dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Friday, August 9, 2019

“Ujutar” wa kisiasa na kuporomoka kwa demokrasia!


BARAZANI

“Ujutar” wa kisiasa na kuporomoka kwa demokrasia

Na Ahmed Rajab
SITOSHANGAA ukinambia hujui “ujutar” ni nini au “jutar” ni nani?

Niliwauliza watu kadhaa wa sehemu mbalimbali za Uswahilini na wapo pia walionambia hawajawahi kuzisikia kalima hizo mbili.

Nimechungulia kwenye makamusi mawili matatu ya Kiswahili humo namo sikuyaona.

Hata hivyo, tuko wengi wa mjini Unguja tulioyasikia na tunaoyatumia maneno hayo mawili. Mimi nayakumbuka tangu utotoni mwangu. Nilikulia na kucheza pamoja na watoto wenzangu waliokuwa pia wakizungumza lugha zitokazo Bara Hindi, hasa Kigujarati.

Niliweza kuokota maneno ya Kigujarati na kutunga sentensi chache kwa lugha hiyo, sentensi ambazo hadi leo hazijanitoka. Maneno mengine tuliyageuza na kuyafanya ya Kiswahili.

Kwa sababu hiyo, ilinipitikia kuwa labda asili ya maneno hayo ya “jutar” na “ujutar” ni Uhindini kama yalivyo maneno “ubepari” na “bepari” yalioingia na kustakimu katika msamiati wa Kiswahili.



Niliamua kumwandikia rafiki tuliyesoma pamoja skuli ya sekondari Mzanzibari mwenye asili ya kabila la Wapathani kutoka Afghanistani ambaye hivi karibuni alistaafu akiwa profesa wa isimu ya Kiswahili katika chuo kikuu cha Uppsala, Sweden.

Profesa huyo, Abdulaziz Lodhi, amefanya utafiti mkubwa, na ameandika mengi, kuhusu maneno yaliyoingia katika Kiswahili kutoka lugha mbalimbali za Bara Hindi. Haya ni yale ambayo wataalamu wa lugha wanayaita maneno “yaliyoazimwa”.

Aliponijibu ilionesha kwamba hata yeye hakuwa na uzoefu nalo neno hilo, ingawa naye pia ni mtoto wa mjini Unguja. Alinambia kwamba labda kwa “jutar” nilikusudia “juta” au “njuta” ambayo maana yake ni “viatu vinavyostiri/funika sehemu ya mbele ya uwayo, au uwayo mzima, siyo viatu vya ndara, champal au makubadhi.”

Siku ya nne aliniandikia mstari mmoja tu: “Au ni ‘sutar’? Maana yake seremala.”

Siku mbili baada ya hapo akaniandikia tena yafuatayo: “Kwa Kigujarati, Kihindi na Kipanjabi ‘jutha’ lina maana ya ‘mwongo/waongo’. Tena kwa Kigujarati ‘jutharo’ ni ‘mwongo’ na ‘juthara’ni ‘waongo.’ Ni maneno ya kuaibisha.”

Bila ya shaka, Profesa Lodhi alikuwa amefanya utafiti wake na aliulizauliza. Au pengine alizichakurachakura kumbukumbu zake za Kigujarati. Hatimaye, alifika ndipo.

Mtaalam mwengine aliyebobea katika nyanja mbalimbali za Kiswahili, Dk . Farouk Topan, mwenye uzoefu wa lugha ya Kigujarati amenambia kwamba tunaweza kutafsiri “jutar” kuwa ni “jambazi ambaye mwenendo wake ni wa kilaghai.”

Topan, na Lodhi, wamenipa maana inayokaribiana sana na jinsi, kwa ufahamu wangu, “jutar” alivyo. Huwa sio mwongo tu lakini mwongo mwenye kuupanga uwongo wake kwa mpangilio, mzandiki, bazazi, tapeli, jambazi, laghai mwenye kudanganya watu kwa maslahi yake. “Ujutar” ndio ule usanii wenyewe wa mtu mwenye mambo hayo, ila hizo.

Neno “ujutar” lilinijia mara tu nilipofikiria kuyaandika makala haya kwani siasa za siku hizi kwingi duniani ni siasa za kijutar. Tunaweza kuzielezea siasa za aina hiyo, kwa ufupi, kuwa ni siasa za kihuni. Ni aina ya siasa zenye kuhatarisha demokrasia na uungwana wa nchi zinazohusika.

