dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Thursday, April 2, 2015

Vurugu kura ya maoni bungeni

WABUNGE wa upinzani jana walisababisha kikao cha asubuhi cha Bunge kivunjike, baada ya kusimama na kutaka Waziri Mkuu Mizengo Pinda atoe kauli juu ya mustakabali wa uandikishaji wapigakura na hatima ya kura ya maoni.
Spika wa Bunge, Anne Makinda, alilazimika kuahirisha kikao hicho baada ya wabunge hao kusimama wote na kuwasha vipaza sauti wakimtaka Pinda atoe kauli, kwani kwa muda mrefu Serikali imekuwa haitoi majibu ya suala hilo.
CHANZO CHA VURUGU
Dalili za vurugu zilianza kuonekana baada ya kumalizika kipindi cha maswali na majibu ambapo Mbunge wa Kisarawe, Selemani Jafo (CCM), aliomba mwongozo wa Spika akitaka chombo hicho kisitishe shughuli zilizokuwa zimepangwa na kijadili mustakabali wa Katiba Inayopendekezwa ili Serikali iwasilishe muswada wa sheria kwenye kikao cha 20 cha Bunge ili Katiba ya mpito ipitishwe.
Wakati akiomba mwongozo huo, baadhi ya wabunge wa upinzani walikuwa wamewasha vipaza sauti wakimpinga kwa madai kuwa suala analotaka siyo la dharura.
Baada ya Jafo, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema) naye aliomba mwongozo kwa kanuni ya 47 (1) inayohusu shughuli za Bunge zilizopangwa kwa siku hiyo kuahirishwa ili jambo la dharura lijadiliwe.
Alisema hadi sasa uandikishaji wapigakura nchi nzima haujakamilika hata kwa Mkoa wa Njombe pekee na Watanzania wapo katika sintofahamu ni lini wataandikishwa kwenye daftari la kudumu la wapigakura.
“Jambo hili ni la dharura kwa sababu ilikwishatolewa hoja ya dharura juu ya jambo hili katika mkutano uliopita wa Bunge, ukaagiza Kamati ya Bunge ishughulikie, majibu yatolewe kwenye mkutano huu wa Bunge, leo mkutano unakwenda kufungwa bila majibu kutolewa.
“Tusitishe shughuli zote tuhakikishe tunajadili, majibu yapatikane leo katika mkutano huu wa Bunge, nimeomba miongozo juu ya jambo hili mara mbili na mara zote Serikali kupitia kwa Waziri Mkuu naamini umeipa maelekezo ya kutoa majibu, lakini inakwepa kutoa majibu.
“Katika mazingira kama haya hakuna sababu yoyote ya kuendelea na mjadala wowote katika mkutano huu wa Bunge wala kusubiria chochote, tupate majibu ili tuweze kufanya kazi ya kuishauri na kuisimamia Serikali kwa mujibu wa Ibara ya 63 (2) ya Katiba ya nchi.
“Waziri Mkuu yupo hapa anaweza kutoa majibu na tukajadili jambo hili hapa,” alisema Mnyika.
Baada ya Mnyika kumaliza kuomba mwongozo, Spika Makinda alisema: “Hoja hii inafanana na hoja ya kwanza (ya Jafo).”
Baada ya kauli hiyo, Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali (NCCR-Mageuzi), aliwasha kipaza sauti bila kuruhusiwa na Spika na kusema hoja hizo hazifanani.
“Hoja hii haifanani na hoja ya kwanza, ile ya kwanza inataka majibu ya mkutano wa 20 na hoja hii ya pili inataka majibu mkutano huu,” alisema Machali.
Wakati Machali akiendelea, Mnyika huku akimnyooshea mkono waziri mkuu alisikika akisema: “Hoja hii itolewe majibu Waziri Mkuu yupo hapa… atoe majibu.”
Naye Machali alidakia tena na kusema: “Tunataka majibu, tumechoka kuburuzwa.”
Spika Makinda aliwajibu kwa kusema: “Anawaburuza nani, nimewaambia kwamba swali lile litajibiwa leo (jana).”
Huku wabunge hao wakiwa bado wamesimama, Spika alimwita Msemaji Kambi ya Upinzani kwenye Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Susan Lyimo ili asome maoni ya kambi hiyo juu ya Muswada wa Sheria ya Miamala ya Kielektroniki ya mwaka 2014 na ule wa Makosa ya Kimtandao wa mwaka 2015.
Hata hivyo, msemaji huyo hakwenda kusoma maoni yake na badala yake waliendelea kushinikiza kutaka majibu kutoka kwa waziri mkuu.
Baada ya kuona hali hiyo inaendelea, Makinda aliahirisha kikao hicho.

