dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Monday, January 18, 2016

January Makamba-Waziri wa Nchi, Ofisi ya M/Rais, Muungano na Mazingira

Waziri wa Nchi, Ofisi ya M/Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba
Historia na elimu
January Yusuph Makamba ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano na Mazingira katika Serikali ya Awamu ya Tano. Ameteuliwa kwenye baraza la kwanza la mawaziri la Rais John Magufuli.
January ametimiza miaka 42 mwezi Januari na alizaliwa mwaka 1974 mkoani Singida akiwa mtoto mkubwa wa Yusuph Makamba.
Makamba (Baba) ni mwanasiasa mkongwe ndani ya CCM aliyefikia ngazi ya ukatibu mkuu wa chama hicho tawala, lakini pia aliwahi kuwa mkuu wa mikoa kadhaa kwa vipindi tofauti. Mama mzazi wa January ni Josephine Joseph mwenyeji wa Wilaya ya Missenyi mkoani Kagera na baba yake anatokea Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga.
January alisoma shule nne za msingi kwenye maeneo mbalimbali ya nchi kutokana na wazazi wake kuhamahama kikazi. Baadaye aliendelea na masomo kwenye Shule ya Sekondari ya Handeni mkoani Tanga kabla ya kuhamia Shule ya Sekondari Galanos pia ya Tanga.
Masomo ya elimu ya juu ya sekondari alipata kwenye Shule ya Sekondari ya Forest Hill iliyoko Morogoro.
January alianza masomo ya elimu ya juu kwenye Chuo cha Quincy jijini Massachussetts nchini Marekani ambako alifanya mafunzo ya awali kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha St. John’ University kilichoko mji wa Minnesota. Huko alichukua masomo ya amani (Peace Studies) kama shahada yake ya kwanza.
Alipohitimu alishinda tuzo iliyompa nafasi ya kujiunga na taasisi ya rais mstaafu wa Marekani, Jimmy Carter inayoitwa “Carter Presidential Center” kwenye jimbo la Atlanta pia Marekani.
Wakati akiwa na taasisi hiyo alipata fursa ya kwenda nchini Sierra Leone kusimamia Uchaguzi Mkuu na kusimamia mradi wa ufufuaji wa taasisi zilizosambaratika baada ya vita. Safari ya Sierra Leone ilikuwa ya mafunzo maalum.
Alipomaliza mradi wa Sierra Leone alirejea Marekani na kuendelea na shahada ya pili (M.A) ya sayansi ya uchambuzi na usuluhishi wa migogoro. Shahada hii ya pili aliipata mwaka 2004 kwenye Shule ya Uchambuzi na Usuluhishi wa Migogoro ya Chuo Kikuu cha George Mason kilichopo jimbo la Virginia.

Kutokana na ugumu wa maisha ya Marekani na uwezo usioridhisha wa taasisi zilizokuwa zinamfadhili, January nusura aamue kuachana na masomo yake ya uzamili. Lakini alipata wazo la kuanza kuwaandikia watu mbalimbali ambao alijua wanao uwezo wa kuendelea kumsaidia. Mmojawapo alikuwa Rais wa Serikali ya Awamu ya tatu, Benjamin Mkapa. Mkapa alipopata ombi la January aliamua kumsaidia kwa sharti kuwa atakapohitimu masomo arejee Tanzania kusaidia shughuli za Serikali na kutoa mchango wake.
January ni mume wa Ramona Urasa ambaye walifunga naye ndoa mwaka 2005 na wana watoto wawili.

