Dar es Salaam. Rais mstaafu, Benjamin Mkapa amezitaka sekta binafsi kuwa karibu na Serikali, ili kuimarisha sekta ya afya nchini.
Mkapa aliyasema hayo juzi katika harambee ya kuchangia Taasisi ya Benjamin Mkapa, ambayo ilifanikiwa kupata Sh1.17 bilioni zitakazotumika kuimarisha sekta ya afya kwa wenye mahitaji maalumu.
“Naamini sekta binafsi zina mchango mkubwa kwenye uchumi endelevu wa nchi yetu. Hivyo, nashauri kuwapo ushirikiano wa karibu na Serikali,” alisema Mkapa.
Pia, alipongeza Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais mstaafu, Jakaya Kikwete kwa kuisaidia taasisi hiyo kufikia malengo yake na kwamba, anaamini Serikali itaimarisha zaidi uhusiano huo.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo, Mfanyabiashara maarufu na Rais wa Kampuni za MeTL Group, Mohammed Dewji alisema taasisi hiyo imetoa mchango mkubwa kuboresha huduma katika sekta ya afya, hivyo inahitaji kusaidiwa.
Dewji alisema uwapo wa mafanikio kwenye jamii, lazima rasilimali watu, fedha na moyo wa kujitolea uwapo.
“Sekta binafsi zina mchango mkubwa wa kusaidia taasisi kama hizi katika kupunguza changamoto zinazoikabili jamii, kwani wafanyabiashara hawawezi kufanya biashara zao kwenye jamii yenye maradhi na uchumi duni,” alisema Dewji.
Katika hafla hiyo, Dewji alichangia zaidi ya Sh200 milioni, huku akiahidi kuendelea kushirikiana ili kufikia malengo yake.
Awali, Mtendaji Mkuu wa taasisi hiyo, Dk Ellen Mkondya-Senkoro alisema tangu mwaka 2012 walianzisha utaratibu wa kutafuta rasilimali za kujiendesha nchini kwa kushirikisha kampuni, mashirika na taasisi za umma.
Dk Senkoro alisema lengo ni kuchangia miradi mbalimbali ambayo imekuwa inafadhiliwa na wahisani wa kimataifa, hali itakayojenga kujitegemea. Taasisi hiyo ilianzishwa mwaka 2006. Miongoni mwa kazi ambazo imezifanya ni kufadhili wanafunzi 890 kutoka halmashauri 137 nchini, kujiunga na vyuo vikuu 93 vya afya kwa mwaka wa masomo ulioanza 2014 hadi 2016.
No comments :
Post a Comment