Na Sharif Mbukuzi
TUNAPOJIULIZA swali muhimu la ni wapi imepotea ile elimu yetu nzuri tuliyo tukijivunia kuwanayo Zanzibar, tunapaswa kabla ya yote, kurudi nyuma na kuulizana nani amepindisha viwango?
TUNAPOJIULIZA swali muhimu la ni wapi imepotea ile elimu yetu nzuri tuliyo tukijivunia kuwanayo Zanzibar, tunapaswa kabla ya yote, kurudi nyuma na kuulizana nani amepindisha viwango?
Tunasema pale juu kileleni ilipokuwepo ilijengeka kwa sababu ya kuwepo misingi madhubuti. Ilikuwa elimu ya viwango vilivyojengwa vikajengeka.
Kwamba matunda ya uchumi mkubwa uliokua kwa kutegemea mauzo ya karafuu na viungo vingine mbalimbali ndani ya nchi, yalisambaa kwenye jukumu muhimu la kuitunza na kuiengaenga elimu.
Sasa leo tungali tunalitambua hili? Tungali tunapeleka fedha za kutosha kwenye dhamira ya kuikuza elimu yetu au tumekuwa tukijitia hamnazo na kujifurahisha tunayo elimu nzuri kwa kutaja tu nambari?
Nani kasema sekta ya elimu inapewa kipaumbele katika mgao wa fedha? Na hata kama zinatengwa nyingi, si tunaona sehemu kubwa ya fedha za bajeti zinatumika kwa ajili ya masuala ya utawala zaidi kuliko eneo la kuijengea msingi elimu.
Hapo ndipo tunapojikuta tunadanganya na kujidanganya. Kitu kibaya ni kwamba tunajisahau na kudanganya wananchi, wale waliokubali kutoka jasho kufanya kazi kwa moyo mmoja kwa ajili ya maslaha ya nchi yao.
Tunajitia tu mabingwa wa nambari kama vile tunao mfano wa kuonesha ni wapi au mahali gani nambari hizi – tarakimu – zimetumika kupata kusaidia kuinua elimu. Maendeleo ya elimu si tarakimu ni viwango, ndivyo UNICEF wasemavyo.
Haifai watu wazima wenye akili kudanganyana na kudanganya umma. Elimu yetu imeshuka tena kwa kiwango cha kutisha na kukatisha tamaa. Juu yake, panahitajika marekebisho makubwa ili kuirudisha kule ilikokuwa imefikia.
Tunashuruti la kurudi kwenye sheria yenyewe ya elimu. Irekebishwe ili iende na wakati uliopo. Lakini irekebishwe kwa minajil gani? Hili ni jambo muhimu kulizingatia. Tunataka sheria inayomtambuwa mwalimu kuwa kiongozi kisekta.
Itakuwa ni kazi bure iwapo tutaendelea kuimba mwalimu ni muhimu lakini hatuoneshi jitihada za kweli za kumjenga binafsi na kumjengea mazingira rafiki ili afundishe kimatarajio.
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itenge fungu la kutosha la bajeti kwa ajili ya kujenga maslaha ya walimu; kuinua miundombinu ya elimu; kununua vifaa na vitendea kazi vya walimu.
Tunataka eneo la ukaguzi liimarishwe kwa ngazi inayohusika na uteuzi wa wakaguzi kuteua walimu wenye uwezo wa kuifanya kazi hiyo inavyotakiwa.
Tupandishe madaraja walimu waliopo. Tuwape mafunzo mepya ya ufundishaji wa kisasa. Tujenge maabara na kuzipatia zana zake stahili. Tupunguze idadi ya watoto wanaokaa darasa moja. Ni kupoteza nguvu bure mwalimu kuongoza watoto 100 au 150 kwa darasa. Hii haiwezekani.
Na hapa lazima tukubaliane kuwa hatuwezi kumudu kupata watoto wenye utashi wa kusoma masomo ya sayansi iwapo hatukutilia mkazo kuujenga msingi tangu wakiwa watoto kabisa.
Inabidi kurudi kule ambako mwalimu aliyebobea anakaa na watoto, akishinda nao huku akiwa anawaangalia nani amefanya nini, wakati gani na nani ameshinda vipi. Nazungumzia suala muhimu la utafutaji wa vipaji vya watoto mapema utotoni kwao.
Wenzetu wanawaweka watoto huria katika eneo fulani na kuwapatia kila kitu cha kuchezea. Vitu vingi vya kuchezea unavikuta wanawekwa navyo. Vitu vya kujumlisha, kuhesabu na kutoa. Vinakuwepo na vitu vya kuzidisha. Wanawekewa vitu vya kuchorea kadhalika.
Mwalimu mbobezi anaangalia kila mtoto anapenda kitu kipi, kufanya nini. Akishakipata anakitumiaje? Anatengeneza kitu au anachora kitu. Anafanya nini?
Katika mazingira kama haya kwa mwezi mzima au hata mitatu, mwalimu mlezi wa watoto hawa anakuwa ameshabaini vipaji mbalimbali kutokana na watoto wetu.