Uzoefu
Baada ya shahada ya uzamili, Makamba alirejea Tanzania kama alivyoahidiana na Mkapa na kuajiriwa Wizara ya Mambo ya Nje, akiwa ofisa wa daraja la pili. Mwaka 2005, Rais Jakaya Kikwete, akiwa Waziri wa Mambo ya Nje, alipitishwa na CCM kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na hivyo kumuomba January ajiunge na timu yake ya kampeni.
January alikubali na kuwa mmoja wa watu muhimu wa kupanga mikakati na hivyo kusafiri na JK nchi nzima. Baada ya Kikwete kuingia Ikulu, alimteua January kuwa msaidizi wake katika nafasi ya msaidizi binafsi wa Rais katika mambo maalum.
January alitumikia wadhifa huu kutoka mwaka 2005 hadi 2010. Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 Makamba aliacha kazi Ikulu na kuingia kwenye siasa za kitaifa. Akaomba ridhaa ndani ya CCM kugombea ubunge wa Jimbo la Bumbuli, wilayani Lushoto.
Kwenye kura za maoni za chama hicho, January alimshinda mbunge aliyekuwa anatetea nafasi yake kwenye jimbo hilo, William Shelukindo. January alipata kura 14,612 dhidi ya 1,700 za Shelukindo. Baada ya kushinda ndani ya chama chake hakukutana na mpinzani yeyote kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 na hivyo akaingia kwenye rekodi ya wabunge waliopita bila kupingwa.
Katika Bunge la 10 alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini na mwaka 2011, chama chake kilimteua kuwa katibu wa siasa na mahusiano ya kimataifa, akichukua nafasi ya Bernard Membe. Alitumikia wadhifa huo hadi mwaka 2012 alipomuachia Dk Asha Rose-Migiro.
Katika mkutano mkuu wa nane wa CCM, January alichaguliwa kuwa kati ya wajumbe 10 wa Kamati Kuu ya CCM upande wa Tanzania Bara, akipata kura 2,093. Mwaka 2012 aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia na amedumu hapo hadi uongozi wa JK ulipomaliza muda wake mwaka 2015.
Ndani ya jimbo lake alianzisha Mfuko wa Maendeleo wa Bumbuli (Bumbuli Development Corporation – BDC). Mfuko huo ulianzishwa Julai 2012 ukiwa na jukumu la kutafuta mapato ya ziada ya kusaidia miradi mbalimbali kwenye jimbo lake. Huu ni moja ya mifuko ambayo inatoa elimu ya lazima kwa wabunge kufanya mambo kwenye maeneo yao kwa mapana zaidi.
January ni mmoja wa wana-CCM walioanza mipango ya muda mrefu ya kuusaka urais wa Tanzania tangu aingie bungeni. Mwishoni mwa mwaka 2014, January alitoa kitabu maalum cha maswali 40 kilichochapishwa na mwandishi Privatus Karugendo kikionyesha maswali na majibu ya namna atakavyoweza kupambana na changamoto za urais iwapo chama chake kitampa ridhaa na Watanzania kumchagua.
Katika kinyang’anyiro cha mwisho ndani ya CCM, January ndiye kijana pekee aliyeweza kuvuka vizingiti na kuingia kwenye tano bora iliyopaswa kupigiwa kura na Halmashauri Kuu, lakini hakuvuka kuingia tatu bora iliyopelekwa kwenye Mkutano Mkuu baada ya kupata kura 124 na kushikilia nafasi ya nne akimuacha Membe katika nafasi ya tano.
Kukosa nafasi ya kuiwakilisha CCM kulimrudisha January kwenye ubunge wa Bumbuli, ambako aliongoza kwa kupigiwa kura 17,805 dhidi ya kura 2,403 za mshindani wake wa karibu Abdulkadir Mgheni. Kwenye uchaguzi wa Oktoba 25, 2015, January alimshinda mgombea wa Chadema kirahisi baada ya kupata kura 17,805 na kushika nafasi hiyo kwa kipindi cha pili. Ubunge ndiyo umempa January nafasi ya kuteuliwa kwa mara ya kwanza kuwa waziri kamili.

Nguvu
Kwanza, kwa zama za sasa za CCM, January anabakia kuwa mmoja wa wanasiasa wenye nguvu katika kada ya vijana. Alivyopenya hadi kufikia tano bora ya kuwania urais, sikushangaa. Jambo hilo lilizidi kumtofautisha na vijana wengine waliokuwa na malengo sawasawa na ya kwake na lilianza kumjengea imani kuwa anaweza siku moja kufanikiwa kwa kupita njia waliyopita wanasiasa wengine wakubwa kama Kikwete ambao waliingia kwenye orodha ya juu ya ushindani ndani ya CCM mwaka 1995 na miaka 10 baadaye wakaikwaa ofisi ya juu.
Jambo la pili, January ni mwanasiasa wa kisasa na mwenye malengo ya muda mrefu. Watu wengi nilioongea nao wanaona kuwapo kwa kwake kwenye Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira ni mpango wa kumbana au kumnyima pumzi ya kufanya siasa za kitaifa na kushiriki kwenye maamuzi mengi ya mara kwa mara yatakayomjenga.
Hali hiyo ya kufichwa kwenye Muungano na Mazingira, naichukulia kama faida kwake kwani wizara aliyomo ina masuala ambayo wananchi wengi wanaona kama hayawahusu sana na hilo linaweza kumfanya aendelee kuonekana mwema, bora na mkarimu kwa wananchi, tofauti na wenzake wengi ambao wamepewa wizara za kusimamia mambo “mstari wa mbele” yanayoweza kuonyesha rangi zao zote kwa wananchi.
Mwisho, January anaendelea kuwa mmoja wa vijana wenye akili pana ya kupanga mikakati inayolipa ndani ya CCM. Katika kampeni za urais za mwaka 2015, yeye ndiye alionekana kusimamia kila jambo lenye mamlaka na kulitolea maelezo, ufafanuzi au mchanganuo. Kwa mtu aliyefuatilia siasa hizo anaweza kukubaliana nami kwamba kwa sasa January ni mmoja wa wapanga mipango na mikakati wakuu ndani ya CCM. Mchango wakje unahitajika sana.

