dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Friday, April 17, 2015

Tuwe na Baraza la Wazee washauri wa taifa, siyo Chama!

Image result for ali hassan mwinyi

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimeunda chombo kitakachokuwa na jukumu la kuwashauri watendaji wakuu wa chama hicho, na hasa katika masuala makubwa, mazito na nyeti yanayogusa mustakabali wa taifa letu.
Chombo hicho kimepewa jina la Baraza la Wazee la Ushauri wa Chama. Kwa kuitwa baraza la wazee, maana yake ni kwamba viongozi na wajumbe wake wanapaswa na wana haki, kwa heshima ya chombo hicho, kuitwa wazee.
Halmashauri Kuu ya CCM, chini ya Mwenyekiti wake, Jakaya Kikwete, imemteua Mzee Ali Hassan Mwinyi kuwa Mwenyekiti wa Baraza hilo, huku Mzee Pius Msekwa akiteuliwa kuwa Katibu wa Baraza. Wajumbe ni Mzee Benjamin Mkapa, Mzee John Malecela, Mzee Dk. Salmin Amour Juma na Mzee Amani Abeid Karume.
Mzee Mwinyi na Mzee Mkapa, wenyeviti wastaafu wa CCM, na pia marais wastaafu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Mzee Dk. Salmin na Mzee Amani ni makamu wenyeviti wastaafu wa CCM (Visiwani), na pia marais wastaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, wakati Mzee Msekwa na Mzee Malecela, mbali na kuwa makamu wenyeviti wastaafu wa CCM (Bara), wamewahi pia kuwa Spika wa Bunge (Msekwa) na Waziri Mkuu na Makamu wa kwanza wa Rais (Malecela).
Kwa kifupi, Bazara hilo la Wazee, limeundwa na wajumbe sita; watatu kutoka kila upande wa Muungano. Wajumbe wote hao, ni wazoefu katika uongozi wa nchi hii, uongozi wa kisiasa na ni wazoefu katika masuala ya kidiplomasia.
Kuwaundia jukwaa la kisiasa pekee, na kuwapachika kwenye Chama kimoja pekee, katika nchi yenye vyama vingi vya siasa, ni kutowatendea haki. Wazee wetu hawa waundiwe Baraza la Wazee la Ushauri wa Taifa, na baraza hili litambulike kikatiba, na hivyo litamkwe na Katiba Mpya tunayotarajia kuiunda.
Nasema CCM imefanya vizuri kuja na wazo hili la kuwaweka pamoja wazee hao kwa kuwaundia jukwaa lao. Lakini CCM imekosea kwa kuwapatia jukumu la kuwa washauri wa chama chao. Hawa wanapaswa kupatiwa jukumu la kuwa washauri wakuu wa Taifa, kwa mambo yote ya kitaifa.
Na ili kuwapa hadhi ya kitaifa na wakubalike kitaifa, kila chama chenye wabunge ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano, kitoe wazee sita wa kuingia katika chombo hicho, na Katiba ijayo ielekeze hivyo.
Watanzania wenzangu naomba mnielewe. Tangu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere afariki dunia Oktoba 14, 1999, taifa letu hili limeishi kama mtoto yatima. Halina baba wa kulisemeaTangu Mwalimu afariki dunia, Watanzania hatuna pa kukimbilia kuzishitaki tawala zetu na watawala wetu pindi wanapochukua au kufanya uamuzi wa hovyo. Hii ni tofauti na enzi za uhai wa Mwalimu.
