Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Sunday, February 14, 2016

MTAZAMO WANGU : Ni kweli tumekosa wa kulikwamua Taifa?

Na Musa Juma
Taifa la Tanzania kwa sasa lipo katika mkwamo wa kisiasa wa Zanzibar na mkwamo wa uchaguzi wa meya wa jiji la Dar es Salaam.
Tangu kumalizika Uchaguzi Mkuu, Oktoba 25, mwaka jana sintofahamu imetawala kuhusu mustakabari wa Zanzibar na sasa uchaguzi wa meya wa jiji la Dar es Salaam.
Kwa kiasi kikubwa siasa zetu ndiyo zimetufikisha hapa, kwani katika mazingira ya sasa upofu umetawala na kuwagawa viongozi na wasomi.
Hakuna tena ambaye anaweza kuongea ukweli na kueleweka, wale viongozi wetu wastaafu ambao tulipaswa kusikiliza na kuheshimu maoni yao nao wamegawanyika.
Kwa taifa kama la Tanzania lenye wasomi lukuki wa kada mbalimbali, sambamba na uwepo wa viongozi wakuu wastaafu wenye ujuzi na uzoefu mkubwa wa siasa, Taifa kuingia katika mkwamo huu ni aibu.
Nasema ni aibu kwa sababu, viongozi ,wasomi wetu wa kada mbalimbali, wanajua ukweli wa yanayotokea sasa, Zanzibar na katika sintofahamu ya Meya wa jiji la Dar es Saalam.
Yupo wapi mtu ambaye, atasimama na kusema hadharani, nani mchawi katika sintofahamu hii na kuungwa mkono na wote, jibu inaonekana hayupo na kama yupo hofu inamwandama.
Wapo wachache ‘waliojilipua’ na kutoa maoni kuhusianana hali ya Zanzibar, Waziri Mkuu mtaafu, Jaji Joseph Warioba, wasomi wa sheria, akiwapo mtoto wa Rais mstaafu wa Zanzibar, Fatuma Karume.
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa na Waziri wa mambo ya nje wa zamani, Benard Membe kwa suala la Zanzibar wametoa maoni yao, lakini hakuna mwanga.
Ushauri wa wakubwa hawa, umewekwa kapuni, wanaharakati, wanahabari na wanasiasa kadhaa wametoa maoni yao kuhusu hali ya Zanzibar na uchaguzi wa jiji la Dar es Salaam lakini inaonekana hakuna anayezingatia.
Katika kumaliza sintofahamu, wengine wakaenda mbali zaidi na kumtaka, Rais John Magufuli aingilie kati kama Amiri Jeshi mkuu ili kumaliza mgogoro wa Zanzibar, lakini taasisi nyingine zikaibuka na kusema hana mamlaka hayo Kikatiba.
Cha ajabu anayeombwa ni kiongozi mwingine wa juu, lakini wanaojibu ni wengine hili ni jambo la ajabu na wengi wanahoji jeuri hiyo wanaipata wapi.
Sasa kinachoendelea ni vurugu, tunashuhudia hali ya Zanzibar kundi la watu wasiojulikana wakiitwa mazombi wanafanya uhalifu kila kukicha, maskani za vyama zinachomwa moto, nyumba na maeneo ya wafuasi wa vyama vya CCM na CUF zinaharibiwa.
Lakini bado inaelezwa hali ya Zanzibar ni shwari na taratibu za marejeo ya uchaguzi zinaendelea Machi 20, licha ya chama kikuu cha upinzani Zanzibar(CUF) kueleza wazi hawatashiriki uchaguzi huo.
CUF wanaungwa mkono na vyama vingine vidogo tisa na baadhi wa wajumbe wa tume ya uchaguzi Zanzibar(ZEC) kuwa tangazo la marejeo ya uchaguzi ni batili na wanataka washindi wa oktoba 25 watangazwe.
Katika jiji la Dar es Salaam, tulishuhudia uchaguzi wa Mameya wa Ilala na Kinondoni ukifanyika baada ya tafrani kubwa na washindi kupatikana lakini sasa kuna taarifa za kufutwa uchaguzi huo.
Awali tulishuhudia bila aibu vyama vikikopa wapiga kura kutoka Zanzibar na kuelezwa ni madiwani wapya katika halmashauri za jiji la Dar es Salaam, lakini baada ya msuguano mkubwa uchaguzi ukafanyika.
Kama vile hakuna viongozi wakuu wa vyama wanaoona aibu hii, Sarakasi za Umeya zinaendelea na ni wazi zinakwamisha maendeleo ya wananchi wa jiji la Dar es Salaam ambao wao walikamisha kazi ya kuchagua wanaowataka kuwaongoza.
Sintofahamu katika mambo haya mawili ni aibu wa wasomi na ni aibu kwa viongozi, kwani kuna mambo ambayo hayahitaji hata elimu ya msingi kubaini ukweli lakini upofu umetuvamia na sasa kuwa wanasiasa .
Kibaya zaidi hata baadhi ya viongozi wa dini, wamejikuta wakijiingiza katika sintofahamu kwa kujua ama kutojua, kwani badala ya kutoa kauli za maridhiano wao wanatoa kauli za kuegemea upande mmoja na hapa ndipo najiuliza ni nani atatunasua katika mkwamo huu.
Hivi ni kweli hayati baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ameondoka na kuliacha taifa lisilo la watu wa kusimama na kusema ukweli, jambo hili hapana na hili ndio na wengine wote kufuata.
Binafsi naamini bado taifa hili lina hazina kubwa ya viongozi na wasomi ambao wakikubali kuwa huru wanaweza kutukwamua katika mkwamo huu.
Mussa Juma ni mwandishi gazeti la Mwananchi mkoa wa Arusha.0754296503.     

No comments :

Post a Comment