dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Saturday, September 1, 2012


Zoezi la sensa lawatia hofu masheha
Na Khamis Mohammed
BAADHI ya masheha wameonyesha wasiwasi wao juu kusahaulika kwa watu kwenye zoezi la sensa ya watu na makaazi inayoendelea nchini kote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, masheha hao walisema, wakati zoezi hili likiingia siku ya sita, zipo baadhi ya kaya ambazo hazijafikiwa na makarani wa sensa, hali inayowatia hofu huku zoezi hilo likiwa linaelekea kukamilika siku ya Jumamosi.

Sheha wa Pangawe wilaya ya Magharibi Unguja, Abdallah Juma Mtumweni, alisema, kumekuwepo na maeneo ambayo hadi sasa zoezi hilo halijafanyika kutokana na kuwepo kwa makarani wachache kwenye maeneo hayo.


Aliyataja maeneo hayo ni pamoja na Fuoni Mambosasa ambako idadi kubwa ya kaya hazijahesabiwa na kwamba wananchi wanaendelea kutoa ushirikiano na uongozi wa shehiya kuhakikisha wanafikiwa na makarani hao.
Hata hivyo, alisema, pamoja na kasoro hiyo ndogo, zoezi la sensa linaendelea vizuri kwenye shehiya hiyo, ingawa zilikuwepo changamoto nyengine wakati wa kuanza kwa zoezi hilo.

"Yupo karani ambaye aliibiwa kabrasha lake la sensa, lakini huyu muhalifu alitiwa mikononi na jeshi la polisi na taratibu za kisheria zinaendelea", alisema Mtumweni.

Naye sheha wa Tomondo, Mohammed Omar Said,  alisema, wapo baadhi ya watu katika shehiya hiyo wanaoendelea kugomea zoezi hilo sambamba na kubandikwa kwa vipeperushi vyenye kutoa vitisho kwa wananchi wengine juu ya zoezi hilo la kitaifa.

"Ipo nyumba iliyobandikwa tangazo la kutishia makarani, lakini uongozi wa shehiya umeshalifanyia kazi suala hilo".

Alisema, watu wanagomea zoezi hilo wanaendelea kutoa sababu za kidini wakitaka kupata kauli kutoka kwa masheikh wao kabla ya kushiriki zoezi hilo.

Sheha wa Fumba, Issa Hassan Shoka, zoezi linaendelea vizuri  huku baadhi ya watu wakiwagomea makarani wanaofika kwenye kaya zao ikiwa pamoja na kutoa lugha za matusi  kwa makarani hao.

"Tulijaribu kuwaelemisha watu hawa umuhimu wa zoezi la sensa, lakini hatimaye walituelewa na kutoa ushirikiano kwa makarani", alisema Shoka.

Mapema Mkuu wa wilaya ya Magharibi, Hassan Mussa Takrima, aliwataka wananchi kutumia vizuri fursa hiyo huku wakielewa zima kubwa inayowakabili katika kuleta maendeleo ya taifa na wananchi kwa ujumla.

Sensa ya idadi ya watu na makazi ilianza nchini kote usiku wa kuamkia Agosti 26 mwaka huu ambapo Watanzania wote bila kujali itikadi za vyama, dini ama kabila wametakiwa kushiriki kikamilifu zoezi hilo la kitaifa.

Chanzo: Zanzinews

No comments :

Post a Comment