Hata hivyo, amesema uamuzi wa kuanzisha chama chake kipya cha siasa utasubiri kwanza uamuzi utakatolewa na mahakama katika kesi yake iliyopo mahakamani inayohusiana na uanachama wake ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Novemba 22 mwaka jana, Zitto alisimamishwa unaibu Katibu Mkuu wa Chadema na unaibu kiongozi wa upinzani bungeni baada ya kutuhumiwa kuhusika na njama za kukihujumu chama hicho.
Zitto alisema hayo juzi wakati akihojiwa kwenye kipindi cha Mkasi kinachorushwa na kituo cha televisheni cha EATV baada ya kuulizwa kuwa kuna fununu kwamba ana mpango wa kuanzisha chama chake kipya cha siasa.
“Kwa hivi sasa nina kesi mahakamani inayohusiana na uanachama wangu kwenye chama cha Chadema, kwa hiyo siwezi kusema lolote kuhusiana na kuanzisha chama kipya au hapana kwa sababu nasubiri maamuzi yatakayotolewa na mahakama,” alisema.
Alisema kwa jinsi ambavyo maamuzi ya kesi hiyo yatakuwa, kwa kuwa ni mwanasiasa na anataka aendelee kubaki kwenye jukwaa la siasa, nia yake ni kubaki kwenye siasa, lakini siyo katika Chama Cha Mapinduzi (CCM) au katika vyama mojawapo vya siasa vilivyopo.
Hata hivyo, wakati Zitto akisema hayo kumekuwapo na taarifa za kumhusisha Zitto na chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT)-Tanzania kutokana na viongozi wake kuwa ni waliotimuliwa ndani ya Chadema.
Miongoni mwa viongozi wa sasa wa chama hicho ni aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba, ambaye alisimamishwa uongozi sambamba na Zitto, lakini baadaye Chadema kilimfuta uanachama kutokana na tuhuma za uasi.
Mwingine aliyesimamishwa uongozi sambamba na Zitto na Mwigamba ni Profesa Mshiriki Kitila Mkumbo ambaye alikuwa mjumbe wa kamati kuu ya Chadema.
URAIS 2015
Kadhalika Zitto alisema ingawa angelipenda kugombea urais mwakaji, kikwazo ni katiba ya sasa na Rasimu ya Katiba mpya ambayo inaeleza sifa za mtu anayetaka kugombea urais ni lazima awe na umri wa kuanzia miaka 40 wakati katika nchi kama Kenya, Malawi, Marekani, Rwanda, Burundi, Msumbiji na Afrika Kusini ni miaka 35.
Zitto alisema kama hali itabaki hivyo, atamuunga mkono mgombea anayeijua nchi vizuri kwa sababu Tanzania inahitaji rais atakayewaunganisha Watanzania na siyo anayewagawa.
“Tunahitaji rais ambaye haya anayajua na ameonyesha ni namna gani atayatekeleza na siyo blabla,” alisema.
KUTUMIWA NA CCM
Zitto alisema amekuwa akisikia baadhi ya watu wakisema kuwa anatumiwa na CCM, lakini bahati mbaya wanaodai hivyo hawaelezi kwa undani anatumiwa vipi na chama hicho tawala.
“Hivi mbunge anayetumiwa na CCM anaweza akapeleka hoja bungeni kutaka kumuondoa madarakani Waziri Mkuu, anaweza akapeleka hoja bungeni ya kuhakikisha mikataba yote inakuwa wazi ikiwamo ya gesi?” alihoji.
Alisema wanaotoa madai hayo wajitokeze waseme wamefanya nini kwa ajili ya taifa lao na kwamba anachofahamu hizo ni propaganda tu za kisiasa na siasa nyepesi za Tanzania ambazo hazina mashiko.
ATOFAUTIANA NA UKAWA
Katika mahojiano hayo Zitto alisema si sehemu ya Umoja wa Kutetea Katiba ya Wananchi (Ukawa) kwa sababu vyama vinavyounda umoja huo ni pamoja na Chadema ambacho ana mgogoro nacho kutokana na kukifungulia kesi mahakamani akipinga kumvua madaraka.
Alisema ana msimamo tofauti na CCM na Ukawa kuhusu muundo wa Muungano kwani kwa mtazamo wake ni kuwa na Rais mmoja wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar na Tanganyika ziongozwe na mawaziri wakuu.
Alifafanua kuwa kufanya hivyo kutasaidia kuwa na Muungano imara kwani Muungano wa sasa hautendi haki kwa upande mmoja ambao hata hivyo, hakuutaja.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment