Ziara ya Mhe. Salva Kiir, Rais wa Jamhuri ya Sudan Kusini Tarehe 15 Aprili 2016
Mhe. Salva Kiir Mayardit, Rais wa Jamhuri ya Sudan Kusini atafanya ziara ya kikazi ya siku moja nchini Tanzania tarehe 15 Aprili 2016. Rais Kiir anakuja nchini kusaini Mkataba wa kuwezesha Jamhuri ya Sudan Kusini kuwa Mwanachama kamili wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambapo tangazo la kukubaliwa kuwa Mwanachama wa EAC lilitangazwa na Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa EAC uliofanyika jijini Arusha mwezi Machi 2016.
Rais Kiir atawasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere saa 3:00 asubuhi na baadaye ataelekea Ikulu na kupokelewa na Mwenyeji wake, Mhe. Rais John Pombe Joseph Magufuli. Baada ya hapo, Viongozi hao watashiriki hafla ya uwekaji saini ya Mkataba huo iliyopangwa kuanza saa 5:00 asubuhi na kisha watapata fursa ya kutoa hotuba na kusainiCommunique.
Rais wa Sudan Kusini atashiriki hafla ya chakula cha mchana kilichoandaliwa kwa heshima yake na Mwenyeji wake kabla ya kuondoka nchini baada ya hafla hiyo.
Sudan Kusini ni nchi ya sita kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki, ambapo inaongeza fursa nyingi za kiuchumi ambazo zinaweza kuzifaidisha Nchi Wanachama ikiwemo Tanzania, endapo mipango madhubuti itawekwa kuzichangamkia. Fursa hizo ni pamoja na za kibiashara kwa kuwa bidhaa nyingi zinazotumika Sudan Kusini zinaagizwa kutoka Nje ya nchi. Hivyo, jamii ya wafanyabiashara wa Tanzania wanahimizwa kuchangamkia fursa zinazopatikana nchini humo na ndani ya Jumuiya kwa ujumla.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa,
Dar es Salaam, 14 Aprili, 2016
No comments :
Post a Comment