JAFO
Awali akiomba mwongozo wake, Jafo alisema taarifa zilizopo ni kwamba wananchi wamejitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapigakura, lakini kuna changamoto za upungufu wa vitendea kazi (Mashine za Biometric Voters Registration – BVR).
Alisema kutokana na hali hiyo, ni vigumu upigaji kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa ukafanyika Aprili 30 kama ilivyopendekezwa.
Jafo alisema upigaji kura ya maoni utatanguliwa na utoaji wa elimu kwa mpigakura, jambo linaloonyesha kuwa muda wa kufanya yote hayo haupo.
“Sisi tuna dhamana ya Watanzania, hali halisi tunaiona, zoezi la uandikishaji bado linaendelea, tutumie mkutano wa 20 kikao cha mwisho tuhakikishe Serikali inaleta muswada wa hati ya dharura, kwamba Bunge lipitishe Katiba ya mpito,” alisema Jafo.
Alisema katiba hiyo ibebe mambo makuu manne ambayo ni tume huru ya uchaguzi, matokeo ya rais kupingwa mahakamani, umri wa mbunge na mgombea binafsi.
“Kwa sababu taifa sasa hivi lipo katika hali tete, kuna matamshi ya aina mbalimbali, endapo tutafanya hivyo tutakuwa na Katiba ya mpito ya kati ya miezi sita hadi 12, itaturuhusu kufanya uchaguzi na baadaye watu wataenda kwenye kura ya maoni wakiwa wamepata elimu ya kutosha juu ya Katiba Inayopendekezwa.
“Hii itainusuru Tanzania yetu tunayoitaka kulikoni leo hii taifa kuingia kwenye kura ya maoni likiwa kwenye mparanganyiko mkubwa,” alisema.
Baada ya Jafo kuzungumza, Spika Makinda alisema suala hilo si utaratibu na litatolewa ufafanuzi jioni na waziri mkuu wakati akiahirisha Bunge.
Wakati akisema hivyo, baadhi ya wabunge wa upinzani waliendelea kusema kuwa alichofanya si utaratibu.
Hali hiyo ilionekana kumkera Makinda. “Muendeshe ninyi, njooni hapa mkae wote,” alisema kwa hasira na kuendelea:
“Kifungu cha 47 kinasema iwapo Spika ataridhika kwamba jambo hilo ni la dharura na lina masilahi kwa umma, basi ataruhusu hoja itolewe kwa muda dakika tano, na mjadala wa hoja utawezekana kama Spika ataridhika.
“Sasa kwa sababu Waziri Mkuu anafunga hotuba yake leo, hatulijadili hili swala, naomba msome kanuni na kuwepo na uvumilivu.”
Wakizungumza nje ya Ukumbi wa Bunge, Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia (NCCR Mageuzi), alisema vyama vya siasa chini ya Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) walishafanya makubaliano na Rais Jakaya Kikwete juu ya kupitisha mambo muhumu kabla ya uchaguzi mkuu.
Alisema walikubaliana kuwa kura ya maoni ifanyike baada ya uchaguzi mkuu na marekebisho ya Katiba yafanyike ili kuwe na Tume Huru ya Uchaguzi, mgombea binafsi, mshindi wa urais apate ushindi wa kuanzia asilimia 51 na matokeo hayo yaweze kupingwa mahakamani.
Mbatia alisema Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilisema ikipata BVR 15,000 ingeweza kutumia miezi minne kuandikisha wapigakura nchi nzima, lakini Serikali ikasema inaweza kutoa mashine 8,000 peke yake lakini hadi sasa zilizopo ni 250 pekee.
“NEC wameenda kuomba hizi mashine Kenya wakanyimwa, wameenda Nigeria, Malawi kote wamenyimwa, sasa kwa mtindo huu kuandikisha wapigakura kwa muda haiwezekani,” alisema.