Tuko kwenye mchakato wa kuandika Katiba Mpya. Tunahitaji mno kuwa na Baraza la Wazee Washauri wa Taifa letu, watakaosaidia kuwashauri Watanzania kwa umoja wao kupitia Tume ya Mabadiliko ya Katiba, juu ya mambo yapi yanabakia kuwa tunu za taifa letu, na yasiyostahili kuguswa kabisa ili kudumisha amani na mshikamano wetu ili kudumisha Muungano wetu wa Tanganyika na Zanzibar.
Kipindi tulichomo sasa hakina tofauti na kipindi kile cha mwanzoni mwa miaka ya 1990, yalipoibuliwa mambo makubwa mawili yaliyotishia kusambaratisha kabisa taifa letu, lakini tukabakia salama kwa sababu tu tulikuwa na Baba wa Taifa, ambaye jamii nzima ya Watanzania ilimheshimu.
Mambo makubwa hayo yaliyotishia kulitikisa taifa letu, kwanza; ilikuwa ni kuamua tuwe na mfumo wa vyama vingi vya siasa au la, na pili; ilikuwa ni kuibuka kwa kundi la wabunge wa G55 ambao walitaka kurejeshwa kwa taifa la Tanganyika ndani ya Muungano.
Katika kipindi hicho, wahafidhina ndani ya CCM hawakutaka kusikia kabisa kitu kinachoitwa mfumo wa vyama vingi vya siasa. Walitaka CCM iendelee kuwa chama pekee cha siasa nchini, kinachoendelea kushika hatamu zote za uongozi wa taifa hili.
Kwa upande wa pili, lilijitokeza kundi la wale waliokuwa wametupwa nje ya mfumo wa uongozi wa nchi baada ya kushindwa kuishi na kuhimili mfumo wa uongozi wa CCM. Hawa nao wakawa kama wamefunguliwa kutoka kifungoni, wakawa na ndoto za kutesa kwa zamu, wakajiapiza kwamba lazima mfumo wa vyama vingi vya siasa vije ili CCM ing’olewe madarakani.
Katika mparanganyiko huo wa kitaifa, Tume ya Jaji Francis ikaundwa. CCM ikatuma makada wake kila kona ya nchi kuwahamasisha wanachama wao na wananchi kwa ujumla waukatae mfumo wa vyama vingi. CCM ikafanikiwa katika hili.
Tume ya Jaji Nyalali na kundi la wapenda mabadiliko ya mfumo wakaambulia asilimia 20, huku wahafidhina wa ndani ya CCM wakizoa asilimia 80. Ushindi wa kimbunga. Ushindi huo wa kura za maoni ya wananchi kuhusu swali lililouliza kama Watanzania tunataka vyama vingi vya siasa au la, uliwafanya wahafidhina wa CCM waingie katika vikao vyao wakiwa vifua mbele, wengi wao wakiamini katika demekorasia ya wengi wape.
Huko kwenye vikao vyao, wakamkuta Baba wa Taifa akiwa meza kuu. Mwenyekiti wa vikao, Ali Hassan Mwinyi, akasoma agenda za kikao. Mwalimu akazisoma nyuso za wahafidhina hao, kisha akawaambia wajumbe kwamba mandhali tunayo asilimia 20 ya Watanzania wanaopenda tuwe na mfumo wa vyama vingi vya siasa, basi pamoja na uchache wao, wanayo haki ya kusikilizwa…mfumo wa vyama vingi uruhusiwe uje, utasaidia kuiamsha CCM isilale. Wahafidhina wote ndani ya CCM wakanywea, hilo likaisha.
Likaja jingine la pili. Hili lilikuwa ni jaribio la kutaka kuvunja Muungano. Lilianzia na kuratibiwa bungeni na kundi la wabunge waliojipachika jina la G55, kabla ya kundi hilo kupata baraka za watendaji wakuu wa ndani ya CCM na Serikali yake.
Hoja yenyewe hiyo ya kutaka kurejeshwa kwa Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano, ilikuja kama mzaha tu kutokana na majibu ya aliyekuwa Rais wa Zanzibar wa wakati huo, Komandoo Dk Salmin Amour Juma kwa wabunge hao, ambao baadhi yao waliohoji mantiki ya Zanzibar kujiunga na Jumuiya ya Nchi za Kiislamu (OIC).
Wakati hoja hiyo inaibuliwa bungeni, tayari Zanzibar ilikuwa imeshajiunga na OIC. Yalikuwepo madai kwamba kujiunga huko kwa Zanzibar OIC, kuliratibiwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimatifa, iliyokuwa chini ya Ahmed Hassan Diria, ambaye alikuwa ni Mzanzibari.
Wabunge bungeni Dodoma wakahoji ni kwa vipi Zanzibar kama Zanzibar inaweza kujiunga na jumuiya ya kimataifa, wakati masuala yote ya nje na ushirikiano wa kimataifa katika mambo ya Muungano, yako chini ya Jamhuri ya Muungano.
Dk Salmin akazisikia kelele za wabunge wa Bara bungeni Dodoma. Akawajibu kwa ‘jeuri’ kwamba wote wanaohoji hilo la Zanzibar kujiunga na OIC walikuwa wanatikisa kibiriti, na kwamba wanapaswa kufahamu kuwa kibiriti hicho kimejaa, hakitikisiki.
AahMbunge wa Lupa, Njelu Kasaka, mbunge wa kuteuliwa Jenerali Ulimwengu na mbunge wa Kibondo, Arcado Ntagazwa, wakawaongoza wabunge wenzao kupima ujazo huo wa kibiriti hicho cha Komandoo Salmin. Wakakitikisa, kikatikisika hadi mwangwi ukamfikia Baba wa Taifa.
Mwalimu akawaita wabunge hao nyumbani kwake Msasani, Dar es Salaam. Akasikiliza hoja za wabunge wa G55 bila kufikia muafaka, hadi vikafika vikao vinne. Mwalimu akaamua kutoka ndani na kuita waandishi wa habari ili awape salamu viongozi na watawala wa nchi hii.
Hoja ya G55 ikafa kifo cha mende, suala la Zanzibar kujiunga na OIC likafa kifo cha mende. Kibiriti cha Komandoo kilichokuwa kimejaa, kikabakia kasha tupu lisilokuwa hata na njiti moja. Watanzania kama taifa, tukasonga mbele hadi leo.
Hoja ya Serikali tatu ndani ya Muungano iliyoanzishwa na kuratibiwa bungeni na wabunge wa G55 kabla ya kuzimwa na Mwalimu, imerejea tena katika mijadala ya kura za maoni mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba inayoongozwa na Jaji Joseph Sinde Warioba.
Watanzania tunaye wa kumkimbilia ili kuzuia Serikali tatu ndani ya Muungano wetu huu? Mwalimu, katika kuzima hoja hiyo ya Serikali tatu, mbali ya kutumia hoja ya sera za chama chake, CCM, aliwahoji Watanzania kama wamekwishampata Boris Yeltsin wao atakayeiongoza Serikali ya Shirikisho. Yeltsin alikuwa mtawala wa zamani wa Shirikisho la Nchi za Urusi kabla ya taifa hilo kusambaratika mwishoni mwa miaka ya 19980.
Baraza la Wazee la Ushauri kwa Taifa, linaweza kuwa kimbilio letu katika kuzuia Serikali tatu hizi, ambazo kwa vyovyote vile iwavyo, akitokea kiongozi wa ovyo akaingia Ikulu ya Tanzania au Ikulu ya Zanzibar, na akaikuta Tanganyika au Zanzibar huru, yenye mamlaka kamili ya nchi, atatangaza uasi, na huo utakuwa mwisho wa Muungano wetu.
- See more at: http://www.raiamwema.co.tz/tuwe-na-baraza-la-wazee-washauri-wa-taifa-siyo-chama#sthash.m5F0YGoM.dpuf

PIA SOMA - http://zanzibarnikwetu.blogspot.ca/2015/04/mkapa-mwinyi-karume-wakutana-kuinusuru.html

No comments :

Post a Comment