dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Wednesday, April 17, 2013

Tukichezea sheria itatuchezesha shere


Na Salim Said Salim

NAMNA ambavyo mwili wa binadamu umegawika unatoa mafunzo makubwa kwa wale wanaotaka kujifunza na wasiotaka.
Kila sehemu ya mwili au kiungo cha binadamu huwa na kazi yake maalumu. Kazi ya mdomo ni kusema, iwe kwa sauti kubwa, ndogo, upole au ya ukali.
Macho hufanya kazi ya kuona, masikio kusikia kinachozungumzwa kwa sauti kubwa au kunong’onwa, pia huwa inanusa harufu na kutoa pumzi, miguu inatusaidia kwenda na kadhalika.
Hata siku moja sijapata kusikia bega kufanya kazi ya akili au meno kumsaidia mtu kukimbia mbio. Hivyo ndivyo ilivyo kwa maisha ya kila siku ya mwana wa Adam na Hawa.
Hali hii ni kielelezo kizuri tulichopewa na Mola wetu (kwa wale tunaoamini kuwepo kwa Mwenyezi Mungu) juu ya umuhimu wa kazi na hatari za watu kuingiliana katika kazi zao na majukumu waliyonayo, iwe katika familia zao au jamii.
Ni kwa mantiki hii ya mgawanyo wa kazi uliopo katika mwili wa binadamu ndiyo Waswahili wa ukanda wa Pwani wakaja na msemo wa kukataa mtu mmoja kufanya kazi zote unaoeleza…. “Mlalamikaji Msomali, mwendesha mashitaka Msomali na hakimu Msomali.”

Lengo la usemi huu ni kuitahadharisha jamii juu ya hatari ya anayelalamika kuwa ndiye huyo huyo anayefungua mashitaka na hata kuchukua kazi ya hakimu. Hapa unajitokeza umuhimu wa mgawanyo wa kazi katika kutekeleza na kusimamia sheria na katika kutoa haki.
Kwa upande wa Mrima (Bara) upo usemi unaofana na huu unaotoa onyo kwa kesi ya nyani kumpa ndegere kuhukumu.
Ni katika mtazamo huu nilioueleza ndiyo katika dunia ya leo ukasisitizwa umuhimu wa kugawana majukumu ili kuhakikisha demokrasia inastawi na utawala wa haki na sheria unafanya kazi, ikiwa pamoja na mfumo wa mahakama huru.
Polisi nao wakapewa madaraka na mamlaka ya kuwabana wanaotuhumiwa na uhalifu na kufanya uchunguzi juu ya tuhuma zinazowakabili ili kupata ushahidi wa kuwasilishwa mahakamani kwa kutolewa hukumu.
Lakini katika kuonyesha kuwa polisi hawasimamii uendeshaji wa mashitaka ndiyo pakaundwa ile tunayoielewa kama Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP).
Tanzania Bara imekuwa na ofisi hii kwa zaidi ya miaka 40 sasa. Zanzibar ilikawia kuwa na ofisi hii, lakini iliamua kwenda sambamba na ulimwengu wa mfumo haki na sheria miaka 12 iliyopita kwa kuanzisha ofisi ya DPP.
Kwa hili Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) inastahili pongezi, ijapokuwa ilikawia kufanya hivyo. Wazee walitupa faraja kwa kutwambia bora kukawia kufika kuliko kutoifanya safari kabisa (Better late than never).
Kwa bahati mbaya, katika siku za karibuni kumeonekana kuingiliwa kikazi au kuwekewa vizingiti ofisi ya DPP katika utendaji wake wa kazi na kupelekea baadhi ya watu kujiuliza: Tunaelekea wapi?
Wapo watu, tena wengi, walioanza kuwa na wasiwasi mkubwa kwamba tunaonekana kutaka kurudi (au kurudishwa) kule tulikotoka kwa ‘mlalamikaji Msomali, mwendesha mashitaka Msomali na hakimu Msomali.’
Ule ndio wakati tuliokuwa na zile zilizoitwa mahakama za wananchi (people’s courts) ambazo wengi wa mahakimu wake walikuwa hawajui kusoma wala kuandika, watu ambao umri mkubwa ulikuwa umewapunguzia hekima na busara na matokeo yake kusinzia wakati walipokuwa wakisikiliza kesi.
Kichekesho kikubwa zaidi ni kuwa aliyeendesha mashitaka baadaye ndiye aliyekuwa mtetezi wa hao hao aliowatia hatiani, yaani jana alisema wana makosa na siku ya pili anaiambia mahakama kwamba washitakiwa hawana makosa.
Mfano ni ule wa kesi ya uhaini kufuatia kuuawa kwa Rais wa kwanza wa Zanzibar, Abedi Amani Karume mwaka 1972.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali alisema washitakiwa walikuwa na hatia na baadaye akaja kuwatetea na kusema hawana hatia. Huko ndiko ilikotoka Zanzibar.
Miongoni mwa mifano iliyojitokeza karibuni na kuanza kutia shaka kama upo utawala wa haki na sheria Zanzibar ni namna ambavyo jamii imesikia juu ya baadhi ya kesi nyeti zinazoendelea Zanzibar. Miongoni mwao ni ile ya kijana Omar Musa Makame anayetuhumiwa kumuua Padre Evaristus Mushi miezi miwili iliyopita.
Katika kesi hii tulielezwa kuwa Ofisi ya DPP ilikataa kutoa hati ya mashitaka kwa Jeshi la Polisi. Ofisi ya DPP na Polisi zilirushiana mpira juu ya mvutano huu kwa kila upande kukataa kueleza kwanini hati ya mashitaka ilikuwa haikutolewa.
Huu sio utawala bora, wa ukweli na uwazi kwa sababu kilichoonekana hapa ni usiri na wahusika kutojiamini katika utendaji wao wa kazi.
Hili ni suala ambalo umma unaficha watu haki ya kupewa habari zake na kitendo cha kuficha watu kupata habari ni ukiukaji wa haki za binadamu.
Lakini baadaye tukaona mshitakiwa amefunguliwa mashitaka, lakini pia haikuelezwa kama cheti cha kuruhusu kesi hiyo kuanza kilitolewa, na kama ni hivyo kwa misingi gani na ni nini kilichotokea hata ofisi ya DPP ikasalimu amri.
Hapa ipo shaka na tayari zinasikika tetesi nyingi katika jamii juu ya suala hili nyeti, nyingine zikiwa zimeongezwa chumvi na nyengine zimepunguzwa sukari.
Ukimya na uvumi kwa kiasi fulani vinapunguza imani ya wananchi kwa serikali yao, Jeshi la Polisi na ofisi ya DPP.
Wananchi pia wanataka walezwe kwa nini polisi walikaa na mshitakiwa kwa zaidi ya wiki mbili bila ya kumfikisha mahakamani wakati sheria inakataza hilo kufanyika. Au ndiyo tuseme polisi ndio wenye haki ya kuvunja sheria za nchi hii na raia ndio wanaolazimika kuziheshimu?
Ni muhimu katika masuala kama haya kwa kila taasisi kuelewa mipaka ya kazi yake, kuheshimu wajibu na mamlaka ya taasisi nyingine na umma kuelezwa kwa uwazi kila jambo linalowagusa maisha yao na mwelekeo wa nchi yao.
Wale wanaofikiri wanaweza kufanya watakalo, waelewe zama zile zimepita na wasije kusema wanaonewa ikifika siku wakawajibishwa kwa kuvunja sheria zilizotungwa na Baraza la Wawakilishi na kuwekewa sahihi na Rais wa Zanzibar ili zitumike.
Nchi yetu imesaini mikataba ya kuheshimu haki za binadamu, hivyo tunalazimika kuheshimu yale yote yaliyomo katika hiyo mikataba, ikiwa pamoja na mtindo wa kuendesha kesi kwa staili za ‘kumuachia Msomali kumkamata mtuhumiwa, kumfungulia mashitaka na kumhukumu’.
Mahakama nayo inapaswa kusimama kidete kusimamia uhuru wake iliopewa kisheria na wale wote wanaoichezea wachukuliwe hatua za kisheria, lakini sio kwa uonevu bali kwa misingi ya sheria.
Baadhi yetu tunaojifanya kuwa na vifua vipana kutokana na madaraka tuliyonayo au kwa sababu nyingine, lazima tuelewe kuwa mtu huhukumiwa kwa maovu yake na sio mema yake.
Viongozi wa Jeshi la Polisi wanapaswa kuelewa mipaka yao ya kazi na kuheshimu wajibu na mamlaka ya taasisi nyingine. Ipo siku watarudi uraiani na watakapotakiwa maelezo kwa yale ambayo jamii inahisi hayakuwa ya haki ambayo waliyatenda walipokuwa kazini wasilalamike.
Mtu huvuna anachokipanda, kwa hivyo wajitahidi kupanda mbegu nzuri ili mavuno yao hatimaye yawe mazuri.
Viongozi wetu, wakiwemo maafande, wanapaswa kujifunza kwa yale yanayowakuta wengine baada ya kustaaafu.
Hii leo watu wanawalalamikia viongozi wakuu wa nchi kama rais na waziri mkuu na hata kuwafungulia mashitaka. Kama hao wanashitakiwa patakuwa na ugumu gani kuwashitaki waliokuwa wakuu wa Jeshi la Polisi?
Tujifunze kwa tunayoyaona na kuyasikia. Dunia hii ni hadaa na ulimwengu ni shujaa. Tusikubali kudanganywa na wakati tulionao, tuangalie usoni na kumuoma Mungu atusaidie na kutupa hatima njema.
Lakini hatma njema hujengwa na mtu mwenyewe na kinachofanywa na jamii baadaye ni kuitilia mbolea na kupalilia.
Narudia. Tunapaswa kuwa na hadhari na tusijaribu hata wakati mmoja kuzichezea sheria za nchi. Tukizichezea sheria ipo siku hizo sheria tunazozichezea zitatugeukia na kutuchezesha shere.
Wakati huo umri wetu utakuwa mkubwa, wengine tukitumia mkongojo kwenda na kwahivyo kushindwa sio kucheza hiyo shere tu, bali hata kuisikia au kutikisa mikono, miguu au kichwa.
Chanzo – Tanzania Daima

No comments :

Post a Comment