Dar es Salaam. Wanasheria wamekosoa utaratibu unaotumiwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuwatangaza watu anaowatuhumu kuhusika na uuzaji, utumiaji wa dawa za kulevya au anaodhani wana taarifa muhimu zinazoweza kusaidia Jeshi la Polisi kuwakamata.
Tangu mapema wiki hii, Makonda amekuwa akitangaza majina ya watu hao, wakiwemo wanasiasa, wafanyabiashara wakubwa na wadogo na wasanii, akiwataka wakutane naye Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam kwa mahojiano.
Pamoja na kujitetea kuwa ana mamlaka hayo na kwamba asiye na hatia atakuwa amesafishwa baada ya mahojiano na polisi, wanasheria wanaona mteule huyo wa Rais anakiuka taratibu.
“Kinachofanyika sasa kwa kuwataja hadharani watuhumiwa wa dawa za kulevya, kinafanyika kisiasa ndiyo maana hakifuati sheria inayowaruhusu watu maalumu kuita na siyo mkuu wa mkoa,” alisema Dk Onesmo Kyauke, mhadhiri mwandamizi wa sheria wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Alisema polisi, hakimu, mtu wa kawaida wanaweza kumkamata mtuhumiwa bila kuwa na hati ya kukamata iwapo mtuhumiwa amefanya kosa mbele yao.
“Kuna (mkuu wa upelelezi wa wilaya) DCI, (wa mkoa) RCO, kikosi maalumu cha dawa za kulevya, hao ndiyo wana wajibu wa kufanya hivyo kwa sababu ni wataalamu na wamebobea katika kupeleleza, kuagiza watuhumiwa wajisalimishe na hata kukamata,” alisema Dk Kyauke.
Alisema pamoja na ukweli kwamba mkuu wa mkoa ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama, kisheria hatambuliki na suala hilo linasababisha ukakasi, kitu ambacho kinaweza kufanya hata walioitwa kukakataa wito kwa kuwa hakuna sheria inayowabana.
“Kwa jinsi hii shughuli inavyoendeshwa bila kufuata sheria wala kujali madhara ya kisheria yatakayotokea ikiwa ni pamoja na kufunguliwa kesi, inaharibu nia njema ya kukomesha maharamia wa dawa za kulevya,” alisema Dk Kyauke.
“Badala yake (kazi hii) inakuwa kichekesho. Ukitazama, kuna watu wameitwa jina moja moja, wasipokuja hawatalaumiwa kwa sababu wenye majina hayo wapo wengi kila mmoja akikana, hakuna atakayekuwa na jibu.
“Ikiendeshwa kwa kufuata sheria na taratibu ni jambo jema ambalo lilikuwa linasubiriwa na Watanzania wengi tena wenye mapenzi mema na nchi na mustakabali wa vijana.”
Maoni kama hayo alikuwa nayo mwanasheria wa jijini Dar es Salaam, Faraja Mangula ambaye alisema kisheria mamlaka ya kukamata au kuita mtu kituoni ni ya Jeshi la Polisi na watendaji wa vyombo vingine kulingana na kosa, lakini kuna taratibu zake.
Mangula alizitaja baadhi ya hatua zinazotakiwa kufuatwa na polisi ili mtu akamatwe kuwa ni pamoja na kumchunguza na kujiridhisha kuwa mtuhumiwa amefanya au amehusika na kosa analotuhumiwa.
Aliitaja hatua ya pili ni kumkamata mtuhumiwa huyo baada ya kujiridhisha na anayeruhusiwa kufanya hivyo ni polisi. Alisema ya tatu ni kupeleka faili lake Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kama upelelezi umekamilika ili lipelekwe mahakamani. Alisema katika sheria hakuna mahali popote panapomtaja mkuu wa mkoa wala mtu mwingine yeyote katika kuwaita watu kwa ajili ya mahojiano zaidi ya Jeshi la Polisi, hivyo mkuu wa mkoa anapofanya hivyo anajishushia hadhi kwa sababu yeye yupo juu na anachotakiwa kufanya ni kuwaelekeza polisi cha kufanya badala ya kufanya kazi yao.
“Haki inayomtambua kisheria moja kwa moja ni ya kumuweka mtu ndani saa 48 na si kumwita mtuhumiwa polisi kwa ajili ya mahojiano,”alisema Mangula.
Naye wakili wa kujitegemea Bernard Otieno alisema kuwa kuna mahitaji ya kisheria kabla ya kumkamata mtuhumiwa kwa mujibu wa Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai. Alisema mambo hayo ni ukamataji wa kutumia hati (warrant of arrest) na ukamataji bila hati (without warrant of arrest).
Alisema hati hiyo hutolewa na polisi kwa ajili ya kumkamata mtu anayetuhumiwa kwa kosa la jinai baada ya polisi kupata taarifa kutoka kwa mlalamikaji.
Alitaja baadhi ya vitu vinavyotakiwa kuwa ndani ya hati hiyo iwe imetolewa na mkuu wa kituo cha polisi au hakimu, lazima iwe na mhuri wa polisi au mahakama, iwe imesainiwa, iwe na maelezo ya mtuhumiwa kama jina kamili, kabila, dini na ieleze mtuhumiwa akikamatwa anafikishwa kwenye vyombo vya kisheria.
“Watu wa kawaida na hakimu wana haki ya kumkamata mtuhumiwa bila kuwa na hati hiyo iwapo wamemuona akitenda kosa hilo mbele yao, vinginevyo anayeruhusiwa kufanya hivyo ni polisi na kwa kufuata utaratibu maalumu,”alisema Itieno.
Akizungumzia hatua hiyo ya kukomesha watumiaji na wauzaji wa dawa za kulevya, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Ernest Mangu alisema vita hiyo haipo Dar es Salaam peke yake bali nchi nzima.
Alisema makamanda wa mikoa wa polisi wanatambua suala hilo na tayari wameanza kulitekeleza.
Akizungumzia kitendo cha watuhumiwa kutajwa hadharani, mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo Bisimba alisema ili mtu asiharibiwe jina lake kwa kosa ambalo hajatenda, angalau kuwe na ushahidi unaomuhusisha na tuhuma hizo. Alisema kuwataja bila kuwa na ushahidi wa kujiridhisha walau kidogo, baadaye ikathibitika hawakuwa na hatia wala ushahidi kuonyesha kama wanahusika, taswira yake na utu wake katika jamii utakuwa umeondoka.
“Kwa mfano inawezekana wafanyabiashara, viongozi wa siasa na wananchi wa kawaida, walikuwa wanaheshimika na jamii zao, wanatajwa hadharani na inabainika hawakuwa na kosa, zilikuwa tuhuma tu, nani atawasafisha? Ina maana itakuwa ndiyo basi utu wao umeingia dosari, ”alisema Dk Bisimba.
No comments :
Post a Comment