Na Mackie Mdachi
Nasua au kujinasua ni ‘kutoa au ondoa mtegoni kitu kilichonaswa’. Imekuwa sasa kama kawaida kwa mizozo mizito ya kugombea ushindi, ambao hatimaye unapatikana kwa malalamiko mengi huko Zanzibar.
Mwaka 1995 hadi mwaka 2010 hali kama hii ilivyotokea 2015 imekuwa ikijirudia kwa Chama cha Wananchi (CUF) kuulalamikia na kutoridhia ushindi wa CCM. Hofu imetanda nyakati zote.
Kwa busara zilizotumika kati ya viongozi wa kitaifa wa vyama vya CCM na CUF upande wa Zanzibar; yaani Rais mstaafu Amani Karume na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad, makubaliano mema yalifikiwa kati yao na kuunda Serikai ya Umoja wa Kitaifa (SUK). Nawapa hongera za dhati.
Ni busara na utu wao ndiyo uliofanikisha maridhiano mema.
Najua baadhi ya viongozi ving’ang’anizi wa madaraka hawakuipenda hali hiyo ya kiungozi; ambapo CCM Zanzibar na CUF walichangia ama kugawana baadhi ya madaraka ya uongozi.
Wako waliojenga chuki binafsi kutokana ‘busara na hekima’ iliyofikiwa na Karume. Inaendelezwa kwa mgongo wa wananchi kutofurahia CUF kupewa madaraka ya ungozi.
Ni unafiki.
Ulimwengu wa kisiasa uliipongeza hatua ya maridhiano ya uongozi wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK); kwani ilipunguza jazba, sintofahamu, uadui, chuki na kutoaminiana kulikokuwapo kwa miaka mingi ya uongozi wa CCM kule Zanzibar.
Kwa jambo hilo, Rais mstaafu Karume ameweka rekodi mpya ya ki-uongozi Zanzibar. Nampongeza.
Rekodi iliyojaa utashi wa amani ya kweli. Ni rekodi ya kipekee kabisa iliyoongozwa na busara na hekima.
Huu ni msemo unaotumiwa pindi mtu au kiongozi anapofikia hatua ya kukata tamaa ya kufanya uamuzi sahihi ya tatizo ama jambo fulani.
Ni ishara pia ama ya kuzingatiwa mno na woga au hata kushindwa kufikiri zaidi. Inaweza pia kuwa ndiyo njia pekee aionayo kiongozi fulani ya kuwaridhisha baadhi ya viongozi wenzake au wale waliochangia kumwweka yeye katika nafasi aliyonayo hata ikiwa ni kwa gharama ya wanajamii wengi.
Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salum Jecha hana ‘ubavu’ wa kufanya mwenyewe uamuzi aliofanya wa ‘kufuta’ uchaguzi wa Zanzibar na hata uamuzi wa tangazo la ‘kurudiwa’ uchaguzi huo Machi 20, 2016.
Hana ‘ubavu’ huo wa kuvunja Katiba na Sheria stahiki peke yake na ndiyo maana hakuishirikisha tume yake ipasavyo.
Jecha amefanya aliyoyafanya yote haya kutokana na ‘nguvu’ iliyokuwa nyuma yake, na ndiyo maana CCM Zanzibar na makao makuu hawajamlaumu wala kumkemea; ingawa ripoti ya ‘waangalizi’ wa kimataifa’ kutoka nje ya nchi wamesema uchaguzi ulikuwa wa haki, salama na amani’. Tatizo limetokea wapi? Na ni lipi kwa ushahidi upi? Kwao, liwalo na liwe.
Rais Dk Shein jinasue
Ni dhahiri mkwamo wa Zanzibar kiungozi na matokeo ya ‘liwalo na liwe’ ni dhahiri kuwa Dk Shein umejinasisha kwenye ‘mtego’ wa waliokuwamo na wasiokuwamo kwa gharama hasi ya wanajamii na wasimamizi wa kimataifa wa uchaguzi, walioona mambo yote yako sawa.
Wananchi na nchi za nje zaidi ya kumi zinaamini kuwa uamuzi uliofikiwa na kufuta uchaguzi siyo sawa na kushauri busara ifikiwe ili kuepusha madhara mabaya ya fujo. Je, wote hao hawaioni haki stahiki zaidi ya waionavyo CCM? Na ikiwa hakukuwa na vurugu kuna haja gani ya kutumia nguvu za ‘dola’ kwa kupeleka au kuongeza vikosi vya Jeshi la Polisi na wanajeshi. Kwa nini vikosi vya KMKM-Zanzibar vitande mitaani.
Nani wanaovunja usalama ama amani iliyokuwapo awali?
Maswali ni mengi ambayo hayapatiwi majibu, hivyo ni bora Rais Shein kutumia ‘busara na hekima’ zaidi kujinasua kwenye zigo na wimbi hili ovu la kutengenezwa lenye kila dalili za hatma mbaya kwa nchi.
Kauli yako ya dhati ya kujinasua na kutoa haki kwa matokeo stahiki; ndiyo njia pekee ya kuendeleza demokrasia ya kweli na amani ya kudumu Zanzibar.
Kete ya mwisho ya turufu ya uamuzi makini wenye kila sifa ya utu na uongozi bora unayo wewe; vinginevyo Rais Shein hutakuwa na utetezi wowote wa kukunusuru wewe na yatakayojiri Zanzibar; hapo ndipo na wewe utakapojiwekea rekodi ya kipekee kwako.
Rekodi mbaya.
Nchi nyingi za iitwayo ‘dunia ya tatu’ hufikia madhara mabaya kutokana ung’ang’anizi wa madaraka na uvunjaji wa Katiba zao na vingozi wakuu kujikuta wameachwa njia panda isiyo na amani hata kwao.
Watu waishio pwani wana msemo usemao: “Uamuzi bora hufanywa ufukweni, jahazi likitweka tanga, yaliyobaki ni majuto mjukuu.”
Nakumbuka kauli nzito yenye ubaguzi na uchochezi aliyoitoa marehemu Asha Bakari kwa kujiapiza bungeni mwaka 2015 kuwa ‘uongozi wa Zanzibar hautatolewa kwa makaratasi’, je Dk Shein ndiyo haya yatokeayo sasa? Rais Shein ujinasue mtegoni kwa kukubali matokeo halali ya uchaguzi; badala ya kulazimisha uchaguzi kurudiwa ili uendelee kukuweka wewe madarakani. Tafakari.
maoni@mwananchi.co.tz
No comments :
Post a Comment