dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Friday, September 6, 2013

Tunataka Katiba ya mwafaka, siyo jeuri na kiburi

NA MHARIRI

6th September 2013


Katuni
Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kwa siku mbili mfululizo umekuwa shubiri bungeni.
Juzi wabunge wote wa kambi ya upinzani kutoka vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi walitoka bungeni kuonyesha kutokufurahishwa kwao na uamuzi wa kukataliwa kwa pendekezo la kuuondoa kwanza bungeni ili kutoa fursa kwa wadau wa Zanzibar kutoa maoni yao.

Jana ilikuwa ni tafrani tena baada ya pendekezo la kutaka kuondolewa bungeni kwa muswada huo kukataliwa baada ya kupigwa kura hali iliyoishia kiti cha spika kuamuru Kiongozi wa Kambi Rasmi Bungeni, Freeman Mbowe, kutoka nje kwa madai kuwa alikataa kutii kiti.

Hali iliyoonekana bungeni haikuwa nzuri kwa vigezo vyovyote vile.

Muswada huu umekuwa na mwelekeo unaovunja maelewano, mshikamano na kuna kila dalili kwamba wabunge wa kambi ya upinzani wanaamini kwamba serikali inatumia nguvu zake hasa kwa kujiegemeza kwenye wingi wa wabunge wake kuupitisha muswada huo.

Tangu jana asubuhi kulikuwa na dalili kwamba baadhi ya wabunge hawakuwa radhi muswada huo ujadiliwe katika mkutano wa sasa na badala yake walikuwa wanaomba uondolewe bungeni ili kufanya mashauriano.

Swali aliloulizwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwake, kama hakuona ni busara kwa serikali kuondoa muswada huo bungeni, ilikuwa ni kielelezo kingine cha kuonyesha kwamba bado kulikuwa na mwako mkubwa wa kisiasa kwamba mambo hayakuwa yamekaa sawa juu ya muswada huo.

Kimsingi muswada huu ni sehemu ya mchakato wa kuandika katiba mpya ambayo inatarajiwa kwamba ifikapo mwaka 2015 itakuwa tayari ili itumike kwenye uchaguzi mkuu wa rais na wabunge.

Hadi sasa Tume ya Katiba imekwisha kupokea maoni ya wananchi juu ya katiba wanayoitaka, imetayarisha rasimu ya katiba, imeunda mabaraza ya katiba, na yatari mjadala wa mabaraza umemalizika juu ya rasimu husika na mapendekezo yamewasilishwa kwa Tume.

Hata hivyo, pamoja na hatua zozote zilizopigwa hadi sasa juu ya mchakato wa katiba mpya, safari bado ni ndefu na ngumu. Ugumu wa safari hii unajikita kwenye jambo muhimu kubwa, maelewano ya kisiasa.

Kwamba ni kwa kiwango gani wadau wote kwa ujumla wao, iwe ndani ya bunge, nje ya bunge, ndani ya  baraza la wawakilishi, kwenye vyama vya hisari na kila mwenye kuitakia nchi hii mema na anayeweza kuwa na maoni juu ya  mchakato huu, wamehusika katika kuandaa sheria ambayo mwisho wa siku itawapatia katiba nzuri ambayo ni sheria mama.

Kwa upeo wetu, kazi ya kutunga katiba kwa mataifa mengi imekuwa ya mgogoro mkubwa sana. Yapo mataifa mengi ya Afrika ambayo yaliishia kusambaratishana kwa sababu tu ya kushindwa kuendesha vema mchakato wa katiba.

Kwa Tanzania kumekuwa na mwanzo mzuri. Awali kulikuwa na kishindo kilichosababisha rasimu ya awali ya sheria ya kuundwa kwa Tume ya Katiba kuamsha taharuki kubwa. Hali ilitulizwa kwa mazungumzo na kuingiza ndani ya muswada yale yote yaliodhaniwa kuwa na umuhimu wa kuzingatia maslahi mapana ya kitaifa.

Lakini pia kuna wakati Rais Jakaya Kikwete kwa hekima zake, aliamua kusikiliza kilio cha baadhi ya vyama vya siasa hata pale sheria ilipopitishwa kwa msukumo tu wa wingi wa wabunge wa chama tawala, bila kuzingatia maslahi mapana ya kitaifa.

Rais aliita makundi ya vyama vya siasa Ikulu na kupokea mawazo na mapendekezo yao ambayo yalizaa marekebisho ya sheria ya kuundwa kwa Tume ya Marekebisho ya Katiba.

Umauzi wa Rais Kikwete ulifikiwa bila kujali kwamba waliokuwa wamepitisha muswada husika walikuwa ni wabunge wa chama chake tena wakiwa wengi ndani ya bunge.

Hakung’ng’ana tu na hoja ya wingi wa wabunge wake. Hakubweteka tu kwa kuwa ana wabunge zaidi ya theluthi mbili wanaotokana na chama chake, ila  alisukumbwa na  hoja ya kutaka kuona makubaliano ya pamoja yanafikiwa katika machakato wa katiba mpya.

Kila sauti na hoja yenye nguvu inasikika, inazingatiwa kwa kuwa katiba ni maafikiano ya kitaifa kuliko dhana tu ya wengi wape.

Ni kwa msingi huu sisi tunasema kuwa mijadala ya kisiasa katika kutengeneza sheria katika mchakato mzima kuelekea kupatikana kwa katiba mpya, ni lazima dhana ya makubaliano ya kitaifa itawale akili za wale wote wanaodhani kwamba leo wako salama sana kwa sababu tu wanatokana na upande wa chama kinachounda serikali.

Ni vema ikaeleweka kwamba katiba ni zaidi ya vyama vya siasa. Ni zaidi ya uanachama wa chama cha siasa; ni misingi wa haki, uhuru na wajibu katika taifa.

Wapo wabunge wengi ndani ya bunge la sasa ambao awali hawakuwa wanachama wa vyama ambavyo vimewapa uwakilishi. Lakini, katiba ni ile ile, wakiwa chama tawala, wakiwa upinzani na vinginevyo.

Tunaasa kwamba hasira, jeuri, kiburi na unazi havitatupa katiba mpya inayokidhi vizazi vya sasa ni vijavyo. Tuwe makini.
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment