dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Friday, January 30, 2015

Balozi Ali na coalition ya Zanzibar

Balozi Ali Abeid Amani Karume - all in green!

Written by Foum from Mzalendo.net

Kwetu inawezekana

Moja kati ya hoja kubwa za sasa ni mfumo mzima wa serikali ya umoja iliopo hapa visiwani ambao kumekuwa na jitihada nyingi za kuufanya uonekane ukiwa haufai na wa kuondoshwa. Mifano mikubwa inayotolewa ni mfumo wa serikali ya Ujarumani ambayo kwa leo nimeona ipo haja ya kuuzungumza mfumo wenye na kuondosha utata unaopangwa makusudi kwa hoja zisizo na ukweli. Lengo ni kuwaelimisha wananchi na kuweka wazi pale kwa makusudi wenye maslahi yao binafsi hujaribu kuutia dosari mfumo kwa kuweka mnasaba na kitu kisichoshabihiana kihistoria au hata na mifumo mengine ya serikali nyingi duniani.
Ujarumani ni moja ya nchi zenye mfumo wa kipekee wa uongozi katika serikali yake. Upekee huu umekuja kutokana na historia ya nchi yenyewe hasa katika kipindi cha utawala wa Adolf Hitler, na mamlaka ya kidekteta ya Nazis. Tukumbuke nguvu kubwa alizokuwa nazo Hitler ndizo zilizopelekea kufanyika kwa vita ya pili ya dunia na ndio msingi wa serikali ya Ujarumani kujiwekea formula maalum kuhakikisha hakutatokea na uongozi wa “absolute power” kama wa Hitler utakaozaa mashaka kwa nchi na dunia kwa jumla.
Mkuu wa serikali ya Ujarumani ni “Chancellor” ambae kisheria na mantik anafanana na nafasi ya Waziri Mkuu katika serikali kama za Uingereza na nyengine ambazo si kijamhuri. Na tafauti ya Chancellor ukilinganisha na Waziri Mkuu ni kwamba Chancellor wa Ujarumani anakuwa “elected” wakati nafasi ya Waziri Mkuu mara nyingi huuongozwa na kiongozi wa chama cha siasa chenye viti vingi bungeni. Chancellor ndie mwenye uwezo wa kuunda Baraza la Mawaziri na ndie mwenye kuongoza sera za serikali ambayo inawajibika kwa wananchi kupitia katika bunge lao liitwalo Bundestag. Kinadharia mkuu wa nchi ya Ujarumani ni Chancellor na ndio maana ukakuta shughuli zote zinamweka mbele yeye kama ilivyo kwa Waziri Mkuu katika Himaya ya Muingereza.
Nafasi ya Urais wa Ujarumani ni tafauti kabisa na mfumo wa Rais katika serikali ya Jamhuri kama ilivyo hapa nchini. Rais wa Ujarumani hachaguliwa kwa kura za wananchi moja kwa moja kama ilivyo kwa Rais wa Zanzibar, wala hana nguvu za kipekee kama ilivyo kwa Rais wa Zanzibar ambaye huhitaji ushindi katika uchaguzi mkuu ili kuweza kuunda serikali. Kinadharia nafasi ya Rais wa Ujarumani ni “ceremonial” yenye nguvu lakini kwa ridhaa zaidi ya Chancellor pamoja na Bundestag. Ili kuweza kupatikana kwa Rais wa shirikisho la Ujarumani hufanyika uchaguzi umaoongozwa na convention maalum ya uongozi katika bunge lao pamoja na wale wanaounda shirikisho lao. Nguvu za Rais wa Ujarumani zinakizuizi kikubwa kutokana na katiba yao ya kifungu 58 kinachomlazimisha kwanza kupata ridhaa ya Chancellor wa Ujarumani.
Ukitazama hii nafasi ya Rais wa Ujarumani haina tafauti kubwa na nafasi ya malkia wa Uingereza, kwa sababu katiba zao zimewapa heshima kubwa lakini mamlaka yao yanazingatia kwanza makubaliano na muendeshaji mkuu wa nchi ambae kwa Uingereza ni Waziri Mkuu na kwa Ujarumani ni Chancellor. Kinachotafautisha mfumo wa serikali ya Ujarumani na wa nchi nyengine ni msingi wa “Basic Law” ambao umeibuka kama suluhishisho la kuepukana na uongozi wa kiimla kama uliokuwa wa wakati wa Hitler. Hivyo kimsingi Ujarumani ni ngumu sana kuongozwa na serikali ya chama kimoja na ndio maana ukakuta mara nyingi kutokana na vikwazo hivyo vya kisheria na katiba yao serikali ya Ujarumani hufuata mfumo wa serikali za Umoja wa vyama tafauti (Coalition goverment).
Tumeona kwa ufupi mfumo wa uundwaji wa serikali ya shirikisho la Ujarumani linazungukwa na mambo manne muhimu. Kwanza Bunge lao, pili Mkuu wa Serikali ambae ni Chancellor, tatu ni Rais ambae ndie “head of state” na mwisho ni katiba yao inayoshurtisha mfumo wa serikali ya umoja wa kitaifa. Katika nafasi ya Chancellor, pia iko nafasi ya Makamo wake, ambae mara nyingi hutoka katika vyama vinavyounda ushirika katika uongozi wa serikali. Hivi sasa Chancellor wao ni Dr Angela Merkel wa kutoka chama cha CDU na Makamo wake ni Sigmar Gabriel kutoka SPD. Kujuwa umuhimu wa hii nafasi ya Vice Chancellor basi turudi nyuma mwaka 1974 ambapo nafasi hii iliidhinishwa na Rais wa shirikisho kuendesha serikali baada ya kujiuzulu kwa Chancellor mpaka uchaguzi ulipoitishwa.
Sasa turudi kwenye hoja ya Balozi Ali ambae anasema mfumo huu wa kwetu ni potofu na unaomzawadia alieshindwa nafasi kubwa ya serikali na kufika hadi kusema hata huko Ujarumani hakuna Rais na Makamo wake. Mwishowe anamalizia kwa kusema kwamba mfumo wa kijarumani katika coalition government ni kwa mawaziri tu si kwa Rais. Kutokana na mazingira ya mfumo wa Ujarumani tulioutazama hapo mwanzo utakuta anachokisema Balozi kimekosa hoja kwa sababu mfumo wa serikali ya Zanzibar hauendani kabisa na wa Ujarumani. Kwanza nafasi ya Urais katika serikali ya shirikisho ya Ujarumani haufanani na wa kwetu kwa vile Rais wetu ndie huchaguliwa moja kwa moja na wananchi wakati wa Ujarumani huchaguliwa na wajumbe kutoka mabunge yao katika kongamano maalum.
Pili Rais wa Ujarumani hawezi kutimiza lolote bila ya kwanza ridhio kutoka kwa Chancellor au Bunge la nchi, hivyo nafasi yake haiwezi kufananishwa sawa na Rais mwenye mamlaka ya juu ya serikali anayoiongoza. Baraza la Mawaziri la serikali ya Zanzibar huchaguliwa na Rais wa nchi wakati la Ujarumani huchaguliwa na Chancellor kwa uhuru wake. Huwezi kuzifananisha nafasi za Rais katika mfumo wa Jamhuri kuwa sawa na nafasi za rais mwenye mamlaka yenye kipimo cha ceremonial. Hapa hatutaweza kuyatendea haki maelezo yetu kwa kutazama mfumo wa nchi mbili tafauti katika uongozi.
Lakini tuende sasa katika shughuli za serikali katika mfumo wa shirikisho la Ujarumani, la mwanzo la kulitazama ni jinsi gani serikali ya Ujarumani inajiendesha katika mfumo wa coalition government. Rudia nyuma kwamba Mkuu wa serikali ni Chancellor ambae ndie anaeunda Baraza la Mawaziri na ndie ambae huchaguliwa kwa wingi wa kura katika bunge lao. Kwa huku kwetu uchaguzi unaendeshwa katika mfumo wa “republic democracy” ambapo Rais huchaguliwa moja kwa moja na kuunda serikali bila ya kuhitaji ruhusa kwa yeyote sawa na chancellor democracy ambayo huunda serikali baada ya uchaguzi wa kumchagua chancellor mwenye mamlaka kamili ya uongozi. Lakini muundo wa serikali huo hauishii kwa mawaziri tu kama anavyotaka tuamini, bali hata kwa Makamo wake ambae hutoka katika chama kinachoshikiri katika uundaji wa serikali.
Sasa tazama namna gani nadharia potofu inapofananishwa na moja ya demokrasia kubwa duniani. Uchaguzi wa Ujarumani umeweka kiwango cha asilimia tano za kura kwa chama kidogo kitachoweza kushiriki katika uundwaji wa serikali ya umoja wa kitaifa. Mfano ukitazama asilimia ya viti kwa CDU cha Dr Merkel ni asilimia 33.8 na kwa wingi wa kura ni asilimia 41. Wakati mshirika wake alieunda serikali wa chama cha SPD ilivuna asilimia 23 ya viti pamoja na wingi wa kura wa asilimia 25. Hoja iko hapa kwetu washirika wa muundo wa serikali ya umoja walipishana kwa asilimia 1 tu kwa vile CCM ilikuwa na alimia 51 wakati CUF ilikuwa na asilimia 49, Jee kati yetu na Ujarumani ni nani hasa anaezawadia alieshindwa nafasi ya uongozi? Na ikiwa Balozi anautukuza mfumo huo wa Ujarumani kwa vile tu hautoi Makamo wa Urais, kwa nini asiwabeze na wajuramani hao hao ambao wameunda serikali ya umoja wakiwa na popular votes kwa CDU asilimia 41 wakati SDP ni asilimia 25?
Kama hoja ya kwamba hakuna mfano wa serikali ya umoja yenye Rais na Makamo kutoka chama ushirika basi kwa nini aende mbali kuutazama wa Ujarumani bali ya jirani zetu Kenya ambao walikuwa na mgogoro unaofanana na wa kwetu kupelekea kuundwa serikali ambayo Rais Kikwete aliisimamia. Kwa nini asiseme tu hakukuwa na haja ya kuwa na Makamo wa pili ambae hana kura za wananchi za kumpa heshima hio na pili ikiwa ni muumin madhubuti wa serikali ya umoja kutokana na mchanganuo wa kura za washindani? Kwa nini tusiwe kama Kenya yenye Rais wa chama kilichobeba kura nyingi na Waziri Mkuu wa kutoka upinzani mwenye popular votes, au kama ilivyokuwa Zimbabwe na hata tunapoelekea katika mfumo wa serikali ya Sudan ya Kusini? Kinachonishangaza ni nguvu nyingi kuwekweza kwa alietoa changamoto kubwa kwa wingi wa kura za asilimia 49, huku akitukuzwa Makamo wa pili alieshinda kwa kura za jimbo lenye watu wasiozidi alfu tano, jee hio ndio tafsiri ya demokrasia pana tunayotakiwa kuitukuza katika ulimwengu wa sasa?
Turudi kwenye hoja ya kwamba serikali za umoja haziishii kwenye mawaziri tu bali hupishana baina ya mkuu wa serikali na makamo wake kama ilivyo Ujarumani ambayo Chancellor ni kutoka CDU lakini Vice Chancellor kutoka SPD. Hizi ni nafasi kubwa katika uongozi wa nchi, haziwezi kufananishwa na mawaziri tu kwa sababu kama tulivyoona mwaka 1974, Vice Chancellor ndie alieiongoza serikali wakati wa kujuzulu kwa Chancellor mpaka uchaguzi ulipoitishwa. Hata katika mfumo wa serikali ya sasa ya Uingereza, Makamo wa Waziri Mkuu ni kutoka upinzani tena kwa wingi wa popular votes za asilimia 23 tu lakini akaweza kuwa mshirika wa serikali ya sasa na kuchukuwa nafasi ya pili ya juu ya serikali. Hebu tuondoshe giza la fikra tulizonazo na tuwe wakweli hivi tunafikiri Raila Odinga angelikubali kuunda serikali ya Umoja wao kama si kupewa dhamana ya Waziri Mkuu ambae angelisimamia mabadiliko ya katiba yao, tume ya uchaguzi na uendeshaji wa serikali yao kabla ya uchaguzi uliofuatia?
Ikiwa tunashangaa na kuchukizwa na mfumo wenye Rais na Makamo wawili visiwani, basi tungelionyesha kwanza mfano kwa kupinga uchafu zaidi wa kuwa na rasimu pendekezwa ya Rais na makamo wa tatu wa muungano. Sifahamu mantiki hasa ya kuharamisha ya Zanzibar kwa vile tu kuna nafasi ya wapinzani kuunda serikali, lakini tukahalalisha ya muungano yenye Rais, Makamo wa Kwanza, wa pili na wa tatu kwa sababu tu upo uwezekano mkubwa wa nafasi hizi kushikwa zote na chama tawala? Hatuzitendei haki dhamana zetu za uongozi na tunajivunjia heshima kwa kutokuwa wa kweli katika hatima ya uongozi na demokrasia pana tunayoihitaji.
Ikiwa hoja ni kuzuia zawadi kwa walioshindwa, jee kwa nini tuishie kwa Makamo tu wa kwanza wa Rais na si kwa Mawaziri na dhana nzima ya kuundwa kwa serikali ya pamoja? Ikiwa dhamana ya kuthamini demokrasia ya wingi wa kura za asilimia 49 za mgombea mmoja ni zawadi katika serikali ya umoja, ya nini kushughulika zaidi na nafasi ya Makamo (ambayo kusema kweli haina nguvu zaidi ya kumshauri tu mkuu wa nchi) na tusijikite pia kwa kufuta nafasi za Baraza la Mawaziri na mfumo mzima wa serikali ya umoja? Sababu ya kuunda SUK ni kura za mshindi za asilimia 49, tusipoona umuhimu wa wingi huu katika multiparty democracy kuna haja ya mawaziri kutoka upinzani?
Ni kawaida yetu kuvunja kwetu na kujenga kwa majirani, na ndio maana tulishiriki ipasavyo kwa asilimia 100 kurejesha amani na utulivu Kenya kwa uundwaji wa serikali ya umoja, hata Zimbabwe na sasa Sudan ya kusini. Sishangai na baadhi ya hizi kauli, wakati Zanzibar ilipozama katika hasama za kisiasa wengi hawakuwako kushuhudia idhlali ya kuishi kwa mfarakano, hawafahamu madhila ya majirani wanaosusiana kwa sababu ya itikadi wala hawatatambua insafu ya utulivu unaokuja na mfumo wa serikali za pamoja kwa vile maslahi na uchu wa uongozi binfasi ni mkubwa mno kuliko maslahi ya nchi na wananchi walio wengi.
Aluta continua.

No comments :

Post a Comment