JAJI BOMANI
Naye mwanasheria mkuu mstaafu wa Serikali, Jaji Mark Bomani, ameonya kuwa iwapo Katiba Inayopendekezwa ikipitishwa italigawa taifa na kusababisha machafuko.
Kutokana na hali hiyo, Jaji Bomani ameshauri ni vizuri Serikali ikasitisha kupiga kura ya maoni inayotarajiwa kufanyika Aprili 30 na kuendelea na uboreshaji wa daftari la wapigakura.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Jaji Bomani alisema kama viongozi waliopewa mamlaka hawatachukua hatua, taifa linaweza kuingia kwenye mfarakano mkubwa.
Alisema Katiba Inayopendekezwa imewagawa wananchi tangu wakati wa Bunge Maalumu la Katiba baada ya wajumbe kushindwa kuelewena na wengine kususia vikao na kutoka nje.
“Mambo yalianza kuharibika tangu wakati wa Bunge Maalumu la Katiba kiasi kwamba wengine walijitoa, hili lilikuwa doa kubwa kwa mchakato mzima, wale waliobaki waliendelea wakatoa Katiba Inayopendekezwa ambayo imezua mjadala.
“Kutokana na hali hii, binafsi kuna matatizo ambayo nayaona… kwanza ni makundi ambayo wengi wao wanaamini Katiba Inayopendekezwa ilitupilia mbali baadhi ya mambo yaliyopendekezwa na Tume ya Jaji Joseph Warioba, lakini wengine wanatishia kutoipigia kura,” alisema.
Alisema jambo hilo linasikitisha na si la kupuuza kwani Katiba ni sheria mama na msingi wa kuendesha nchi, lazima ipatikane Katiba nzuri inayoungwa mkono na wananchi wengi.
“Katiba inayopingwa na kundi kubwa la watu ni chanzo cha mfarakano kwenye nchi. Endapo inapigiwa kura nyingi za hapana au inapigwa upande mmoja wa Muungano, iwe Zanzibar au Tanganyika, basi hatima yake ni kuvunja Muungano. Je, ni sawa tufike huko?” alihoji.
Alisema iwapo kama nchi itafika katika hatua hiyo, itakuwa imeingia katika matatizo na uhasama mkubwa hali ambayo itasababisha kutokea kwa machafuko hayo.
“Tuweke muda wa mazungumzo ili tuafikiane, kwani Mtanzania wa kawaida anataka nini, hataki uchu wa madaraka bali maisha bora kwa kupambana na maadui wale watatu (ujinga, maradhi na umasikini), haya masuala ya idadi ya serikali ni ya viongozi,” alisema.
Akizungumza juu ya matumizi ya mashine za BVR, alisema Serikali na Tume ya Uchaguzi (NEC) imekurupuka kwa kutaka kuzitumia bila ya kuwa na maandalizi ya kutosha ikiwa ni pamoja na rasilimali fedha.
“Kura itapigwa mwishoni mwa mwezi huu, lakini sidhani mpaka hii leo uandikishaji bado unasuasua… naambiwa mpaka sasa watu walioandikishwa hawazidi hata milioni moja na tupo zaidi ya milioni 45. Je, hawa waliosalia wataweza kuandikishwa ndani ya wiki nne zilizobaki? Nafikiri itakuwa ni muujiza kufanya hivyo,” alisema.
VIONGOZI WA DINI
Akizungumzia kitendo cha baadhi ya viongozi wa dini kutoa maneno ya kashfa kama sehemu ya kuwashawishi waumini wao kupiga kura ya hapana, alisema kinapaswa kulaaniwa.
“Viongozi wa dini wana haki ya kuelimisha waumini wao, watambue waumini hao nao wana haki ya kukubali au kukataa ushauri huo wa viongozi wao na si kulazimishwa.
“Lazima tulaani jambo hili kama ambavyo tulifanya wakati ule wa Jaji Warioba pale alipokuwa akilaumiwa, tulikemea kitendo kile kwa nguvu zote,” alisema.

No comments :

Post a Comment