Tunataka kuamua mapema kuwajenga kisayansi. Wapende hayo wanayoyapenda kielimu. Watakua hivyo taratibu. Mwisho wa siku tutakuwa na watoto waliojigawa. Huyu anapenda eneo fulani la sayansi na yule anapenda eneo fulani.
Tunatafuta mabingwa wa hesabu wa siku zijazo. Wapo watakuwa wamejipambanua kuwa ni wajuzi wa kuchora na kuchora nini. Wengine watakuwa wamejipambanua kwa maeneo yao. Sawasawa.
Ndiyo watoto wa Kijapani hulelewa. Kwa kuwaweka na vitu mbalimbali na kuwaangalia, unawapa nafasi ya kujiamulia tangu utotoni kwao wanavyotaka kuja kuwa wakifikia wakubwa.
Kwa namna hii inakuwa rahisi kupata watoto wanaojitawanya kwenye maeneo mbalimbali ya fani za sayansi. Tunajitengenezea mabingwa wa miaka 20 ijayo mbele.
Sasa kama katika mipango yote hiyo niliyoieleza hakuna upuuzi wa siasa, vyereje tunaingiza mambo ya siasa katika elimu yetu? Siasa itasaidia nini kuinua elimu kama siyo kuzidi kuitumbukiza shimoni?
Kumbukumbu za matukio, zinaonesha kuwa siasa imechangia sana kuiangamiza nafasi ya Zanzibar kama moja ya nchi zilizokuwa juu kwa kiwango cha elimu Afrika. Upendeleo utatoa mchango gani katika mipango hii?
Nasema katika kuifufua elimu yetu, siasa na upendeleo visipewe nafasi kamwe. Mambo haya sote tunajua vizuri kuwa ni adui wa maendeleo yoyote, popote pale. Tusiyaendekeze.
Kila hatua ya mipango yetu yapasa iandaliwe vizuri, kwa ustadi, na kutekelezwa kwa kuzingatia viwango vilivyowekwa. Ndo tunaenzi viwango hapa. Sasa ni muhimu kwa kila mmoja wetu kuonesha uzalendo wake katika jambo hili.
Hapo tumejenga mazingira ya kumpata mwanafunzi wa kusomeshwa. Tunataka sasa kuona mazingira ya skuli zetu yalivyokaa; je yanatosha kumvutia mtoto kusoma? Bali je, yanatosha kumshawishi mwalimu kubaki darasani kusomesha?
Mwalimu hubaki darasani kusomesha kwa mambo mengi. Lakini, kama tayari tumemtizama mahitaji yake, kama tumeangalia maslahi yake na kuyasuka upya, kama anaviona vifaa na vitendea kazi, na kama anajua skuli yake ina uongozi mzuri, ana sababu gani ya kutosomesha kwa nguvu?
Tumebainisha namna gani tunaweza kupata vipaji vya kitaaluma mapema kupitia kwa watoto wetu. Eneo linalofuata ni mitihani.
Iwapo mazingira ya skuli zetu yatakuwa yanavutia watoto kusoma, hapana shaka yoyote na mwalimu atakosa pa kukimbilia au pa kukwepa wajibu wake wa kuwasomesha watoto.
Kusomesha watoto kunakwenda sambamba na kuwapima kati na kati – kila hatua fulani. Mitihani inapaswa kuangaliwa upya tangu maandalizi yake ya utungaji wa maswali mpaka ulinzi wakati wa kuchapishwa na usafirishaji wake hadi kufikia skuli.
Kwa kuwa walimu watakuwa wamejengwa vizuri, sasa nao watajitambua maana itakuwa wanajua walivyotangulia kutambuliwa na mwajiri wao. Hapa mwajiri amefuta dharau kwao, amefuta kejeli kwao, amefuta uadui kwao, na amefuta ubabe kwao.
Inatupasa kuwachukulia walimu vile walivyo. Kila mwalimu tumpe nafasi ya kusomesha somo analolimudu.
Kusiwe na kitu kulazimishana mzigo wa masomo ambayo tunajua mwalimu hatayamudu. Huko ni kupoteza muda wake, muda wa kazi na raslimali pia.
Ndio kusema inatakiwa kupanga tuna walimu wangapi kulingana na mahitaji. Tunao walimu wa kutosha wa masomo yote? Ni somo gani kuna pengo la mahitaji na idadi waliopo? Kama kweli lipo pengo, linazibwaje? Kwa muda mfupi, wa kati na mrefu.
Sasa tuseme tayari tuna walimu wenye uwezo wa kufundisha; na wenye ujuzi wa kumudu masomo ambayo mwalimu amekubaliana na kiongozi wake kuwa anayamudu, tunatarajia watatulia na kufanya kazi. Hapa tutakuwa na haki ya kusubiri matunda.
Katika mafanikio kama hayo ya kuijenga skuli kumvutia mtoto kusoma na mwalimu kupenda kusomesha, tutapata uhakika wa mitihani kusalimika.
Hatutatarajia kusikia tena mtihani fulani umevuja.
Ukweli, watumishi wa kada nyingine zinazohusishwa katika maandalizi ya mitihani, hawatakuwa tena na haja ya kuvujisha mitihani. Ili wapate nini wakati kila jambo lao la maslaha nao limeangaliwa vizuri?
Tatizo la mitihani kuvuja linasababishwa zaidi na suala la watumishi wa umma kuamua kudharau maadili ya kazi. Pia wale walioteuliwa kusimamia hatua za uandaaji mitihani mpaka kufikia skuli, kutojitambua umuhimu wao.
Bado tusimamie hapo kwamba pale penye mazingira yaliyojengwa vizuri kwa mwalimu na watumishi wengine, hakuna sababu ya mitihani kuvuja. Turudi nyuma kufikiria kule ilikuaje mitihani isivuje wakati ikichapishwa London, bali leo inapochapishwa nyumbani?
Kwa kuwa mazingira yameshajengwa ya kupanga na kuenzi viwango katika maeneo mengine, kilichosalia ni kimoja:
Hatua za haraka na kali zaidi kufuata dhidi ya mtumishi atakayebainika ameiba au kuvujisha mtihani.
Kusiwe na muhali hata kidogo kuchukua hatua za kinidhamu na kisheria kwani wizi na udanganyifu katika mitihani yamekuwa matatizo sugu yaliyochangia elimu yetu kupotea.
Tukisha hapo, tujiulize tunapasishaje watoto? Kweli tumewapima, je wanaotangazwa au kuteuliwa kusonga mbele wamefikia viwango hivyo? Hili ni eneo lenye mgogoro pia.
Katika lile kongamano lililoandaliwa na taasisi ya uchambuzi wa utafiti na sera za masuala ya umma, ZIRPP, mwalimu wa sekondari ya Field el Castro, kisiwani Pemba, alisema wamebaini watoto wengi wanaopasishwa kuingia michepuo, Form I, hawana uwezo huo.
Hili ni jambo la ajabu kabisa. Mtoto anapelekwa vipi mbele wakati hakufuzu mtihani? Huu ni uzembe na kwa kweli ni uhuni pia.
Basi wao Field el Castro wameanzisha mtihani maalum kuwapima upya watoto wanaoteuliwa kujiunga hapo.
Huwa wanaulizwa maswali stahili ya kiwango wanachotarajiwa kuwa wamefikia. Hapo yule anayefuzu tu ndiye wanamruhusu kuanza masomo ya kidato cha kwanza.
Inashangaza kumsikia mwalimu anasema wapo baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakikwepa hatua hiyo ya kupimwa upya, kwa kujijua watakwama kwa vile ni kweli hawakupita kwa njia stahili. Hapo ndio huwa mwisho wa udanganyifu wao au matumaini ya wazazi wao.
Mwalimu anasema kwa wale wanaoshindwa kukidhi kiwango, wanawarudisha wizarani kwa ajili ya kutafutiwa skuli nyingine. Hakika hili ni jambo la kushangaza sana kila mtu anayelisikia.
Kumbe kati ya yale majina mengi yanayotangazwa redioni kuwa wanafunzi wamefaulu, yapo ya watoto waliopandikizwa kinyume na uwezo wao? Lahaula.
Hili ni tatizo kubwa na miongoni mwa vikwazo vikuu vilivyoishusha elimu yetu.
Ni hapo sitakuwa nimekosea kuhoji kauli au msimamo wa serikali kwamba elimu yetu bado haijaporomoka. Tukubali tu imebaki ya maneno matupu.
Chanzo: Fahamu
Inapofika mahali Kiongozi Mwenye madaraka na Uwamuzi kwa wananchi na ikatokezea kiongozi huyo amezaliwa katika familia ya kisilamu na yeye anajita ni Muisilamu halafu akatowa kauli kwa kusema haogopi hukumu ya Mmungu ujuwe binadamu kama huyo anaweza kuamrisha lolote lile na kufanya chochote kile .
ReplyDeleteSi rahisi kurudisha hadhi ya elimu katika visiwa vyetu vya Unguja na Pemba iwapo viongozi serikalini hawataacha itikadi zao za ubinafsi,uporaji na uingizaji siasa katika maswali ya elimu.Ninahakika Mheshimiwa Ali Juma anakumbuka fika darja ya elimu visiwani katika miaka ya 1960s.Ukilinganisha na sasa haifiki hata robo ya wakati ule.Kama sikosei katika mwaka 1963 Zanzibar ilichukua nafasi ya kwanza, katika Africa ya Mashariki, katika mchuano wa mtihani wa kidato cha nne.Kuna vijana wa Kizanzibari waliosoma Tanzania bara katika vyuo vya mifugo mnamo 1968,na miongoni ya wanafunzi walikuwemo wanafunzi sita wa Tanzania bara waliomaliza kidato cha sita,waliobaki wote ni kidato cha nne.Inafurahisha kusema katika mtihani wa mwisho wanafunzi wa Kizanzibari waliwashinda hata hao wa kidato cha sita.Inawezekana kurudisha hali ilivyo sasa ikiwa ipo nia safi ya kutekeleza hayo.
Delete