dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Tuesday, January 19, 2016

Lowassa awapa mtihani mameya wa Ukawa Dar.

  Adai atakayechemsha kutimuliwa, Wainue mapato maradufu, Waling�arishe jiji lao kwa usafi, Watafute dawa kero ya usafiri, Utendaji wao uwaumbue CCM.

Aliyekuwa mgombea urais wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa.
Aliyekuwa mgombea urais wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa, amewapa mambo matatu mameya wa Manispaa ya Ilala na Kinondoni wanayotakiwa kuyafanyia kazi kuidhihirishia dunia kuwa upinzani unaweza kuongoza na kufanya vizuri zaidi.
 
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana baada ya kukutana na Mameya na Manaibu Meya wa Manispaa hizo ofisini kwake, Lowassa alisema kila watakachokifanya ni lazima kiwe cha kuleta matokeo chanya kwa wananchi wa kawaida.
 
Lowassa ambaye aliwataka Mameya hao kueleza mikakati yao kabla ya kuwapa wasio wake, alitaja mambo hayo muhimu ya kuzingatia katika utekelezaji kuwa ni:
 
Mapato:
Alisema Manispaa ya Kinondoni ni tajiri, lakini imeshindwa kukusanya mapato yanayotakiwa na yanayokusanywa yanapotea ovyo na kushindwa kuonekana katika miradi inayotumiwa na Watanzania wa kawaida.“Ni lazima muonyeshe Tanzania na dunia kuwa mnaweza kufanya zaidi ya CCM. Huu ndiyo wakati wa kuonyesha hilo kwa vitendo, tunataka makusanyo yaonekane kwenye maisha ya kawaida ya wananchi na siyo kitarakimu,” alisisitiza.
 
Alisema ili kutimiza hayo, ni lazima waondokane na sheria kandamizi ya masuala ya mhimili wa mkuu wa wilaya na mkoa ambayo itakuwa kikwazo katika utekelezaji wa majukumu yao, lakini viongozi hao watatumia sheria kuwakwamisha.
 
Lowassa ambaye amewahi kuwa Waziri Mkuu, alitaja sheria nyingine ni inayowaruhusu Manispaa kukopa nenki kwa ajili ya miradi ya maendeleo inayonufaisha wananchi.
 
“Mkiweza kuondokana na sheria hiyo na kuwa na kibali cha kukopa benki, hakikisheni fedha zinakwenda kwenye miradi inayonufaisha wananchi wa kawaida moja kwa moja,” alisisitiza na kuongeza:
 
“Ninachotaka kutoka kwenu ni uthubutu wa kufanya mambo, fanyeni yanayoonekana katika maisha ya wananchi wa kawaida, onyesheni kuwa mnaweza kufanya mambo zaidi ya CCM.”
 
Usafi:
Lowassa alisema Jiji la Dar es Salaam linaongoza kwa uchafu, jambo ambalo ni aibu kubwa katika ulimwengu wa sasa.
 
“Jiji ni chafu sana, unapotembea katika mitaa mbalimbali ni aibu sana kwa dunia kama hadi leo watu wanaugua kipindupindu,” alisema Lowassa ambaye pia aliwahi kuwa waziri katika wizara tatu tofauti.
 
Usafiri:
Alisema wananchi wanapata shida ya usafiri wa umma na ni jambo la kawaida kuwakuta kwenye vituo vya daladala na kwenye foleni muda ambao wangepaswa kuwa ofisini wakizalisha.
 
“Muda ni mali, ukipiga hesabu ya muda unaopotea barabarani kila siku kutokana na foleni, kiuchumi ni fedha nyingi sana inapotea. Ni lazima hili mlishughulikie lifike mwisho,” alisema na kuongeza:
 
“Duniani kote watu wanafanya kazi usiku, tangu nikiwa serikalini niliwahi kusema kazi za ujenzi zifanyike hadi usiku, lakini nchi hii usiku binadamu analala na mashine nazo zinalala.” 
 
ATAKAYESHINDWA KUTIMULIWA
Aidha, Lowassa alipoulizwa juu ya hatua zitakazochukuliwa kwa kiongozi atakayeshindwa kufikia viwango vya uwajibikaji unaowekwa na Chadema, alisema makubaliano ndani ya chama ni kwa watakaoshindwa kufikia viwango ndani ya mwaka mmoja watavuliwa nyadhifa hizo.
 
Hata hivyo, jitihada za kumpata Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, kuzungumzia maamuzi hayo ya chama simu yake haikupatikana na hata alivyotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi haukufika.
 
MAMEYA WAAHIDI MAKUBWA
Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Boniface Jacob na Ilala, Charles Kuyeko, walimshukuru Lowassa kwa kuwapa moyo na kuwaweka kambini ambako kumewezesha Ukawa kuwa kitu kimoja kwa Chadema kuwa na Meya na Cuf Naibu Meya.
 
Jacob alisema Kinondoni watafanya kazi kwa kauli mbiu ya Mabadiliko na kazi, huku kukiwa na utatu mtakatifu wa waanchi, watumishi na wataalam.
 
“Thamani ya fedha katika miradi mingi haipo, mfano mkubwa barabara nyingi zinajengwa chini ya kiwango na makandarasi husika licha ya kuboronga bado wanapewa zabuni za ujenzi. Mfano, ni barabara ya Afrika Sana na  Kijitonyama ambayo mkandarasi ameshindwa kumaliza na sasa kapewa kipande cha kuelekea Wanyama Hotel,” alibainisha.
 
Alisema kazi kubwa watakayoifanya ni kukataa kufanya kazi na wakandarasi wa aina hiyo ikiwa ni pamoja na kampuni ya ukusanyaji mapato ya ndani ya halmashauri ambayo hujimegea faida ya asilimia 20 kwa kila fedha wanayokusanya na hakuna uwazi katika mfumo husika.
 
“Nataka kusikia kauli ya serikali kuruhusu bomoabomoa kuendelea ili nami nikabomoe maeneo ya wazi 78 ambayo vigogo wamejimilikisha na kujenga humo,” alisisitiza.
 
Aidha, alibainisha kuwa Jiji halina dampo la taka jambo linaloongeza gharama za uzoaji taka kuwa juu na kampuni za kutoa huduma hiyo kukataa kutokana na kukosa faida.
 
“Taka zinazozalishwa kwa siku ni tani 17,000 zinazozolewa ni tani 4,000 huku tani 13,000 zikiendelea kuwapo mtaani. Tumeongea na Baraza la Usimamizi wa Mazigira (Nemc), kufanya uchunguzi katika eneo la Mabwepande kama panafaa kuanzisha dampo,” alisema.
 
Meya wa Ilala, Kuyeko alisema kazi watakayofanya itaonekana kwa wananchi a ifikapo mwaka 2020 CCM itashindwa kufurukuta Dar es Salaam kwa kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana katika miradi ya maendeleo.
 
LOWASSA AONYA BOMOABOMOA
Aidha, Lowassa aliitaka serikali kulifanya suala la bomoabomoa kwa kuzingatia ubinadamu kwa kuwa linaivunjia heshima Tanzania kidunia.
 
“Sikutaka kulizungumzia sana, lakini hata kama watu hawa walivunja sheria, ni lazima bomoa bomoa ifanyike kwa kuzingatia ubinadamu. Ni aibu kwamba tunafanya jambo ambalo linakosa sura ya ubinadamu…Mke wangu alinionyesha ujumbe wa mlemavu mmoja kwenye mitandao ya kijamii amejenga nyumba yake miaka mingi na imevunjwa,” alisema.
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment