa siyo msemaji, aliithibitishia Nipashe kuwa akaunti za shirikisho hilo zimezuiwa na TRA kwa zaidi ya wiki sasa.
"Ni kweli, akaunti za TFF zimezuia kwa zaidi ya wiki sasa, mambo mengi yaliyopangwa kufanyika yanaweza kukwama ukiwamo mkutano mkuu," alisema mtoa habari huyo.Mkutano mkuu wa kawaida wa TFF ulipangwa kufanyika Tanga kuanzia Desemba 19-20 mwaka huu na huenda usifanyike kabisa kama shirikisho hilo litashindwa kufikia muafaka na TRA.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa bila kufafanua kama akaunti za shirikisho hilo zimezuiwa, ilionyesha wazi kuwa TRA imezibana akaunti zao.
"Kwa kutambua umuhimu wa ulipaji kodi na wajibu wa Mamlaka ya Mapato katika kuhakikisha kodi inakusanywa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Taifa, TFF ipo katika mawasiliano na TRA kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa suala hili ikiwa ni pamoja na kupitia upya mahesabu ili kujua wajibu halisi (net liability) wa TFF na namna ya kulipa au kulipwa kutegemea ulali wa mahesabu," ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Iliongeza: "Hii si mara ya kwanza hili kujitokeza, lilijitokeza Oktoba 2012 na Sh. milioni 157.4 mgawo wa klabu kuchukuliwa na TRA. Kufuatia tukio hilo, yalifanyika mazungumzo kati ya TFF na serikali na kukubaliana fedha hizo kurejeshwa na bado TFF inafuatilia hadi sasa."
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment