dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Tuesday, January 19, 2016

Ufisadi kutikisa Bunge

  Ni wa bilioni 300/- ulioibuliwa tangu Oktoba

Rais Dk. John Magufuli.
Wakati Mkutano wa Pili wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Mungano wa Tanzania utaanza Jumanne ijayo mjini Dodoma, kashfa mbalimbali zilizoibuliwa kuanzia Oktoba, mwaka jana na kuligharimu taifa takriban Sh. bilioni 300 zinatarajiwa kutikisa.
 
Hoja zingine kadhaa zikiwamo za mashirika ya umma yasiyo na tija, sheria tata na miswada iliyowekwa viporo, pia zinatarajiwa kutikisa mhimili huo wa dola wenye dhamana kubwa ya kutunga sheria.
 
Baadhi ya wabunge walioingia bungeni kwa mara ya kwanza, ni miongoni mwa watunga sheria wanaotarajiwa kuibua hoja mbalimbali ambazo zitajikita kwenye kashfa hizo na sheria tata zilizopitishwa kwenye Bunge la 10.
 
Uchambuzi wa Nipashe umebaini kwamba, kati ya Oktoba, mwaka jana,  na Januari, mwaka huu, kashfa mbalimbali zimeibuliwa na Mamlaka ya Ununuzi wa Umma (PPRA), zingine kadhaa zilizoibuliwa na viongozi wa serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dk. John Magufuli ambazo kwa ujumla zimeligharimu taifa takriban Sh. bilioni 300.
 
KASHFA TANRODS 
Mapema Oktoba mwaka jana, PPRA ilitoa ripoti yake ya mwaka 2014/15 iliyoonyesha ucheleweshwaji mkubwa wa malipo kwa wakandarasi kwenye miradi ya ujenzi wa barabara nchini, chini ya Wakala wa Barabara (TANROADS) na miradi ya maji kwenye serikali za mitaa, imeisababishia serikali hasara ya mabilioni ya shilingi.Mwenyekiti wa Bodi ya PPRA, Balozi Dk. Matern Lumbanga, aliwaambia waandishi wa habari kwamba, mikataba 301 ya TANROADS yenye thamani ya Sh. trilioni 5.3 ilicheleweshewa malipo hivyo kusababisha malimbikizo ya riba ya Sh. bilioni 124.8 hadi Juni, mwaka jana na kuwapo kwa malipo hewa ya Sh. milioni 377.
 
Aliongeza kuwa walibaini kuwapo kwa taasisi tisa zilizofanya malipo kwa kazi au ununuzi ambao haukufanywa kabisa, huku miradi yenye thamani ya Sh. bilioni 6.4 ikibainika kuhusika na malipo ya aina hiyo pia.
 
Lumbanga aliongeza kuwa pia walibaini kuwapo kwa malipo ya ziada ya Sh. milioni 951.7 yaliyofanywa kwa makandarasi kwa kazi hewa.
UFISADI TRL
Licha ya wabunge kuipania Kampuni ys Reli Tanzania (TRL) kutokana na ufanisi mbovu, matumizi mabaya ya fedha ni jambo lingine litakalofanya linyooshewe vidole.
 
Desemba 7, mwaka jana, Rais Magufuli alitengua uteuzi wa Katibu Mkuu wa iliyokuwa Wizara ya Uchukuzi, Dk. Shaaban Mwinjaka, kutokana na ubadhirifu wa Sh. bilioni 16 ndani ya TRL.
 
Ubadhirifu huo ulibainika kutokana na ziara ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, aliyoifanya TRL Desemba 4, mwaka jana.
 
“Nilifanya ziara TRL, nikaenda kujifunza mwenendo mzima lakini nikiwa na taarifa za matumizi mabaya ya fedha Sh. bilioni 16.5. kati yake Sh. bilioni 13.5 zilitolewa na serikali kwa ajili miradi ya TRL ili iweze kujiendesha.
 
“Pia Sh. bilioni tatu TRL ilipata mkopo kutoka TIB (Benki ya Rasilimali Tanzania) ili kuendesha miradi yake. Fedha zote hizi zilitumika visivyo na uchunguzi bado unaendelea,” alisema Majaliwa.
 
MADUDU YA TPA 
Tangu serikali ya awamu ya tano iingie madarakani, ukwepaji kodi katika Bandari ya Dar es Salaam, ni suala lililotikisa na kufanya vigogo kadhaa wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na wale wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wasimamishwe na wengine kufukuzwa.
 