Udhaifu
Udhaifu mkubwa wa January umeendelea kuwa ufuataji wa nini chama chake kinafanya. Mara kadhaa CCM inaweza kufanya mambo kinyume kabisa na utaratibu, lakini January atayasimamia kwa miguu miwili na ama atakaa kimya kama anaona mambo hayo si salama, yeye si aina ya wanasiasa ambao wasiporidhishwa na jambo wanasimama hadharani na kulizungumzia.
Ni mara chache sana ungemsikia akijitokeza hadharani kukosoa mwenendo wa chama chake. Ni wakati ule tu alipokuwa anagombea urais ndiyo alijitokeza kukionya chama chake juu ya nia yake ya kuwabeba wagombea wenye madoa mengi. Huko nyuma niliwahi kuelezea misimamo yake tata katika masuala ya Katiba mpya, misimamo ambayo ilipingana na makada wengine vijana kama Ridhiwani Kikwete na Mwigulu Nchemba ambao wangelipenda suala la Katiba litatuliwe kwa kuzingatia maslahi mapana ya wananchi kuliko mkakati wa chama tawala.
Udhaifu wa pili wa January ni kutokuwa muwazi sana. Hivi karibuni Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) liliendesha Oparesheni ya kubomoa nyumba zilizojengwa kwenye kingo za Mto Msimbazi na maeneo mengine hatarishi na baadaye kusitisha kazi hiyo. Siku kadhaa baadaye January alitembelea maeneo yaliyobomolewa akakaa na familia hizo na kuzipa pole kwa hali ile.
Ikumbukwe kuwa Nemc iko chini ya Wizara ya Mazingira ambayo anaiongoza. Leo ukienda kuongea na wakazi wengi wa Msimbazi wanatambua kuwa aliyekuwa anavunja nyumba ni William Lukuvi na siyo January. Baadhi ya wakosoaji wa Januarya wanaitaja hali hii kama mbinu yake kujificha ili asihusishwe na matukio ya kikatili yanayofanywa na Serikali au yale ambayo hakubaliana nayo kwa faida zake kisiasa ama kwa mkakati wake wa muda mrefu wa kutafuta kuungwa mkono na wananchi. Wengi wanaona kuwa ni vema kiongozi asimamie masuala ya serikali kwa uwazi na ahusike nayo yeye mwenyewe ama kama hayaungi mkono aseme hadharani ili

Matarajio
Matarajio ya January yako dhahiri. Anajua kwamba anapaswa kutumia vyema miaka yake hii mitano ili kujijenga zaidi kisiasa, ikizingatiwa kwamba ana ndoto kubwa za kuongoza ofisi kubwa ya nchi hii siku moja.
Watendaji wa wizara aliyomo hivi sasa wanatambua umahiri wake kwenye utendaji, upangaji wake wa mikakati na uwezo wake wa kuhamasisha na kushawishi. Wanadhani ni wakati muafaka atumie vipaji hivyo kuwafanya wananchi wengi zaidi washiriki kwenye shughuli za ulinzi na utunzaji wa mazingira kwa kujitolea.

Changamoto
Masuala ya mazingira yamekuwa tishio kubwa kwa uhai wa wananchi. Mabadiliko ya hali ya hewa yanayotokana na kukosekana kwa misitu iliyokatwa kila kona ya nchi ni jambo linalohitaji ufumbuzi. Mabadiliko ya hali ya hewa yanayotokana na kuathirika kwa mazingira yetu kwa namna mbalimbali ndiyo chanzo cha kunyesha mvua zenye madhara makubwa au kutonyesha kabisa, na hivyo ndiyo chanzo cha kutokuwa na kilimo chenye mafanikio au kinachoandamwa na ukame na jua kali.
Matokeo ya kutodhibiti tabia zinazoathiri mazingira ni kuliingiza taifa kwenye hatari kubwa ya kukabiliana na athari za maeneo ambayo hayakutunza mazingira. Wananchi wengi hadi sasa wamejenga nyumba zao au kufanya uendelezaji wa maeneo ambayo mazingira yake hayapaswi kuendelezwa. Wengine wamejenga kwenye maeneo kama juu ya vyanzo vya maji, kingo za mito na maziwa nafukwe za bahari. Wote hawa wanahamishia shughuli za binadamu kwenye maeneo ambayo hayahitaji shughuli hizo na ama yataathirika zikiendelezwa.
January na wenzake wanalo jukumu la kipekee la kuja na mikakati inayotekelezeka itakayosaidia kuwapo na taratibu za kudumu za kutunza mazingira na taratibu za muda mfupi na muda mrefu za kudhibiti hali ya sasa kwa njia za kibinadamu baada ya kuwaelemisha wahusika wanaohatarisha mazingira yetu na kuwaondoa kwa utaratibu unaofaa.
Lakini pia wizara hii inayo changamoto ya kujipanga na kuja na mipango shirikishi itakayoeleweka na kukubalika kwa wananchi kama njia ya kupambana na viashiria na njia zote za uharibifu wa mazingira.
Masuala ya Muungano ni mtambuka mno. Hili ni eneo ambalo husimama kama kivuli tu kwani mara zote tumeshuhudia mambo ya Muungano yakiwa juu ya mtu mmoja mmoja, taasisi za serikali na viongozi wa juu wa Serikali. Muungano na ukuaji wake, na ubora wake na siri zake na kila kitu chake limebaki kuwa fumbo ndani ya wananchi wengi wanajua Tanganyika na Zanzibar ziliungana na kutengeneza Muungano, wananchi wanajua faida za Muungano na wengine wanajua mapungufu yanayopaswa kurekebishwa lakini wenye uamuzi wa mwisho kwenye eneo hili ni CCM.
January, ambaye kitaaluma ni msuluhishi wa migogoro, atakuwa na kazi ya ziada kufanya ili kuondoa malalamiko mengi kwenye Muungano ambayo nimeshasema yako hata juu ya taasisi za urais. Ikumbukwe kuwa wizara ya Muungano ilianzishwa ili kutatua matatizo ya Muungano ili kutouweka kwenye hatari za kukosa msimamizi na kuvunjika, lakini kadri siku ziendavyo ndiyo Muungano unazidi kutikiswa kutoka pande zote, Bara na Zanzibar.
Wizara hii pia inayo changamoto ya wakati wa sasa inayohusu matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana kusitishwa kutangazwa na mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kinyume na sheria. Mgombea urais wa CUF aliyeungwa mkono na Ukawa ametamka bayana kwamba baada ya mazungumzo yake na viongozi wa juu wa CCM imefikia wakati anaona mgogoro huo unaweza kumalizwa na Rais wa Muungano.
Ili JPM auingilie mgogoro huu na kuutatua, huenda atahitaji taarifa za kina kutoka kwa wizara inayoshughulikia Muungano. Hapa nina maana kwamba wizara ya January inayo kazi ya kufanya juu ya Zanzibar; inayo changamoto za kumbunia Rais Magufuli mkakati ambao anaweza kuutumia kuyaweka chini makundi yanayopingana ili kuona kama panaweza kuwa na hatua za kuchukua zenye mashiko kwa Taifa na kwa kutenda haki.

Hitimisho
Kwa namna January anavyoendesha mambo yake, inaweza kukusumbua sana ukimfanyia tathmini. Anajua kuwa anapaswa kuwa waziri, lakini anajua anapaswa kujijenga kuelekea 2025. Kwa wale ambao wanaziangalia siasa kwa jicho la “makengeza”, lazima wajifunze upya na kujiridhisha nini ni mipango ya January.
Kwa kuangalia miaka 10 ijayo, namuona January kama mwanasiasa mwenye nguvu zilizopitiliza ndani ya CCM. Ni kama ilivyokuwa kwa Kikwete. Lakini January akumbuke kuwa zama za Kikwete si za sasa na kwamba hata watu “aggressive” bado huweza kuzifikia ndoto za kuongoza ofisi za juu na tayari ana mfano wa Magufuli.
January akikosea kujiweka sawasawa kwenye nafasi ya sasa kwa kufanya kazi chini ya kiwango, inaweza kumuweka nje ya ndoto zake kuu.
Namtakia kila la heri.
*Uchambuzi huu unatokana na utafiti na maoni binafsi ya mwandishi).

Kuhusu mchambuzi
Julius Mtatiro ni Mchambuzi wa Masuala ya Kisiasa na Kijamii, ni mmoja kati ya vijana wenye uzoefu mkubwa na siasa za Tanzania. Ana Cheti cha Juu cha Sarufi (“Cert of Ling”), Shahada ya Sanaa “B.A” katika Elimu (Lugha, Siasa na Utawala), Shahada ya Umahiri ya Usimamizi wa Umma (MPA) na Shahada ya sheria (L LB) – Simu: +255787536759, Tovuti: www.juliusmtatiro.com, Email; juliusmtatiro@yahoo.com).

No comments :

Post a Comment