Hizo ni siasa zisizoheshimu katiba za nchi, zenye kuwaona wapinzani au wakosoaji wa sera za serikali kuwa ni adui wa nchi. Ni siasa zenye kutumia njia halali na zisizo halali kuwabana wapinzani na zenye kutumia vyombo vya dola kuwatisha wananchi kwa jumla.

Kila mara huwa wanatafuta njia mpya au hutunga sheria mpya za kuhalalisha vitimbi vyao.

Ubaya wao ni kwamba huwa wanaichimba demokrasia kwa kuzihujumu taasisi za kidemokrasia. Nyakati nyingine huzitumia taasisi hizohizo za kidemokrasia, kama mahakama, bunge au katiba za nchi, kuichimba demokrasia yenyewe. Wala hawaoni haya kufanya hivyo.

Siasa wanazoziendesha wanasiasa wa aina hiyo ni siasa chafu. Inasikitisha kuziona siasa hizo za kihuni “zikichezwa” katika karne ya 21, takriban miaka 70 ushei tangu ufashisti ushindwe katika bara la Ulaya.

Ungedhani kwamba walimwengu walijifunza vya kutosha kutoka vitimbi vya kina Adolf Hitler na Benito Mussolini, watawala wa kidikteta wa Ujerumani na Italia, vilivyosababisha mamilioni ya watu kuuliwa na kuzuka kwa vita vikuu vya pili vya dunia.

Na jambo la kushangaza ni kuziona siasa za aina hiyo zikiibuka Marekani na katika nchi kadhaa za Ulaya. Zinashamiri pia katika nchi za Kiafrika, za Amerika ya Kusini na za Asia.

Wanasiasa wenye kuziendekeza siasa hizo wanazidi kuchipuka kila uchao duniani na kuzifanya siasa zao zionekane kama ni halali, ni sawa kuziendesha bila ya junaha yoyote.

Moja ya misingi ya siasa kama hizo ni habari za uzushi, zile zenye kuitwa “fake news” na wasemao kimombo. Uzushi una madhara yake. Huwatia watu hofu isiyokuwako. Aghalabu watu hao huwa hawayafikirii mambo bali hubururwa tu na jazba pamoja na uzushi wa wanasiasa wazushi.

Mfano mzuri wa mwanasiasa mzushi ni Rais Donald Trump wa Marekani. Trump anaweza akawa zimwi litaloila demokrasia ya Marekani lakini kusema la haki yeye siye aliyasababisha mmomonyoko wa demokrasia nchini mwake. Mbomoko huo ulianza zamani. Trump amezidi kusukuma mbele tu uvunjaji wake.

Kinga za demokrasia ya Marekani zimekuwa zikiregarega tangu miongo ya 1980 na 1990 na zikazidi kuyumba katika miaka ya 2000.

Mambo yalizidi kuchacha Wamarekani walipomchagua Trump 2016. Walimchagua kiongozi mhemshaji, kiongozi anayewashawishi watu kwa kutumia hisia badala ya fikra zao. Ni rahisi kwa kiongozi kama huyo kuwafitinisha watu, kuwafitinisha raia wenyewe kwa wenyewe juu ya misingi ama ya rangi zao, jadi zao, dini zao au hata juu ya tofauti zao za kisiasa.

Hiyo ndiyo sababu kubwa kwa nini Trump na viongozi wa sampuli yake wanatisha na ni hatari. Ni hatari kwa sababu wanaweza mara moja wakaiua demokrasia. Moja ya changamoto zinazoikabili demokrasia duniani ni namna ya kupambana na viongozi kama kina Trump.

Wasomi wawili wa Marekani, maprofesa katika Chuo Kikuu cha Harvard, Steven Levitsky na Daniel Ziblatt, wamelitafakari sana suala la hatari inayoikabili demokrasia nchini mwao. Wameandika kitabu ambacho si kigumu kukisoma chenye kujaribu kuyajibu maswali matatu: Demokrasia hufa vipi? Nini Wamarekani wanachoweza kufanya kuiokoa demokrasia yao? Mafunzo gani historia inayotufunza?