Kutokana na kukithiri kwa ukwepaji kodi huo, Desemba 29, mwaka jana, TPA iliwakamata watumishi  wake 15  kwa tuhuma za kusaidia kutolewa kwa makontena 11,884 bandari kavu bila kulipiwa tozo ya bandari (wharfage). Hatua hiyo ilisababisha serikali kupata hasara ya Sh. bilioni 47.41.
 
Wafanyakazi hao pia walisaidia kutolewa kwa magari 2,019 kwenye bandari kavu mbalimbali zilizoko Dar es Salaam na kusababisha serikali kupoteza Sh. bilioni 1.07.
 
Sambamba na hiyo, Novemba 27, mwaka jana, Waziri Mkuu Majaliwa alifanya ziara Bandari ya Dar es Salaam na kufichua kuwa makontena 349 yalitolewa bandarini bila kulipiwa ushuru wa forodha wa Sh. bilioni 80.
 
Licha ya kuwa Majaliwa hajabadilisha kiasi hicho cha fedha alichotaja, TRA ambayo ndiyo yenye jukumu la kukusanya fedha hizo, imenukuliwa kwenye baadhi ya vyombo vya habari ikisema ushuru wa makontena hayo ni takribani Sh. bilioni 14.
 
MABILIONI YA UINGEREZA
Baada ya Mahakama ya London, Uingereza kutoa hukumu dhidi ya shauri la hati fungani za Sh. trilioni 1.3 zilizotokana na mkopo uliotolewa na benki ya Standard ya Uingereza kwa serikali ya Tanzania, mzimu wa Escrow uliibuka tena.
 
Kashfa hiyo ilikuwa inaihusisha pia benki ya Stanbic Tanzania, ambayo pia ilihusika kwenye kashfa ya takriban Sh. bilioni 300 ya Akaunti ya Tegeta Escrow.
 
Katika kashfa ya hati fungani, Benki ya Standard ya Uingereza iliupatia Tanzania mkopo wa Sh. trilioni 1.3 kwa riba ya asilimia 1.4 lakini benki ya Stanbic Tanzania ambayo ndiyo iliyotumiwa na serikali ya Tanzania kuomba mkopo huo, ikaongeza asilimia moja ambayo ni dola za Marekani milioni sita (Sh. bilioni 13 ikiwa ni hesabu ya kubadilisha dola moja kwa Sh. 2,180).
 
Stanbic Tanzania iliingiza fedha hizo, kwenye akaunti ya Kitanzania ya  EGMA ambayo pamoja na watu wengine, ilikuwa inamilikiwa na aliyekuwa Kamishina Mkuu wa TRA, Harry Kitillya, na ndani ya siku chache zilitolewa kwa fedha tasilimu kinyume cha sheria. 
 
Licha ya kwamba juzi, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilitangaza kuitoza benki hiyo faini ya Sh. bilioni tatu kutokana na miamala hiyo iliyotia saini kutia shaka, suala hilo bado linatarajiwa kulitikisa bunge kwani waliohusika na kashfa hiyo bado hawajachukuliwa hatua.
 
MAAZIMIO SAKATA LA ESCROW 
Kashfa hiyo ya Stanbic, itakuwa kichocheo cha kufufua maazimio manane ya Bunge ambayo baadhi yake yanalenga kuibana taasisi hiyo ya kifedha hayajafanyiwa kazi.
 
Maazimio yaliyopitishwa na Bunge la 10, Novemba 28, 2014, ni pamoja na lile la kuundwa kwa tume ya kijaji ya uchunguzi kuchunguza tuhuma za utovu wa maadili dhidi majaji waliotajwa kwenye kashfa hiyo.
 
Lingine ni lile lililotaka kuanzishwa taasisi mahsusi itakayoshughulikia kupambana na kudhibiti vitendo vya rushwa kubwa, na lile la kuzitaja Stanbic Bank (Tanzania) Ltd na Benki ya Mkombozi Commercial kuwa ni taasisi zenye shaka ya utakatishaji wa fedha haramu.
 
Azimio lingine lilitaka mitambo ya kufua umeme ya IPTL inunuliwe na kumilikishwa kwa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
 
SHERIA NA MISWADA
Mbali na kashifa hizo, katika mkutano wa bunge ujao, serikali inatarajiwa kuwasilisha miswada mbalimbali.
 
Ili kutimiza ahadi ya Rais Magufuli ya kuanzisha mahakama ya mafisadi, muswada wa sheria unaohusu jambo hilo unaweza kufikishwa bungeni kwa hati ya dharura.
 
Pia muswada juu ya sheria ya ununuzi wa umma, huenda ukapelekwa bungeni kutokana na Rais Magufuli kuonyesha kukerwa na sheria ya sasa alipokuwa  akilifungua Bunge.
 
Pia Muswada wa Sheria ya kupata Habari na ule wa  Sheria ya Vyombo vya Habari wa Mwaka 2015, ambayo ilikwama kupitishwa kwenye Bunge la 10 huenda ikarudishwa bungeni kutokana na hali iliyoibuka hivi karibuni ya kufutwa kwa gazei la Mawio.
 
Mbali na miswada hiyo, baadhi ya sheria ambazo zimezua malalamiko mpaka kwenye jumuiya za kimataifa pamoja na ile ya Mtandao, inaweza pia kurudishwa kwenye chombo hicho cha kutunga sheria.
 
Sheria nyingine ni ile ya mafuta na gesi ambayo baadhi ya wabunge walilalamika kuwa ilipitishwa kwa haraka huku ikiwa na mapungufu mengi.
 
HOTUBA YA RAIS KUWASHA MOTO
Kama ilivyo ada baada ya Bunge kuzinduliwa, mkutano unaofuata Wabunge hupata fursa ya kujadili hotuba ya Rais ambayo huwa dira katika mwelekeo mzima wa serikali katika utekelezaji wa majukumu yake.
 
Hotuba hiyo ya Rais ilisheheni mambo mengi, zikiwamo ahadi za kupitia sheria mbovu, kubana matumizi yasiyo ya lazima, kuunda serikali ndogo na yenye ufanisi pamoja na kupambana na rushwa na ufisadi.
 
Pia alisema atashughulikia kero mbalimbali kama vile utendaji kazi serikalini na katika mashirika ya umma. 
 
Mashirika mbalimbali ya umma, yakiwamo Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), TRL, Tanesco, yanajatwa kuendelea kusikika kwenye chombo hicho cha kutunga sheria kutokana na kasoro mbalimbali katika utoaji wa huduma kwa jamii.
 
Hata Rais Magufuli wakati akihutubia bunge aliitaja ATCL akisema licha ya kuwa na ndege moja, ina zaidi ya wafanyakazi 200. Pia alisema suala la umeme ni moja ya vitu vilivyolalamikiwa na wananchi wakati wa kampeni zake.
 
Mradi wa mabasi yaendayo kasi Dar es Salaam, ni jambo lingine litakalotikisa bunge kutokana na ubabaishaji mwingi ikiwa ni pamoja na utata wa thamani ya mabasi, mkataba wa uendashaji, nauli na mambo mengine.
 
Baadhi ya ahadi alizozitoa kwenye hotuba hiyo zimeshaanza kutekelezwa ikiwamo kuondolewa kwa baadhi ya watendaji wakuu wa mashirika na taasisi za umma ambazo utendaji wao uligubikwa na chembe za ufisadi.
 
Kutokana na kuwapo kwa hali hiyo, Wabunge wanatarajia kuibua mijadala mikali wakati wa kujadili hotuba ya Rais pamoja na miswada mbalimbali itakayowasilishwa.
 
Jambo lingine linaloonyesha kuwapo kwa mjadala mzito ndani ya Bunge hiulo linalosubiriwa kwa hamu na mamilioni ya Watanzania ni uwapo wa wabunge wapya vijana na wasomi kutoka kambi ya upinzani ambao watakuwa na shauku ya kuibuka vinara katika hoja na mijadala.      
 
Tayari Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea, amechawasha ‘indiketa’ kuwa atawasha moto ndani ya Bunge hilo atakapoibua suala la kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow kutokana na maazimio mengi kutokutekelezwa na serikali pamoja na wahusika wengine.    
 
Wabunge wa kambi ya chama tawala (CCM), kwa upande wao, wanatarajiwa kuwa wakali kwa kuwa hawatakubali serikali ya chama chao ambayo imeanza kuwang’oa watendaji wabovu.
 
Kama ilivyokuwa katika Bunge la 10 wakati wa mijadala mbalimbali, ukiwamo wa Escrow, Wabunge bila kujali itikadi zao walitanguliza maslahi ya taifa na kuwashughulikia wahusika wa kashfa hiyo na kuwataka wang’olewe.
 
Kwa mantiki hiyo, mijadala katika mkutano utakaoanza Jumanne ijayo inatarajiwa kuwa mikali na yenye kuvuta hisia kwa Watanzania wengi. ambao wakati wa vikao vya Bunge, wafuatilia kwa karibu. 
 
Pia hali ya kisiasa ya Zanzibar, itakuwa moja ya ajenda ya wabunge wa upinzani kutokana na wao kutounga mkono kurudiwa kwa uchaguzi wa Zanzibar.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment