dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Wednesday, April 1, 2015

ACT Ya Zitto kuharibu kura za Ukawa?


  • Wachambuzi kadhaa wa masuala ya siasa wanasema, Zitto Kabwe hapaswi kubezwa, kwani ana uwezo wa kuathiri matokeo ya upinzani.
Huenda mpango wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kufanya vizuri katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, ukatibuliwa kufuatia tishio lililopo la chama kipya cha siasa cha ACT.
Duru za siasa zinakitazama Chama cha ACT chini ya Zitto Kabwe aliyefukuzwa Chadema hivi karibuni, kama tishio kubwa kwa upinzani nchini. Ni chama  kinachoweza kusababisha CCM iendelee kuwa kinara katika chaguzi za Tanzania.
Zitto, mwanasiasa machachari aliyejiunga na ACT, anatajwa kujijengea ngome katika baadhi ya maeneo yanayotegemewa na Ukawa, jambo linaloelezwa na baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa kuwa  huenda likazorotesha nguvu ya upinzani, endapo chama hicho kichanga katika siasa kitaamua kusimamisha wagombea katika maeneo hayo.
Baadhi ya mikoa inayoonekana kuwa tegemeo kwa upinzani chini ya Ukawa na ambayo Zitto anaonekana kujenga himaya yake,  ni pamoja na mkoa wa Kigoma wenye zaidi ya majimbo sita ya uchaguzi ambayo yanategemewa  na upinzani.
Mikoa mingine ni Mtwara, Lindi, Shinyanga, Kagera, Katavi, na Sumbawanga.
Kwa Kigoma majimbo yanayotajwa kuwa hatarini kumezwa na ACT yanatajwa kuwa ni pamoja na Kigoma Mjini, Kigoma Kaskazini, Kigoma Kusini, Muhambwe, Kasulu Vijijini na Kasulu Mjini.
Majimbo mengine ambayo ACT inaonekana kuwa na ushawishi na inaweza au kuyatwaa au kusababisha Ukawa kukosa ushindi ni pamoja na Mpanda na Sumbawanga Mjini.
Zitto ajigamba
Katika kudhihirisha amejipanga vyema kushiriki Uchaguzi Mkuu ujao na kufanya vyema kupitia ACT ambacho kwa muda mrefu amekuwa akihusishwa kukiasisi, Zitto anasema:
“Mimi ni mchapakazi, siangalii nyuma tena, naangalia mbele. Mapambano yanaanza, matokeo mtayaona baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.”
Alitoa majigambo hayo alipotangaza kujiunga rasmi na chama hicho mwishoni mwa wiki, huku akiwa na kundi la watu waliowahi kuwa wanachama na viongozi wa Chadema.
Swali kuu ni; je, ACT kikiwa katika hatua za uchanga, kinaweza kuleta ushindani katika uchaguzi
?
Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana, anasema kuwa kama ACT kitajipanga vizuri kinaweza kufanya vizuri hasa kwa kupata idadi nzuri ya wabunge.
Akifafanua kuhusu kujipanga vizuri, anasema: “Kisiwe na migogoro na kiwe chama kitakachojengwa kama taasisi, kwa maana ya kuwa na mifumo, sera na mikakati inayoeleweka.’’
Kuhusu nafasi ya Zitto, Dk Bana ambaye ni miongoni mwa wasomi wanaojitokeza kuchambua masuala mbalimbali ya kitaifa, anasema kuwa mwanasiasa huyo ana umuhimu mkubwa katika siasa za Tanzania kwa kuwa ana uzoefu na mvuto hasa kwa vijana.
“Kwa kuwapo ndani ya ACT, wanaweza kupanda chati haraka na kuwa miongoni mwa vyama vya siasa vyenye wafuasi wengi na vyenye nguvu nchini,” anaeleza.
Anasema kumpuuza ni kujidanganya, kwani historia aliyojijengea hakuna mtu anayeweza
“Zitto bado ni hai kisiasa, anajua kujenga hoja na akaisimamia mpaka mwisho. Angalia hoja zake nyingi alizozijenga mpaka leo zinaisumbua CCM. Ana ushawishi mkubwa na anaheshimika na kupendwa ndani ya nchi kwa jumla.”
Anaongeza: “Pamoja na uwezo wake, asaidiane na wenzake kuhakikisha kile chama kinajengwa kama taasisi, kijulikane kuwa ni chama cha siasa chenye wafuasi na viongozi wake wawe na sera mbadala zinazojikita katika misingi aliyosimamia Baba wa Taifa.”
Kura za Chadema kupungua?
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa George Shumbusho anasema licha ya changamoto kubwa iliyopo kwa Zitto na ACT, anaamini mwanasiasa huyo ataondoka na wanachama wa Chadema, hivyo kupunguza kura za chama hicho kikuu cha upinzani nchini.
Hata hivyo, anatoa angalizo kwa ACT akisema kinakabiliwa na changamoto ya kuruhusu kuendeshwa kwa msingi wa nguvu ya mtu mmoja.
Changamoto hiyo inaweza kukififisha haraka chama hicho, akitoa mfano wa enzi za Augustine Mrema aliyetumia nguvu binafsi kuipaisha NCCR Mageuzi.
“Hofu yangu ni kuwa kama Zitto anataka kujenga ACT, anahitaji muda zaidi kujipanga au vinginevyo aungane na Ukawa ambapo huko chama chake kinaweza kupata umaarufu zaidi,” anaeleza.
Mtazamo wa Mchungaji Msigwa
Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, anasema kuwa haamini kama Zitto ana uwezo wa kuugawa Ukawa, kwa kuwa hata umaarufu wake ulijengwa na Chadema.
Kudhihirisha udhaifu wa Zitto kisiasa, anasema ni kushindwa kwake kuondoka na kiongozi hata mmoja muhimu wa Chadema na kubaki akiokoteza anayoyaita makapi yaliyofukuzwa na chama hicho.
“Katika vitu ambavyo havitunyimi usingizi katika Uchaguzi Mkuu ujao ni ACT na Zitto…siyo tishio kwa Ukawa hata kidogo.
Hawezi kuipasua Chadema wala Ukawa, na mtakubaliana nami baada ya uchaguzi mkuu kufuatia matokeo atakayoyapata,” anasema.
Peter Kuga Mziray
Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini, Peter Kuga Mziray anasema kuwa Zitto atatoa upinzani unaoweza kuitikisa Chadema na Ukawa kwa jumla.
Anasema licha ya ukweli kuwa Chadema ni chama kikubwa chenye mizizi sehemu kubwa ya nchi, uwezo na umaarufu wa Zitto utakiletea upinzani mkubwa katika baadhi ya maeneo.
“Huwezi kumbeza, hakosi wabunge siyo chini ya 10. Anayo safari nyingine ndefu lakini siyo wa kupuuzwa, kwani anaweza kufanya maajabu,’’ anaeleza.


No comments :

Post a Comment