Levitsky na Ziblatt wamekiita kitabu chao “How Democracies Die: What History Reveals About Our Future” (Tafsiri huru ni “Jinsi Mifumo ya Demokrasia Inavyokufa: Kinachofichuliwa na Historia Kuhusu Mustakbali Wetu”).

Kitabu hicho, kilichochapishwa mwaka jana na shirika la uchapishaji la Penguin, kinapaswa kusomwa na kila mtu mwenye wasiwasi na jinsi demokrasia inavyoyumbayumba duniani.

Wasomi hao wameandika kwamba siku hizi demokrasia huuliwa si kwa mapinduzi ya kijeshi au ufashisti usiojisitiri bali huuliwa na serikali zilizochaguliwa kihalali na wananchi. Ni serikali zenyewe zilizochaguliwa kidemokrasia zenye kuiua demokrasia. Ni watawala waliochaguliwa kwa njia za kidemokrasi wenye kuzikaba na kuziua taasisi za kidemokrasia.

Levitsky na Ziblatt wanaitaja mifano ya Venezuela, Georgia, Hungary, Nicaragua, Peru, Philippines, Poland, Urussi, Sri Lanka, Uturuki na Ukraine. Kote huko, wanasema, demokrasia ilianza kubomoka wakati wa uchaguzi. Watawala wa kimabavu huchaguliwa, huendesha demokrasia ya bandia huku wakiitumbua na kuitoboatoboa demokrasia halisi kwa kuzivunja au kuzidhoofisha taasisi za kidemokrasia.

Taasisi zenyewe hugeuzwa na kuwa silaha za kisiasa zinazotumiwa kwa nguvu na wale wenye kuzihodhi dhidi ya wasio na uwezo wa kuzitamalaki.

Hivyo ndivyo watawala wa mabavu waliochaguliwa kihalali wanavyoichimba demokrasia, kwa kuyafanya mahakama na mashirika mingine huru ya serikali yawe “silaha” dhidi ya wakosoaji wa serikali.

Hivyo ndivyo demokrasia inavyouliwa. Waaandishi hao wanaongeza kusema kwamba juhudi nyingi za serikali za kuichimba demokrasia huwa ni za “halali” kwa vile hupata idhini ya bunge au hukubaliwa na mahakama.

Wakati mwingine watawala huhoji kuwa hizo juhudi zao ni za kuifanya “demokrasia iwe bora — kwa kuyafanya mahakama yawe madhubuti zaidi, kwa kupambana na ufisadi, au kwa kuusafisha mchakato wa uchaguzi.” Hawatambui kuwa kumbe polepole juhudi hizo zinaiua demokrasia.

Magazeti huendelea kuchapishwa katika nchi zenye serikali aina hiyo lakini magazeti yenyewe na hata sekta binafsi za uchumi hunyamazishwa ama kwa kuhongwa au kwa kutishwa. Serikali huwa haiwakubali ila wale wasemao: “hewala bwana”, wale wasiothubutu kuikosoa.

Huo ndio ujutar wa kisiasa. Huigeuza haramu na kuifanya iwe halali. Wamarekani wengi wanaogopa. Wana hofu kuhusu yanayotendeka nchini mwao, taifa lenye kujinata kwamba ni la kidemokrasia na lenye kuilinda demokrasia lakini ambalo sasa linakabiliwa na mtihani mkubwa wa kidemokrasia likiwa linaongozwa na mtu asiyeujali uungwana wa kidemokrasia.

Anakuwa tayari kuivunja miiko ya kidemokrasia kwa maslahi yake binafsi. Ni kiongozi anayejiona kuwa hakuna aliye bora ila yeye na mwenye kuamini, kinyume na ushahidi uliopo, kwamba watu wengi sana nchini mwake wanamuunga mkono.

Waandishi Levitsky na Ziblatt wanaonya kwamba haitoshi kushtuka na kughadhibika. Lazima watu wawe wanyenyekevu na jasiri. Wawe tayari kuzisoma alama za nyakati kutoka nchi nyingine zenya demokrasia iliyobomoka ili waweze kuzilinda haki zao za kidemokrasia.

Ni muhimu kitabu chao kisomwe hata na watawala wa nchi kama za kwetu ili waweze kutambua namna watavyoiua demokrasia endapo hawatokuwa makini wanapotekeleza majukumu yao ya utawala.



Baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com; Twitter: @ahmedrajab

No comments :

Post a Comment