dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Thursday, May 28, 2015

Upinzani yataka majibu ya deni bilioni 800/- wanalodai makandarasi.

Msemaji Mkuu wa Kambi hiyo, Felix Mkosamali.
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imeitaka Wizara ya Ujenzi kutoa majibu ya deni la zaidi ya Sh. bilioni 800 inayodaiwa wizara hiyo na makandarasi katika bajeti ya mwaka 2014/2015.
 
Akiwasilisa hotuba ya Kambi hiyo kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2015/2016, Msemaji Mkuu wa Kambi hiyo, Felix Mkosamali, alisema katika mwaka wa fedha wa 2013/2014, wizara hiyo ilitengewa Sh. 662,234,027,000 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo, lakini hadi kufikia Januari 2014, madeni ya makandarasi na washauri yalikuwa Sh. 663,870,636.26.
 
Alisema mfano mzuri ni bajeti 2014/2015 wizara ilikuwa na madeni yaliyofikia Sh. bilioni 760 huku bajeti ya maendeleo kwa wizara na taasisi zake ikiwa ni Sh. bilioni 762.
 
“Kambi rasmi ya upinzani bungeni inamtaka waziri kueleza ukweli Bunge lako tukufu kwamba kwenye bajeti ya 2014/2015 ni fedha kiasi gani zimelipa madeni na fedha kiasi gani zimekwenda kwenye miradi ya maendeleo,” alisema.Mkosamali alisema hata kwa mwaka huu wa fedha, Bajeti ya Maendeleo ni Sh. 890,572,000.00 kwa wizara na taasisi zilizo chini ya wizara huku madeni yakiwa zaidi ya Sh. bilioni 800. “Hakuna uhalisia kati ya fedha za maendeleo zinazoombwa na madeni husika.”
 
Alisema wizara hiyo imekuwa kiandika hotuba ndefu kuwachanganya wabunge kwa kuonyesha barabara zilizojengwa miaka ya 80 na miaka 90 kama vile zimejengwa hivi karibuni.
 
Alisema wizara haijatoa ufafanuzi unaoridhisha juu ya fedha zinazotengwa na kilomita zinazojengwa, mfano wa Barabara ya Dar es Salaam – Chalinze – Morogoro (kilomita 200), sehemu ya Dar es Salaam Chalinze imetengewa Sh. bilioni 2.45. “Hakuna ufafanuzi kwani kilomita 100 haziwezi kujengwa kwa Sh. bilioni mbili tu.”
 
MADARAJA YALIYOAHIDIWA
Kambi hiyo ilisema licha ya mbwembwe nyingi za waziri, madaraja yaliyoahidiwa kujengwa mwaka 2014/15 likiwamo la mto Sibiti lililotengewa Sh. bilioni tatu, lakini fedha hizo hazijatolewa na Hazina na mkandarasi ameondoka eneo la ujenzi na Daraja la Kigamboni ambalo liliahidiwa kukamilika mwezi Juni, mwaka huu, ambalo linaonyesha ahadi haitatekelezeka.
 
BARABARA CHINI YA KIWANGO
Kambi hiyo ilisema licha ya wizara na hata Waziri Mkuu kujigamba kujenga kilomita 13,000 za lami katika awamu ya nne, zimejengwa chini ya kiwango na zinabomoka na kuharibika miezi sita au pungufu au mwaka mmoja baada ya matengenezo.
 
Alitoa mifano hiyo kuwa ni Dar es Salaam – Dodoma ambayo imebonyea upande wa kushoto na inatengenezwa kila wakati, lakini inaharibika, Bagamoyo – Msata, ambayo imeanza kuharibika kabla haijamalizika, Dodoma – Iringa, imejaa mashimo maeneo kadhaa na Dodoma – Mwanza hasa maeneo ya m lima wa Sekenke iliyobomoka muda mfupi mara tu ya kukabidhiwa serikalini.
 
UNUNUZI KIVUKO DSM-BAGAMOYO
Kambi hiyo ilikiponda kivuko hicho chenye kubeba abiria 300 kwa karibu Sh. bilioni nane, lakini kinatumia saa tatu kutoka Dar es Salaam hadi Bagamoyo.
 
“Ni jambo la ajabu kununua kivuko cha kizamani chenye spidi ndogo. Azam Bakhresa ana meli inayotoka Dar kwenda Zanzibar kwa muda wa dakika 90 tu na kinabeba abiria 500, ambacho kwa taarifa tulizonazo kimemununuliwa kwa kati ya Sh. bilioni nne hadi tano tu,” alisema.  
 
KUPUNGUZA MSONGAMANO DAR
Kambi hiyo ilisema inaamini juu ya ujenzi wa barabara zipitazo juu ili kuepusha kero kwenye maeneo ya Tazara, Moroco, Ubungo, Magomeni, Selander bridge na maeneo mengine yenye msongamano.
 
Hata hivyo, ilisema serikali haina nia ya dhati ya kuonyesha msongamano huo kwa kujenga angalau barabara moja inayopita juu.
 
BARABARA ZISIZOTEKELEZWA AHADI
Mkosamali alisema licha ya mbwembwe za uwasilishaji wa waziri wa bajeti hiyo, kila inapofikia mwaka wa uchaguzi, serikali imekuwa ikiahidi kujenga barabara kwa lengo la kupata kura, lakini haitimizi ujenzi wa barabara hizo.
 
Alitaja barabara hizo kuwa ni ya Nyakanazi, Kibondo, Kasulu, Kidahwe zenye urefu wa kilomita 310 ambayo ilikuwa ahadi ya Serikaliya awamu ya tatu na awamu ya nne.
 
Barabara nyingine ni Karatu – Mang’ola –Matala, ambayo iliahidiwa kujengwa kwa kiwango cha lami, lakini mpaka sasa haijajengwa pamoja na ahadi yake kutolewa mwaka 2010 na wananchi kuendelea kula vumbi.
 
Alitaja barabara nyingine kuwa ni Karatu – Mbulu (Kilomita 77), Arusha – Moshi – Himo –Holili (kilomita 140), Bunda – Kisorya –Nansio (kilomita 93) na Kilombero – Ifakara – Mahenge.
 
Nyingine ni Mpemba – Isongole (kilomita 51.5), Kalando- Meatu –Mto Sibiti –Singida na barabara za miji midogo ambazo zilitolewa ahadi ya ujenzi na Rais wa awamu ya nne za mji wa Karatu (kilomita 2), Kibondo Mjii (kilomita 1.5) na ujenzi wa lami Kondoa.
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment